Tag Archives: mafanikio

535: Yanapokuja Usiyoyatarajia…

Weka Email Yako Hapa Upokee Makala Kama Hizi

Kwenye maisha yetu ya kila siku kuna mambo mengi hutokea na kwa namna moja au nyingine mambo haya yanatuathiri moja kwa moja au kwa sehemu. Kila siku kuna mtu atakuwa amezidiwa na akakimbizwa hospitali, kuna ambaye atafiwa, kuna ambaye atapata ajali, kuna ambaye ataibiwa, kuna ambaye atapoteza pesa, kuna ambaye atafanya uzembe Fulani, na mengine mengi sana.

Haya ni mambo yanayotokea katika maisha yetu ya kila siku. Kwa bahati mbaya sana haya mambo mengi hatuna uwezo wa kuyathibiti. Huwezi kuzuia mtu mwingine asiwe mgonjwa asiibiwe, asipate ajali, na hivyo basi yanapotokea yanakuwa ni mambo ambayo tusiyoyatarajia.

Leo natamani kuona wewe unakuwa mtu mwenye furaha na maisha yako yanakuwa bora lakini bado haya mambo yatakuwa yanaingilia furaha yako ya kila siku, mipango yako binafsi,  na hata yale mambo ya muhimu.

Inawezekana wewe ni dereva mzuri sana, hujawahi kupata ajali, hujawahi kuandikiwa kosa lolote hata la bahati mbaya na askari wa usalama barabarani. Siku moja asubuhi unaamka ukiwa na mipango yako mizuri sana, unaingia barabarani halafu unajikuta upo kwenye foleni ambayo itakuchelewesha labda kwa masaa kadhaa. Foleni ile imesababishwa na dereva moja mzembe ambaye amepata ajali. Akaathiri ratiba zako zote za siku nzima. Ubora wako kwenye udereva hapo hautakusaidia chochote.

Unachotakiwa kwenye maisha yako ya kila siku, ni kujiandaa kwa yale ambayo hayatarajiki. Hakuna anaemka asubuhi na kutarajia kwenda kupata ajali, au kuibiwa, au hata kuumwa. Kila mmoja anatarajiwa mambo mazuri. Lakini mambo mabaya hayaachikuja. Yanakuja kwasababu ndio asili ya dunia. Kila saa kuna mambo mengi yanaendelea na yanaweza kukuathiri wewe moja kwa moja au kwa sehemu.

Unachopaswa kuelewa ni kutarajia yasiyotarajiwa. Unapanga mambo yako lakini unaweka akili kwamba lolote pia linaweza kutokea likasababisha hii mipango yako ikakwama. Wakati mwingine sio lazima ujiandae na mabaya, lakini unapaswa tu kuelewa yanaweza kutokea popote na yakakukuta bila kujalisha wewe ni mwadilifu kiasi gani. Ukiwa na hili kichwani mwako hata itokee nini huwezi kuumizwa sawasawa na Yule ambaye akili yake aliiweka kwenye upande mmoja pekee. Kama vile anaishi peke yake hapa duniani.

UNAPOTARAJIA MAMBO MAZURI MAKUBWA KWENYE MAISHA YAKO USIACHE PIA KUTARAJIA NA YASIYOTARAJIWA.

Ni mimi rafiki Yako wa Siku Zote Jacob Mushi.

534: Ni Nini Kitafuata?

Miaka michache iliyopita kuna vingi vilivyogunduliwa kipindi hiki havikuwepo kabisa na vingine hata havikudhaniwa kama vingewezekana. Kilichofanya haya mambo makubwa tuyaonayo sasa yaweze kutimia ni kile kitendo cha watu kutaka kujua wanawezaje kuleta suluhisho kwenye jamii.

Ni muhimu sana kama unataka kuwa mmoja wa watu ambao wataleta mabadiliko kwenye dunia hii basi uweze kujiuliza swali hili,Ni kitu gani kitafuata baada ya hiki? Kwasababu hata hivi vilivyogunduliwa havitadumu milele.

Ukiweza kuwa na majibu ya ni nini kifuatacho kwenye fursa mbalimbali wewe utakuwa mtu pekee ambaye anakwenda mbele zaidi ya mawazo ya wengine na kuleta mabadiliko. Inwezekana, chochote kile ambacho umeweza kukiwaza kwenye akili yako kinawezekana kufanyika na kikawa halisi.

Usiogope Kuwa mtu wa kuchukua Hatua,

Kuwa mtu mwenye uvumilivu,

Kuwa mtu ambaye anajifunza mara kwa mara,

Kuwa mtu ambaye anajiuliza maswali mengi na kuyatafutia majibu.

Usiwe mtu mwenye tamaa ya mafanikio ya haraka.

Usiwe mtu ambaye anataka kuona wengine wanaumia ili tu yeye atomize kile anachoona kinafaa.

Usiwe mtu asiejali binadamu wengine (Hii itakusaidia usije kutengeneza vitu ambavyo vinaweza kuangamiza wanadamu).

Yapo mengi ambayo ningeweza kukwambia, Usipoteze Imani yako kwamba inawezekana, pamoja kwamba wapo wengi watashindwa kuona vile unavyoona wewe hiyo sio sababu ya wewe kuacha.

Mafanikio ni Haki Yako.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi.

Mafanikio ni Mchakato.

Nilipokua sekondari tulitumia barabara mbaya sana kuelekea shuleni kitu kilichofanya safari iwe ya kuchosha sana na yenye kuchukua muda mrefu sana.
Kipindi hicho barabara nzuri ya lami ilikua ikitengenezwa, kila nilipokua nikisafiri kwenda na kurudi shule nilitumia muda huo kujifunza juu ya ujenzi wa barabara!

Ujenzi wa barabara unapoanza unaudhi sana kwani miti hukatwa , udongo huchimbuliwa na miamba huvunjwa, ni kazi isiyotamanisha kuiangalia inapoanza,

Na watu wengi hawapendi kusafiri barabara inapojengwa maana safari huwa ya kuudhi na kuchosha sana!
Ujenzi wa barabara ya lami ni mfano wa mtu anayepitia mchakato kuelekea mafanikio,
Mambo yanayomtokea mengi huwa ya kuudhi na lengo ni kumuimarisha na mengine huja ili kumkatisha tamaa,
Dharau,kejeli,njaa,magonjwa,kuumizwa,kutokukubaliwa na mengine mengi yanayoudhi!
Mara nyingi watu humuepuka na hukwepa kuwa naye karibu kwa kuhofia shida anazopitia!
Na marafiki wengi waliokosa utu humuumiza mtu aliye ktk mchakato kwa kutokujua kesho yake kutokana na anayopitia!
Mfano wa barabara ikishakamilika kila mtu hufurahia na hutamani kuitumia na kuielezea jinsi ilivyojengwa na ilivyo bora!

Na mtu akishafanikiwa kufikia aliyoandikiwa ndipo kila mtu hutamani kuwa naye na hutamani kila mtu ajue kuwa anajuana nae!

Ili uwe mtu bora lazima upitie hatua mbalimbali mfano wa barabara ijengwayo,
Lazima upitie MCHAKATO ndio uwe bora zaidi!
Watu wa kawaida hawapitiagi hatua za ukuaji za kimchakato!

NB. Usiogope mchakato, usiogope watu kukuacha ukiwa mchakatoni
Songa mbele!

Uwe mtumishi wa MUNGU,una huduma,una vipaji, una ujuzi flani, lazima upite kwenye mchakato ili uwe bora!

Watu wote bora tunaowasoma kyk Biblia walipitia michakato tena migumu mnoooo!
Tukiwatazama kina Yusuphu,Musa,Yohana,Petro,Ibrahimu ni mifano mikubwa!
Tumwangalie MUNGU na tusonge mbele

#Noturning back
By Theofrida Gervas

TUSEMEZANE 425; MAMBO 37 YA NILIYOJIFUNZA MWAKA 2018.

Habari Rafiki nimekuwa na utaratibu wa kukuandikia mambo niliyojifunza kila mwaka na mwaka huu hii ndio mojawapo ya mambo ya muhimu kabisa niliyojifunza na ningependa nikushirikishe na wewe.

1 Hakuna kisichowezekana usiipe akili yako kikomo au kusema mimi siwezi hiki.

2 Usipofanya maamuzi magumu hutatoka hapo ulipo hata siku moja.

3 Penda kujaribu vitu ambavyo hujawahi kufanya kwasababu ndio njia pekee ya kukuwezesha wewe upande viwango kwenye unachokifanya na pia kujua vitu vipya.

4 Onesha Tabasamu popote ulipo huwezi kujua litamsadia nani.

5. Maisha Yako sio maonesho, chochote ambacho hakimsaidii mtu hakuna haja ya kukionesha hadharani, mfano Maisha yako binafsi ya ndani. Onesha vile vya muhimu sana na vinavyoweza kuwasaidia wengine.

6. Kelele ni nyingi sana wanaofanikiwa ni wale tu walioweza kuzishinda kelele na kuendelea na mambo yao.

7. Ukianza kufanya mambo makubwa wataanza kuja kukushauri hata watu ambao hukutarajia na wengi wao watakuwa wanakupa ushauri wa bure. Usipendelee ushauri wa bure kutoka kwa mtu alieibuka tu huko baada ya kuona unapaa.

8. Usitafute Watu Sahihi, endelea kufanya vitu sahihi waliosahihi watakuja tu wenyewe katika njia.

9. Usipoteze muda wako kutoa maoni sehemu ambayo unajua hakuna anaepokea maoni hayo.

10. Upendo Unaponya.

11. Tenga Muda wa Kuwa Pekee Yako upate utulivu wa kutosha Kila Wakati Unapoona Mambo hayaeleweki utapata majibu mengi sana kuliko hata pale unapowaeleza wengine.

12. Usiishi Maisha hapa duniani kama utarudi kuishi tena mara ya pili. Usifanye jambo tu pale unapojisikia kufanya. Jisukume Zaidi, fanya Zaidi, kila kitu weka Zaidi.

13. Usitegemee Huruma za Wengine Kuendesha Maisha Yako.

14. Hakuna anaeyawaza Matatizo Yako Na kuyapa kipaumbele kuliko wewe mwenyewe.

15. Kama huna muda wa kufuatilia Maisha yako, Umeshayapoteza Maisha Yako Anza Kuyatafuta, Maana hata Unapokwenda Huenda Hujui.

16. Msimamo ndio utawafanya watu wafanye kazi na wewe, usiwe mtu wa kubadilika badilika kila wakati.

17. Kama huna fedha Jiamini kama unazo, Ukiwa nazo Kuwa kama Huna.

18. Usimweleze kila mtu matatizo yako kwasababu hakuna anaeyajali kuliko wewe mwenyewe.

19. Watu wakiamua kuondoka kwenye Maisha yako sio wakati wote wewe ndio una matatizo mara nyingi wao ndio wanakuwa wamejiona hawastahili kuendelea kuwa na wewe.

20. Watu Wakishusha Thamani wewe usiungane nao na kujiona huna thamani, aliekuumba amekupa thamani.

21. Unapopoteza Kitu usiumie jifunze kwamba hakuna kinachodumu Zaidi ya akili ya kutafuta vitu, hivyo tafuta kingine bora Zaidi.

22. Usibebe huzuni ndani ya moyo wako, lolote ambalo limeshatokea haliwezi kurekebishika liache kama  tukio.

23. Wale ulikuwa unawapenda wakaondoka hapa duniani ni vyema kuwaacha kwa amani na wewe ukaendelea kufurahia Maisha hapa duniani. Si vyema sana kuendelea kuwakumbuka na kuwa na huzuni sana.

24. Usifanye maamuzi kwa kuongozwa na tamaa Ongozwa na Upendo. Tamaa huisha Upendo hudumu.

25. Usisubiri Kitu kiondoke kwako ndipo uanze kuona thamani yake.

26. Kila Siku unapewa Tsh 86,400 lakini hujui na unazitumia kidogo sana au kwenye mambo yasiyo na maana. Huu ni muda unaopewa kila siku (sekunde 86,400). Wewe huwa unazitumiaje pesa hizo?

27. Ipe Thamani ya fedha dakika yako moja na usikubali kuipoteza au kuichezea pesa hiyo kwenye jambo lolote lisilo na umuhimu kwenye Maisha yako.

28. Usipokuwa mchoyo na muda wako hakuna atakaeujali au kukuonea huruma.

29. Kutokujua maana ya Maisha kumewafanya wengi waishie kwenye mbio za kufanya vitu ili waonekane na wao wamefanya bila kujua kwanini wanafanya.

30. Angalia sana unavyoongea au kuwafanyia watu usiowajua kwani mara nyingi hizo kuwa ndio tabia zako za kweli.

31. Huwezi kuishi Unavyotaka kama huna pesa za kutosha, endelea kutafuta pesa, tengeneza mifereji Zaidi ya pesa.

32. Hekima ya masikini haisikilizwi, maana yake ukiwa masikini unadharaulika, hivyo basi njia ya kuondokana na dharau ni wewe kutafuta pesa katika njia sahihi.

33. Asikudanganye mtu eti huwezi kufanikiwa katika njia sahihi, endelea kupambana kwasababu wenye njia zisizo sahihi ndio wale wenye pesa lakini hawana furaha.

34. Pesa itakupeleka sehemu ambayo Huwezi kwenda na Miguu.

35. Huwezi kumtumikia Mungu kwa mali zako zote kama huna mali, hivyo tafuta mali kwa bidii sana.

36. Maisha Yako Ni alama hakikisha unaacha alama kwa watu kwa kuwatendea mema.

37. Andika yale unayotaka kuyafanya ndipo uanze kuyafanya hii itakusaidia kujua ni kipi umefanya na kipi hujafanya. Fikiria kwenye karatasi, chochote unachokifikiria kiandike.

Mambo haya nimejifunza kwenye hatua mbalimbali nilizochukua kwenye Maisha yangu kwa mwaka 2018 pia niliyojifunza kwa wengine. Tuendelee kuwa pamoja tena na tena ili kujifunza mengi Zaidi mwaka ujao.

Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

398: Kuwa Mkweli Kwako Kwanza.

Unaweza kuwadanganya wengine lakini huwezi kujidanganya wewe mwenyewe. Ndani ya nafsi yako unajua ukweli ni upi. Ndani ya nafsi yako unajua kama Maisha unaigiza au ni kweli kile ambacho unakionesha.

Mojawapo ya vitu vinavyowatesa wengi ni kujaribu kujidanganya wenyewe, unakuta unajua kabisa Matendo yako hayaashirii kabisa kile ambacho unataka lakini unajitia moyo wa uongo kwamba upo siku utafanikiwa.

Unasema utafanya jambo Fulani lakini Matendo yako ni tofauti kabisa na Maneno yako. Unasema utafanya mazoezi lakini ukifika wakati wa mazoezi unaleta sababu nyingine Nyingi zisizo za msingi. Unasema utasoma kitabu lakini kila wakati unajikuta husomi.

Anza kujitazama hivi ni kweli unazo bidii ambazo watu wanakusifia au huwa unajidanganya? Ni kweli wanapokuita wewe ni mpambanaji ukijiangalia kweli Matendo yako yanaridhisha kuitwa mpambanaji? Mbona kama ni uongo hivi? Mbona kama wanasema tu ili kukutia moyo?

Wewe  mwenyewe moyo wako unakubali zile juhudi unazoweka? Kama wewe moyoni hujaona kama umefanya vizuri wengine nje wakikusifia basi inakuwa haina maana sana. Wewe mwenyewe ndio una majibu ya ukweli hasa kwenye sifa ambazo wanakupa wengine.

Kuwa mkweli kwako Rafiki usikubali Matendo yako yadanganye. Ukisema unasoma kitabu soma, ukisema unafanya mazoezi nenda kafanye mazoezi. Fanya kile ambacho unasema utafanya, Usiishie kusema tu chukua hatua.

Kila mtu anataka na anatamani kuwa mtu Fulani lakini ni wachache sana wanafanya ili wewe yule mtu ambaye wanatamani kuwa. Usikubali kuishia kutamani na kutaka, ingia katika hawa wachache ambao wanachukua hatua za ukweli kila siku ili kuzifanya Ndoto zako ziwe kweli.

Usije kuishia kua mtu wa Maneno badala ya mtu ambaye wengine watakuja kutamani kufika pale ambapo umefika. Usikubali kujidanganya, usikubali kuridhika na juhudi kidogo ambazo umeweka. Nenda hatua ya ziada, tumia uwezo Mkubwa ndani yako.

Mafanikio yanawakuta wale wachache ambao wanamua kujitenga na wengi ambao ni waoga lakini wana maneno mengi sana. Achana na watu wenye Maneno kaa na watu ambao wanachukua hatua. Una nguvu una uwezo, una kila sababu ya kufanikiwa.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

HEKIMA YA LEO: Usiyafanye Maisha Yako Kuwa Magumu (Sehemu ya 2)

Ugumu wa Maisha wa Kujitakia.

Ni vizuri ukatambua kwamba ili uweze kufika viwango vya juu Zaidi ya hapo ulipo sasa hivi lazima ukubali kufanya maamuzi magumu. Maisha yako hayatakiwi kuwa magumu Zaidi ya inavyotakiwa, wewe mwenyewe kuna sehemu umesababisha kuongezeka kwa ugumu. Kushindwa kufanya maamuzi magumu lazima itakugharimu ugumu Zaidi wa Maisha yako.

Upo kwenye mahusiano ambayo binafsi unayaona ni mabovu kila siku mnagombana ukishindwa kufanya maamuzi magumu mapema. Jiandae kabisa kuja kuwa na Maisha magumu Zaidi kwenye ndoa. Ni lazima ukubali kufanya maamuzi magumu ili kutengeneza Maisha ambayo sio magumu kuliko inavyotakiwa kwenye ndoa yako.

Hautaki kuweka akiba, kila fedha unayopata inaingia kwenye matumizi yote jua kabisa unajitengenezea ugumu wa Maisha yako muda ambao sio mrefu sana. Lazima ukubali kujenga tabia ya kuweka akiba na uweze kupunguza matumizi ya hovyo ya pesa.

Umekubali mwenyewe kujiingiza katika michezo mibaya ya kubeti halafu unategemea Maisha yako yaje kuwa kama ya mtu mmoja hivi maarufu. Ndugu yangu unapoteza muda, ili Maisha yako yawe na unafuu lazima ukubali kuwekeza katika vitu ambavyo vinazalisha. Lazima ukubali kuwekeza katika vitu ambavyo vinaongeza thamani kwa wengine.

Ugumu wa Maisha ndio ni kipimo cha akili kwasababu hapo ndipo unatakiwa ujue kufanya maamuzi sahihi ya kukutoa huko kwenye ugumu. Kama utaendelea kubaki kwenye ugumu huo wa Maisha maana yake ni kwamba wewe akili yako ndio umeipima sasa ilivyo. Lazima ukubali kufika mahali unasema sasa basi, hii hali siitaki tena kwenye Maisha yangu. Aina hii ya shida sitaki tena kuisikia, sitaki tena kukopa pesa za kula, sitaki tena kukopa pesa nikalipe madeni. Lazima useme sasa basi nataka nitoke nisogeee viwango vingine.

Ugumu wa Maisha wa kujitakiwa ni kuamua kuingia kwenye Maisha ya kuiga wengine. Mfano wewe una marafiki zako wote wakiona simu mpya imetoka lazima wanunue cha ajabu ni kwamba wewe hujui hata pesa wanatoa wapi lakini wewe upo tayari ukakope ili ufanane nao. Ndugu yangu hapo unajitengenezea ugumu wa Maisha mwenyewe.

Ugumu wa Maisha wa kujitakia ni pale unapoishia kusema sina mtaji, sina mtaji wakati unajua kabisa hilo neno sina mtaji haliwezi kukupa mtaji. Unaona aibu kuanza biashara kwa shilingi elfu 20 kwasababu itaonekana ni ndogo sana. Maisha yakiwa magumu hapo umejitakiwa mwenyewe, ni bora upate faida ya shilingi elfu mbili uliyotafuta mwenyewe kuliko elfu kumi uliyopewa bure.

Ugumu wa Maisha wa kujitakia mwingine ni pale unaposhinda kwenye mitandao ya kijamii kutwa kuchwa ukitoa maoni kwenye kurasa za udaku bila kujua hakuna anaejali Maisha yako wewe. Huna biashara yeyote unayofanya lakini kila siku unapata hela ya kununua vifurushi vya kufuatilia udaku. Makala kama hizi za kukufungua ukikutana nazo hausomi hata kidogo. Lazima ujitengenezee ugumu wa Maisha.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Chukua Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

HATUA YA 345: Mambo Ambao Wengi Wanakwepa Kufanya.

Kwenye dunia kila mmoja analipwa kwa thamani anayoitoa. Aina ya Maisha unayoishi ni kutokana na thamani unayoipa dunia. Mshahara unaolipwa ni thamani unayoitoa kwa bosi wako. Makossa utakayokuwa unafanya ni kusahau kwamba thamani inaongezwa, na kama inaongezwa basi ujue hiyo uliyonayo kuna kipindi itashuka kama isipoongezwa.

Yapo Mambo Ambayo unapaswa Kufanyia kazi Kila Wakati kwenye Maisha Yako.

#Kuwa Bora Kila Siku kwa Kujifunza na Kusoma Vitabu.

#Fanya Kazi Kwa Bidii Kuliko Wengine Wote.

#Hakikisha Unatoa Nguvu Zako kwenye Jambo Unalotaka Likuletee matokeo.

#Huwezi kufanya Kila Kitu Bali kuna mambo Machache Ukiyafanya Yanaleta Matokeo Makubwa. Chambua mambo ambayo mar azote ukiyafanya hukuletea matokeo makubwa na uwe unayafanya kwa bidii sana.

#Tunza Muda wako, usikubali  kutumia mitandao ya kijamii hovyo, kupoteza muda kutazama Tv, kupekua vitu visivyo na msaada kwako.

#Tenga Muda wako Na wale watu ambao unawapenda na kuwajali. Kwenye dunia ya sasa ni rahisi kuona mtu amemuweka mtu kwenye mtandao na kusema amemmiss lakini hajathubutu kumpigia simu na kuongea nae. Usikubali watu wa karibu wakose uwepo wako kwenye Maisha yao.

#Tengeneza timu ya watu ambao mna Ndoto zinazofanana na mtakuwa na umoja msikamane hadi mfikie mafanikio makubwa. Hii ndio kampani yako na mara nyingi utakuwa unapata muda wa kukaa nao Zaidi. Haina maana usiwe na aina nyingine ya marafiki lakini hawa ni watu ambao mtakuwa mnashirikishana mbinu mbalimbali za kufanikiwa kwenye kile mnachokifanya.

 

#Washirikishe wengine maarifa. Unaweza kumpa mtu zawadi ya nguo atavaa itachakaa, unaweza kumnunulia mtu chakula atakula kitaisha, lakini ukimpa mtu zawadi ya maarifa hataweza kukusahau kamwe kama atayafanyia kazi na Maisha yake yakabadilika. Njia pekee ambayo unaweza kumsaidia mtu ni kumshikirisha maarifa unayojifunza kwenye Usiishie Njiani Academy.

 

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio… https://jacobmushi.com/patavitabu

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog ….. https://jacobmushi.com/jipatieblog

Karibu Usiishie Njiani Academy https://jacobmushi.com/whatsapp/

HATUA YA 342: Unaemngoja Anakungoja Wewe.

Inawezekana kuna mtu unamngoja aje afanye jambo kwenye Maisha yako ili yabadilike. Inawezekana kwenye akili yako unasubiri ipo siku mambo yatakaa sawa na kuwa marahisi Zaidi ya sasa. Inawezekana pia kuna muujiza Fulani unautegemea kwenye akili yako utokee ndio kila kitu kibadilike kwenye Maisha yako.

Napenda kukwambia Rafiki huyo unaemngoja afanye yote hayo anakusubiri wewe uchukue Hatua ndio aonyeshe ushirikiano na wewe. Ukweli ni kwamba hakuna mahali umeambiwa hali itakuja kuwa nzuri hata kama umeahidiwa hivyo hali haitakuwa nzuri kwako kwa kuisubiri. Hakli itakuwa nzuri kwa wale ambao wanachukua Hatua kila siku kwenye Maisha yao.

Kipindi pekee ambacho muujiza ulikuwa unamfata mtu ni kile cha Yesu pekee. Huku kwetu sasa hivi unapaswa kufanya vitu na ukutane na muujiza wako Njiani. Lazima uamue kabisa kwamba nakwenda kuchukua Hatua hii na hadi nione ile Ndoto yangu imeanza kuwa kweli.

Usijidanganye hata siku moja kwamba hali itakuja kubadilika, hakuna hali inayobadilika bila ya kubadilishwa ndugu yangu. Lazima ukubali kuhusika katika mchakato wa mabadiliko kwenye Maisha yako. Ukiendelea kubaki hapo unasubiri muujiza na mabadiliko ambayo hujayafanyia kazi ni sawa na anaesubiria kwenda kuvuna kwenye shamba ambalo hajapanda.

Unajua ombaomba wa barabarani hata ikitokea siku amepewa pesa nyingi sana za kutosha kwenye kufanya aondoke kwenye uomba omba bado atarudi tena kesho akitegemea atakuja mwingine ampe nyingi tena Zaidi. Usikubali akili yako iwe kama ya mtu wa aina hii. Unapaswa kujua namna ya kutengeneza Maisha yako mwenyewe bila kutegemea mabadiliko ambayo yanakuja yenyewe.

Labda nikwambie kwamba mimi nilipokuwa mdogo tulikuwa na tabia ya kwenda kupita kwenye mashamba ya watu na kukusanya mabaki ya mahindi baada ya kuvunwa. Ukweli wa Maisha ya wengi yako hivi. Hata mwaka ukiwa wa mavuno mengi bado hawafaidi chochote kwasababu wao wanasubiria masazo ya wale waliovuna. Sasa usitegemee waliovuna wakubakishie masazo mengi kwasababu tu walivuna mahindi mengi.

Lazima ukubali kuwa mtu anaechukua Hatua na kutetea Maisha yake. Toka hapo ulipo Rafiki yangu. Usikubali kubaki sehemu moja muda mrefu, hakikisha unakuwa bora kila wakati. Hakikisha unaongezekana viwango.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

HII NDIO NJIA YA PEKEE YA KUISHI MILELE.

Kungekuwa hakunaga kufa kwa namna ninavyoona wanadamu hasa wa Africa wangekuwa wavivu sana kuliko viumbe wengine wote. Nadhani kungekuwa hakuna ambaye anajishughulisha sana kwasababu hakuna kinachomfanya afikirie mbali. Kifo kipo ili kuongeza thamani ya uhai wa mtu. Kama kungekuwa hakuna kifo thamani ya uhai ingekuwa ni ndogo sana. Wandamu wangekuwa hawajali sana kama ambavyo sasa hivi baadhi wanajali na kufanya mambo makubwa. Mfano unaumwa na unajua utapona tu, una njaa lakini unajua ipo siku utapata chakula, hakuna ambaye angejali sana. Lakini mtu akizidiwa atakimbizwa hospitali ili kuokoa Maisha yake. Ukikosa chakula utafanya bidi kukitafuta ili usije kufa njaa.

Kifo kipo kutufanya kufikiria ni aina gani ya Maisha tunataka yaendelee kuwepo hapa duniani baada ya sisi kufa. Watu waliokosa matumaini ya Maisha ndio hawajali chochote kuhusu kesho yao wala ya baada ya wao kuondoka hapa duniani.

Kama kila binadamu angeweza kutambua kile ambacho kipo ndani yake na akaweza kukiishi katika uwezo wake wa juu sana basi dunia hii ingekuwa sehemu nzuri sana ya kuishi kuliko hapa tulipo sasa. Nikiwa na maana kwamba kuna watu wengi sana wameondoka duniani na vitu vingi sana vizuri mno vilivyokuwa ndani yao.

Kuna matatizo tunayapitia sasa hivi kumbe kuna mtu mmoja alishazaliwa ili aje kuleta suluhisho lakini akaondoka bila ya kutambua. Kuna changamoto nyingi watu wanapitia maeneo mbalimbali duniani inawezekana kabisa wewe unaesoma Makala hii kuna kitu kipo ndani yako ukiweza kukigundua utaleta msaada mkubwa kwa wengi.

Kila jambo ambalo unalifanya kila siku lina matokeo yake kwa baadae. Matokeo yanaweza kuwa ni kusahaulika kabisa kama uliwahi kuwepo hapa duniani ama kukumbukwa daima. Wapo watu wengi sana ambao historia zao zinatumika kama mifano kutokana na aina ya Maisha waliyoishi. Wapo waliofanya maovu kupindukia na wapo waliofanya mambo mema.

Mojawapo ya watu ambao wameweza kuendelea kuishi pamoja na kwamba miili yao hatunayo tena hapa duniani ni Wanamuziki waliofanya kazi zao kwa ubora wa hali ya juu mfano ni Bob Marley, Wapo wagunduzi wa vitu vingi ambavyo tunatumia sasa. Wapo viongozi wa kisiasa, waandishi, wanafalsafa, waigizaji, wachezaji na wengine wengi ambao unawafahamu. Ukweli ni kwamba hata wewe unaweza kuja kuwa mmoja wa watu ambao kazi zao hazitasahaulika hapa duniani.  Unachotakiwa kufanya ni kugundua ni nini kipo ndani yako na uanze kukiishi na kufanya kwa ubora wa hali ya juu.

Kila mmoja ana uwezo mkubwa sana ndani yake. Wanadamu pekee ndio tuliopewa uwezo wa kugundua vitu mbalimbali. Kwa kutazama kule ulipotoka hadi ulipo sasa unaweza kugundua kwa urahisi vitu gani ambavyo ulikuwa unapenda kuvifanya na ukivifanya vinakuwa na matokeo mazuri sana na moyo wako unasikia furaha.

Hakikisha Unafanya Vitu Hivi.

Jigundue Wewe ni nani.

Ili uweze kupata kitu ambacho utakisimamia na kukipigania hadi unakufa lazima ujue wewe ni nani, ulikuja hapa duniani kufanya nini, na unatakiwa ufike wapi. Huu ndio mwanzo wa wewe kuweza kuishi milele kwa kupitia yale ambayo yaliyowekwa ndani yako.

Chochote Unachokifanya Kifanye kwa Ubora wa Hali ya Juu Sana.

Ukikutana na fursa ifanye kwa ubora wa hali ya juu kiasi kwamba watu wakija waweze kujua hii kazi imefanywa na wewe. Popote unapopita hakikisha kunabaki na alama yako. Kwasababu wewe ni wa pekee basi upekee wako uonekane kwenye kazi za mikono yako.

Usijiweke Wewe Mbele Weka Mbele Kazi Zako na Kuwasaidia Wengine.

Kikubwa ili uweze kubakia na kumbukumbu ya kudumu wekeza nguvu zako katika kuwasaidia watu na sio kwa maslahi yako wewe binafsi. Wapo wengi sana wanahitaji hicho kilichopo ndani yako, endelea mbele ipo siku wengi wataanza kuona thamani ya kile kilichopo ndani yako.

Anza na Mtu Mmoja na Hakikisha Kile Unachokifanya Kimeweza Kumsaidia Hadi Akaridhika.

Usikimbilie kutaka kila mtu aanze kukujua mapema sana, anza na mtu mmoja hakikisha umeweza kumsaidia matatizo yake. Huyu mmoja ndio atakuwa zao la watu wengine wengi nyuma yake. Kama unaimba basi embu imba mtu mmoja akuelewe, kama unaandika andika hadi mtu mmoja akuelewe na asaidike na maandishi yako. Kama unafundishia fundisha mtu mmoja ahadi aweze kufanikiwa. Kama unatatua tatizo tafuta mtu mmoja mtatulie tatizo lake hadi aridhike kisha uanze na wengine na wengine.

Fanya Kila Siku

Ukishajua unatakiwa kufanya nini hapa duniani basi hakikisha kila siku kuna kitu unafanya ambacho kinaongeza thamani yako. Iwe ni kujifunza, kufanya utafiti, na mengine ambayo utayafahamu.

Jifunze Sana Kuhusu Kile Unachokifanya.

Hakikisha unachimba sana kwa undani kile unachokifanya hakikisha unajua wengi waliofanikiwa wamepitia njia gani. Ni vitu gani hasa ukivifanya vinaleta matokeo, ni mambo gani wengi walifanya na wakafeli. Usikubali kujua vitu vichache wakati una uwezo wa kujua vitu vingi.

Usipoteze Muda wako kusikiliza Kelele za Nje.

Duniani kuna kelele nyingi kuna watu wengi ambao wapo tu wao hawajatambua kwanini wapo hapa duniani. Kazi yao kubwa ni kufuatilia watu wanafanya nini ili wawavunje moyo. Wengine wanaweza kuwa marafiki, ndugu, na wengine hata usiowajua kabisa, watakuja tu na kuanza kukuelekeza jinsi ya kufanya. Wataanza kukukosoa na kusema hata wasioyajua. Usipoteze muda wako weka nguvu zako kwenye kile ambacho umeamua kufanya.

Jambo ambalo unatakiwa kutambua ni kwamba ili uweze kutengeneza historia ambayo itaishi milele hapa duniani unapaswa kuweka nguvu nyingi sana katika kuwasaidia watu. Usijifikirie wewe wafikirie wengine. Kwenye Biblia kuna neno linasema “Yeyote atakaekubali kuyapoteza Maisha yake kwa ajili ya wengine atakuwa ameyaokoa. Na yule atakaejaribu kuyaokoa Maisha yake atakuwa ameyapoteza” yaani mtu mbinafsi peke yake ndie anajiwaza yeye mwenyewe, na kila analofanya anafanya kwa ajili yake. Mara zote mtu ambaye anawaza Zaidi juu ya wengine hufikia mafanikio makubwa sana.

Lazima ukubali kujitoa sana kwa ajili ya wengine. Kila ulifanyalo waweke wengine mbele matokeo yake ni makubwa sana na yanagusa Maisha yako moja kwa moja.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

MAMBO 5 YANAYOKWAMISHA WATU WENGI.

Habari Rafiki, leo tena tunakutana kwenye Makala yetu ya MBINU ZA MAFANIKIO. Tunaangalia mambo ambayo yamekuwa ni sababu ya watu wengi kukwama kimaisha. Ninaposema kukwama namaanisha vile mtu anakuwa kwenye hali moja kwa muda mrefu.

Pata Kitabu: SIRI 7 ZA KUWA HAI LEO

Kama ni kazi anafanya basi anakuwa hana mabadiliko yeyote ya nje au hata ya ndani. Kama kuna mambo alikuwa anafanya yanakuwa hayaendi yako vile vile. Kama ni biashara basi biashara inakuwa haikui iko pale pale yaani imedumaa.

Inawezekana kabisa na wewe kuna sehemu ambayo umekwama, zipo sababu chache kati ya nyingi nimekuwa naziona zinajitokeza kwa watu ambao nazungumza nao. Jifunze nami ili uendelee kukua usikwame wala kudumaa.

  • Kukosa Maono Makubwa.

Kukosa maono makubwa ndio sababu ya kwanza kabisa kwenye Maisha ya watu kukwama. Watu wengi wanataka vitu kwenye Maisha yao lakini ni vidogo sana kiasi kwamba hawaweki hata juhudi yeyote kuvipata. Yaani vitu ambavyo wanaviona wana uwezo wa kuvipata hata kama hawataweka nguvu kubwa sana.

Kama unataka kufika mbali basi ona mbali, tengeneza picha kubwa ambayo itakusukuma wewe kupambana hadi itimie. Acha kuogopa kuwa jasiri na kile unachokionamktakwenda kutimia. Hakuna mafanikio yaliyowahi kuja yenyewe. Unapoweka maono madogo unakuwa mvivu kwasababu yenyewe hayakuhamasishi hata kidogo.

Pata Kitabu: Usiishie Njiani, Timiza Ndoto Yako

Unapokutana na changamoto unaweza kuzikimbia kwasababu hujaweka maono yeyote makubwa kwenye Maisha yako. Andika maono makubwa kwenye Mahusiano yako, Afya Yako, Kazi/Biashara na Fedha. Andika kwenye kitabu chako cha maono na anza kuyafanyia kazi kidogo kidogo hadi yatimie.

  • Kutokufanyia Kazi Maono Yao.

Ni kweli unaweza kuwa na maono makubwa lakini unafika mahali unakuwa hufanyi chochote kwenye ile picha yako kubwa uliyonayo. Usiishie kuhamasika na maono yako halafu ukakaa tu bila kufanya chochote. Kama unataka kuwa Mjasiriamali mkubwa hapa Africa basi anza na kitu kimoja leo, kikuze hadi kifike mahali hata mkoani kwako wakijue.

Kutokufanyia kazi maono kunaweza kuletwa na pale mtu anapokuwa anafanya jambo jingine ambalo halihusiani na maono yake. Mfano wewe una maono ya kuwa mfanyabiashara mkubwa halafu bado umeajiriwa. Unaweza kujikuta kila siku unasema nitaanza nitaanza hadi miaka inakatika bado upo pale pale. Sasa ndugu  yangu nitaanza haijawahi kukusaidia, tafuta kitu cha kufanya taratibu uanze kuona matunda yake.

  • Kutaka Kufanya Kila Kitu.

Huwezi kuwa kila kitu, huwezi kufanya kila kitu. Chagua vitu vichache ambavyo utavifanya hadi vikutambulishe. Mfano mimi binafsi nimeamua kuwa Mwandishi, Mjasiriamali na Mwigizaji. Hivi ninaweza kuvifanya na kila kimoja kina wakati wake wa kuanza kufanyiwa kazi. Kwa sasa unanijua kama Mwandishi na Mjasiriamali lakini miaka michache ijayo utaanza kuzitazama na filamu nitakazoigiza.

Unakuta mtu yeye kila kitu kinachokuja anataka afanye, leo limemjia wazo Fulani anajikuta amehama na kukimbilia wazo jipya. Mwisho wa siku unakuta hafiki mahali popote. Sasa Rafiki embu niige hata mimi kidogo chagua kitu kimoja au viwili ambavyo utawekeza muda wako na nguvu zako zote hadi ufikie Hatua kubwa kwenye Maisha yako.

Usiwe mtu ambaye huelewi mwelekeo wako wa Maisha. Tengeneza picha halafu anza kuishi kwa kuifuata hiyo picha. Kila jambo linawezekana kinachokukwamisha ni kutaka kufanya kila kitu mwisho wa siku unajikuta nguvu zako zimepotea kwenye mambo ambayo ulikuwa unagusagusa kila wakati.

  • Kuiga Wengine.

Hii tabia ni mbaya sana, umeona watu Fulani wamefanikiwa kwenye jambo ambalo hujawahi kufanya unataka na wewe uanze kufanya lazima utakwama. Wewe tafuta mtu mmoja au wawili ambao wamefanikiwa sana kwenye kile unachokifanya na ujifunze kwao. Usikubali kuwa nakala ya watu wengine. Tumia muda mwingi kujitengeneza miaka michache ijayo watu wataanza kujifunza kutoka kwako. Ulizaliwa wewe mwenyewe na una kila nafasi ya kufanikiwa kwenye dunia hii.

  • Kuishi Maisha Ya Maigizo.

Kamwe usije ukafanya kosa hili yaani kuigiza Maisha, kuwadanganya watu una Maisha Fulani mazuri kumbe ni uongo. Unajua unajidanganya mwenyewe, unajitesa mwenyewe, kuwa wewe ishi Maisha yako vile ulivyo.

Utakuwa unapoteza muda kama utaendelea na Maisha ya maigizo. Kuna mahali utashindwa kuingia kwasababu unaigiza Maisha. Tengeneza aina ya Maisha ambayo inakupa furaha na uiishi uswe mtumwa wa kuiga.

Umeanza biashara juzi tu lakini leo unataka uishi Maisha kama ya mtu ambaye alikuwa kwenye biashara miaka kumi iliyopita, lazima utafeli. Amini na fuata mchakato, mchakato ndio utakupeleka kule unakotaka kufika. Kabla hujawa bosi kubali kuwa mfanyakazi wako kwanza.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

www.jacobmushi.com/coach