TUSEMEZANE 425; MAMBO 37 YA NILIYOJIFUNZA MWAKA 2018.

Habari Rafiki nimekuwa na utaratibu wa kukuandikia mambo niliyojifunza kila mwaka na mwaka huu hii ndio mojawapo ya mambo ya muhimu kabisa niliyojifunza na ningependa nikushirikishe na wewe.

1 Hakuna kisichowezekana usiipe akili yako kikomo au kusema mimi siwezi hiki.

2 Usipofanya maamuzi magumu hutatoka hapo ulipo hata siku moja.

3 Penda kujaribu vitu ambavyo hujawahi kufanya kwasababu ndio njia pekee ya kukuwezesha wewe upande viwango kwenye unachokifanya na pia kujua vitu vipya.

4 Onesha Tabasamu popote ulipo huwezi kujua litamsadia nani.

5. Maisha Yako sio maonesho, chochote ambacho hakimsaidii mtu hakuna haja ya kukionesha hadharani, mfano Maisha yako binafsi ya ndani. Onesha vile vya muhimu sana na vinavyoweza kuwasaidia wengine.

6. Kelele ni nyingi sana wanaofanikiwa ni wale tu walioweza kuzishinda kelele na kuendelea na mambo yao.

7. Ukianza kufanya mambo makubwa wataanza kuja kukushauri hata watu ambao hukutarajia na wengi wao watakuwa wanakupa ushauri wa bure. Usipendelee ushauri wa bure kutoka kwa mtu alieibuka tu huko baada ya kuona unapaa.

8. Usitafute Watu Sahihi, endelea kufanya vitu sahihi waliosahihi watakuja tu wenyewe katika njia.

9. Usipoteze muda wako kutoa maoni sehemu ambayo unajua hakuna anaepokea maoni hayo.

10. Upendo Unaponya.

11. Tenga Muda wa Kuwa Pekee Yako upate utulivu wa kutosha Kila Wakati Unapoona Mambo hayaeleweki utapata majibu mengi sana kuliko hata pale unapowaeleza wengine.

12. Usiishi Maisha hapa duniani kama utarudi kuishi tena mara ya pili. Usifanye jambo tu pale unapojisikia kufanya. Jisukume Zaidi, fanya Zaidi, kila kitu weka Zaidi.

13. Usitegemee Huruma za Wengine Kuendesha Maisha Yako.

14. Hakuna anaeyawaza Matatizo Yako Na kuyapa kipaumbele kuliko wewe mwenyewe.

15. Kama huna muda wa kufuatilia Maisha yako, Umeshayapoteza Maisha Yako Anza Kuyatafuta, Maana hata Unapokwenda Huenda Hujui.

16. Msimamo ndio utawafanya watu wafanye kazi na wewe, usiwe mtu wa kubadilika badilika kila wakati.

17. Kama huna fedha Jiamini kama unazo, Ukiwa nazo Kuwa kama Huna.

18. Usimweleze kila mtu matatizo yako kwasababu hakuna anaeyajali kuliko wewe mwenyewe.

19. Watu wakiamua kuondoka kwenye Maisha yako sio wakati wote wewe ndio una matatizo mara nyingi wao ndio wanakuwa wamejiona hawastahili kuendelea kuwa na wewe.

20. Watu Wakishusha Thamani wewe usiungane nao na kujiona huna thamani, aliekuumba amekupa thamani.

21. Unapopoteza Kitu usiumie jifunze kwamba hakuna kinachodumu Zaidi ya akili ya kutafuta vitu, hivyo tafuta kingine bora Zaidi.

22. Usibebe huzuni ndani ya moyo wako, lolote ambalo limeshatokea haliwezi kurekebishika liache kama  tukio.

23. Wale ulikuwa unawapenda wakaondoka hapa duniani ni vyema kuwaacha kwa amani na wewe ukaendelea kufurahia Maisha hapa duniani. Si vyema sana kuendelea kuwakumbuka na kuwa na huzuni sana.

24. Usifanye maamuzi kwa kuongozwa na tamaa Ongozwa na Upendo. Tamaa huisha Upendo hudumu.

25. Usisubiri Kitu kiondoke kwako ndipo uanze kuona thamani yake.

26. Kila Siku unapewa Tsh 86,400 lakini hujui na unazitumia kidogo sana au kwenye mambo yasiyo na maana. Huu ni muda unaopewa kila siku (sekunde 86,400). Wewe huwa unazitumiaje pesa hizo?

27. Ipe Thamani ya fedha dakika yako moja na usikubali kuipoteza au kuichezea pesa hiyo kwenye jambo lolote lisilo na umuhimu kwenye Maisha yako.

28. Usipokuwa mchoyo na muda wako hakuna atakaeujali au kukuonea huruma.

29. Kutokujua maana ya Maisha kumewafanya wengi waishie kwenye mbio za kufanya vitu ili waonekane na wao wamefanya bila kujua kwanini wanafanya.

30. Angalia sana unavyoongea au kuwafanyia watu usiowajua kwani mara nyingi hizo kuwa ndio tabia zako za kweli.

31. Huwezi kuishi Unavyotaka kama huna pesa za kutosha, endelea kutafuta pesa, tengeneza mifereji Zaidi ya pesa.

32. Hekima ya masikini haisikilizwi, maana yake ukiwa masikini unadharaulika, hivyo basi njia ya kuondokana na dharau ni wewe kutafuta pesa katika njia sahihi.

33. Asikudanganye mtu eti huwezi kufanikiwa katika njia sahihi, endelea kupambana kwasababu wenye njia zisizo sahihi ndio wale wenye pesa lakini hawana furaha.

34. Pesa itakupeleka sehemu ambayo Huwezi kwenda na Miguu.

35. Huwezi kumtumikia Mungu kwa mali zako zote kama huna mali, hivyo tafuta mali kwa bidii sana.

36. Maisha Yako Ni alama hakikisha unaacha alama kwa watu kwa kuwatendea mema.

37. Andika yale unayotaka kuyafanya ndipo uanze kuyafanya hii itakusaidia kujua ni kipi umefanya na kipi hujafanya. Fikiria kwenye karatasi, chochote unachokifikiria kiandike.

Mambo haya nimejifunza kwenye hatua mbalimbali nilizochukua kwenye Maisha yangu kwa mwaka 2018 pia niliyojifunza kwa wengine. Tuendelee kuwa pamoja tena na tena ili kujifunza mengi Zaidi mwaka ujao.

Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

jacobmushi
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading