Kuna vitu huwezi kuvijua mapema kwasababu ukivijua mapema utashindwa kuwa mnyenyekevu katika sehemu uliyopo sasa. Kule mahali Mungu anataka ufike wakati mwingine hatakuonesha mapema kwasababu ukijua mapema unaweza kuanza kuruka hatua nyingine.

Tukimuangalia Daud alikuwa mtoto wa mwisho wa baba yake, kaka zake walikuwa wanajeshi, yeye alikuwa mchungaji wa kondoo. Lakini Mungu alishamuandaa kuwa mfalme, hakujulishwa yeye wala ndugu zake unajua kwanini? Baba yake angejua huyu mtoto anakuja kuwa mfalme asingelelewa kwa namna ya kawaida, asingechunga kondoo angelelewa kama mfalme, lakini Mungu hakutaka iwe hivyo.

Kumbe Mungu anataka uwe mchunga kondoo kwa muda ili ujifunze unyenyekevu. Ili abadilishe mtazamo wako, Daud asingeweza kupambamba na Goliath kama hakuwahi kujaribu kupambana na simba na dubu. Yale mapambano kule machungani hayakuwa ya bure Mungu alikuwa anamuandaa na kumtengenezea mtazamo wa ushindi ili akija kukutana na Goliath aweze kuwaza kiushindi.

Usifikiri Mungu haoni unachopitia sasa, usimlaumu, usimlalamikie wewe endelea kutafuta ushindi. Huwezi kujua kusudi la wewe kupitia hapo ulipo hadi uvuke. Kuna mambo unaweza kupitia kwenye Maisha na usielewe maana yake hadi pale unaposhinda.

Usijione wewe ni wa kawaida kwasababu wewe upo machungani na wenzako wapo vitani, hapana. Tumia vizuri huko machungani ili uje kupata vitu vya kusema unapokuwa kwenye hatua nyingine kubwa Zaidi. Kaka wa Daud walitaka kumzuia asipigane na Goliath lakini Daudi akasema nilishapambana na Simba alietaka kumla mwanakondoo wangu, nilishapambana na dubu. Kwa shuhuda na mtazamo huo hata ndugu zake wakaanza kuona huyu sio mtu wa kawaida.

Wewe unachopitia sasa hivi badala ya kupambana wewe unalalamika embu badili mtazamo wako. Ukiwa mlalamikaji kuna sehemu hutaweza kufika, utaishia kwenye viwango hivyo hivyo ulivyo sasa.

Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

https://jacobmushi.com/kocha/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading