Katika Maisha tunakutana na watu wa aina mbalimbali wanaweza kuwa wabaya kwetu na wengine huwa baraka kubwa sana kwenye Maisha yetu. Unaweza kukutana na mtu wa pekee sana kwenye Maisha yako na usiweze kujua kwasababu shetani amefunga ufahamu wako usione huyu mtu ni wa namna gani.

Ni vyema ukawa na uwezo wa kufahamu wale watu ambao Mungu anakukutanisha nao kwasababu mara nyingi wanaweza kuwa sababu ya wewe kusogea hatua nyingine. Usikubali mtu ambaye ana vitu vya pekee ndani yake aondoke bila ya kukugawia sehemu ya vitu vile alivyobarikiwa.

Tunaona kwenye Biblia Nabii Elia wakati anaondoka Elisha mtumishi wake alimuomba amuache japo sehemu ya nguvu alizokuwa nazo. Elisha alifanikiwa kuachiwa vazi ambalo lilikuwa ni baraka kubwa na msaada kwenye huduma yake.

2 Wafalme:2.9 Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.

Jiulize wewe ni mara ngapi watu wa maana wamekuja kwenye Maisha yako na baadae unakuja kusikia wamekuwa watu wakubwa sana na hata huwezi kupata nafasi ya kuwasogelea tena? Je watu hawa ungeweza kuwatambua mapema ingekuaje kwako?

Usikubali watu hawa waondoke bila ya wewe kujifunza kitu kwenye Maisha yao, bila ya wewe kuondoka na kitu ambacho Mungu aliwabarikia kuliko wewe. Kilichofanya Elisha akapata kupewa nguvu zile ni kwasababu alijua kung’ang’ania, alidhamiria kumfuata Elia hadi saa ya mwisho japokuwa aliambiwa asiende.

Kuna vitu hutavipata kwa kuomba peke yake bali kwa kuamua kuwa king’ang’anizi, usiogope kuonekana vibaya. Utaonekana wewe una shauku na una nia ya dhati kwenye kile ulichokiomba, usiombe mara moja halafu unasubiri majibu hapana, kumbusha kumbusha, sumbua sumbua, wacha uonekane msumbufu lakini kwa jambo ambalo ni jema.

Usikubali kumwacha aondoke mtu huyu wa maana ambaye amekuja kwenye Maisha yako. Hajaja bure, hujakutana nae bure, kuna jambo ameagizwa akuletee lakini yakupasa kulipa gharama kidogo ili upate kile ambacho unataka.

Kama mlango umefungwa usiondoke, ngonga kwa nguvu, sumbua walioko ndani hadi watoke waje kusikiliza shida yako.

jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

4 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading