Habari ya leo ndugu Msomaji. Ni matumaini yangu unaendelea vyema katika mapambano yako ya maisha. Tunaendelea na mfululizo wa Makala za tabia kwasababu mafanikio yeyote yanaletwa na tabia mbalimbali zinazojengwa kwa kurudiarudia kila siku. Kuna vitu ambavyo hutakaa uvisahau maishani mwako hata ukiwa umelala kitandani unaumwa. Mfano ni silabu, a, e, i, o, u hizi wakati tukia chekechea na darasa la kwanza tulikua tunaziimba kila siku hivyo zikakaa katika ubongo wetu wa kumbukumbu na kutokuzisahau kabisa. Pia kuhesabu namba haiwezekana kwamba ukikaa muda mrefu sana bila kufanya hesabu utasahau. Tunaweza kutumia mifano hii kuzijenga tabia mbalimbali katika maisha yetu na tukajikuta tunafikia mafanikio makubwa sana. Embu jiulize ulishawahi kuamka asubuhi ukasahau kuswaki? Unafikiri ni kwanini? Jibu ni kwamba hua unarudiarudia kila siku. Hivyo pia unaweza kujenga tabia yeyote kwa kurudia rudia kila siku kuifanya.


Inawezekana una vipaji vizuri sana, inawezekana una zawadi nzuri na za pekee sana ndani yako, inawezekana una malengo na ndoto kubwa sana ndani yako. Lakini kitu kimoja kikakuangusha tabia zako zikakufanya ukashindwa kutimiza yale yaliyoko ndani yako. Nguvu za kipekee ulizonazo zinaweza kuharibiwa na tabia mbovu ulizonazo. Ni vyema sana ukajijengea tabia njema ambazo zitakufikisha kwenye mafanikio na kukufanya ubaki juu siku zote. Kwa hapa Tanzania tumekua tunawaona wasanii wa muziki wenye vipaji vizuri mno na sauti za kipekee sana wengi wao wakiishia katika utumwa wa madawa ya kulevya na uvutaji bangi hivyo kupoteza kabisa ule upekee walionao.

Tabia nzuri ni ngumu kuzijenga lakini zina manufaa makubwa sana tabia mbaya ni rahisi kuzijenga lakini zina matokeo mabaya sana kwenye maisha yako.
Leo tunakwenda kuitazama tabia ya Uvumilivu (endurance). Uvumilivu ni uwezo wa kusubiri jambo unalolitegemea au kuendelea kusonga mbele ili hali unapitia magumu, maumivu na mateso bila kukata tamaa ukiamini kua ipo siku yatakwiisha.
Tabia ya uvumilivu inahitaji kila kona ya maisha yetu. Kwenye mahusiano, kazi, biashara, umeomba Mungu au chochote kile unachokifanya lazima ukubali kua na moyo wa uvumilivu. Bila hivyo utajikuta unaishia njiani kwenye kila jambo unalolitaka. Hakuna kitu kirahisi na kinachopatikana kirahisi hivyo ni muhimu sana kujijengea tabia hii ya uvumilivu ikusaidie pale ambapo mambo yanakua magumu kwenye maisha yako na upande ule unapotia changamoto.

Watu wenye maono wana tabia ya uvumilivu. Watu wenye ndoto kubwa na malengo makubwa wana tabia ya uvumilivu. Haijalishi wanapitia ugumu kiasi gani au yale wanayoyapanga hayatokei wanavumilia na kurudia rudia kujifunza na kuangalia pia walipokosea.

Uvumilivu wako ndio unaonyesha ulikua unakihitaji kwa kiasi gani au ulikua hukihitaji kile ulichokua unakitaka. Haijalishi ukubwa wa changamoto unayopitia uvumilivu ni muhimu sana kwenye maisha yako. Kwa wale tunaosoma Biblia kwenye kitabu cha Ayubu tunamwona akipatwa na matatizo makubwa ya kupoteza mali, watoto pamoja na ugonjwa wa majipu mwili mzima. Lakini Ayubu hakukata tamaa kumcha Mungu wako kwakua tu hakumuona akimtetea katika kulinda mali au watoto wake au hata kumponya na magonjwa. Hivyo uvumilivu haunaga mwisho hakuna mahali utafika useme hapa sasa ni mwisho siwezi kuvumilia tena. Naacha hii biashara, au naachana na huyu mtu kwa kua nimechoka tabia zake.  Japo kwenye kuishi na watu lazima uangalie anaongeza kitu gani kwenye maisha yako kama anakuharibu au anaongeza vitu hasi unatakiwa umkimbie haraka.

 Watu wasio na uvumilivu wanalalamika na kulaumu juu ya yale yanaowatokea katika maisha yao. Wakipitia changamoto za mahusiano hua wanaishia kusema jinsi gani wenzao walivyo wabaya. Kwenye biashara hua wanasababu nyingi sana za kwanini wameacha.

Uvumilivu unaonyesha una Imani kiasi gani kwenye kile unachokifanya. Kama huna Imani na kile uanchokifanya ni Biashara huamini kama itakuwezesha ufikie mafanikio huwezi kuvumilia upitiapo changamoto. Kama Ayubu alivyoweza kuvumilia yote aliyopitia ni kwasababu alikua na Imani na Mungu wake. Hata leo unaweza kutazama kile unachokifanya ni misukosuko gani inaweza kukufanya wewe uache kabisa hicho na usirudie tena kufanya?

Uvumilivu unaonyesha unakipenda kwa kiasi gani kile unachokifanya au yule unaemvumilia. Mfano kwenye mahusiano mengi ya sasa unaweza kuachwa tu kwakua umeshidnwa kumhudumia mpenzi wako. Kama mtu anaweza kukukimbia kwakua tu umekosa pesa kidogo basi huyo hakua na upendo na wewe. Kama kazi unayoifanya unaipenda haijalishi unapitia nini utaweza kuvumilia tu. Ndio maana tunasema fanya kile unachokipenda kwakua utaweza kuvumilia wakati wa magumu.
Asante sana kwa kufuatana nami hapa wengi hawana tabia hii ya uvumilivu hata kwenye kusoma ndio maana wengi wanaposoma Makala na kuona ni ndefu sana wanaishia njia wewe umeweza kusoma hadi neno hili la 706 una moyo wa kipekee sana na utaweza kufikia mafanikio katika kile unachokifanya.

Karibu sana
Nguvu ya Tabia
0654726668
Jacob Mushi 2016

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading