511; Unakimbilia Wapi? Tazama Pembeni Yako.

jacobmushi
3 Min Read

 Haya Ndio Maisha yetu kwenye vitu vingi tunavyopitia kila siku, Soma kisa hiki ujifunze: “Habari kaka Jacob, ninaomba ushauri wako kuhusu hili. Ni mwaka wa tatu sasa tangu nikutane na binti mmoja na nikampenda sana. Nina tabia moja huwa sikati tamaa haswa pale ninapokuwa nimekipenda kitu Fulani maishani mwangu. Nimekuwa naamini kwamba ipo siku tu kitakuwa cha kwangu.

Binti huyu kila nilipokuwa namfuatilia ili niweze kuwa nae amekuwa akinisumbua sana, kila wakati ananipiga chenga za namna mbalimbali. Nimejitahidi kumpatia kila anachokitaka, lakini alikuwa anasema anatamani tuwe marafiki tu kwani tukiingia kwenye mahusiano tutakuwa tunagombana na mwisho wake tutaachana.

Kwasababu nilimpenda kwa dhati ikanibidi nimsikilize tu. Sasa huu ni mwaka wa tatu tumekuwa karibu kama marafiki na nilijiapiza sitaingia kwenye mahusiano mengine kwakuwa niliona kama ananipima uaminifu wangu.

Wiki mbili zilizopita kanijia huku akilia machozi na kuniomba msamaha anasema ananipenda sana na yupo tayari kuwa na mimi kuanzia sasa. Anadai amegundua alikuwa anapoteza muda na watu ambao hwakuwa wanampenda bali kumtumia tu.

Hilo halikuwa shida, kubwa Zaidi ananiambia kwamba mwanaume aliekuwa nae kwenye mahusiano kwa Zaidi ya miaka 3 akijua anampenda, amempa ujauzito na kumkimbia. Huku akidai hawezi kuwa nae kwenye Maisha yake.

Naomba ushauri wako, nifanyeje, ukweli huyu binti nampenda sana, changamoto ni huu ujauzito alioniletea, sielewei kama ananipenda kweli au ni kwasababu ya matatizo aliyopitia tu. “

Kijana huyu amekumbwa na mkasa huu mzito sana kwenye Maisha yake. Ni kweli inaumiza sana, nataka na wewe ujifunze kitu kwenye huu mkasa, je ni vitu gani umekuwa ukivikimbilia ukijua ni vyako mpaka pale ulipopoteza?

Huyu binti amekua akishikamana na watu ambao hawakumpenda na akasahau kabisa kuona mtu aliekuwa karibu yake wakati wote. Inawezekana hata wewe kuna vitu umekuwa unavishikilia ukidhani ni vyako na ukasahau vile ambavyo ni vyako siku zote vipo karibu na wewe siku zote.

Embu jaribu kutazama ni nani huwa yupo karibu yako kila mara? Ukiwa na shida, ukiwa na raha yupo. Wakati wowote ukimhitaji anakuwa yupo tayari kwa ajili yako. Naomba nikwambie watu hawa ni wa thamani sana kwenye Maisha yetu. Usikubali kuwa mtu ambaye unaiona thamani yao wakati wa matatizo tu.

Kuna watu wanaweza kukwambia wanakupenda kwa maneno matamu lakini kuna watu wanakupenda kwa kufanya vitendo kwenye Maisha yako. Kuna watu ambao hujawahi kusikia wakisema NAKUPENDA lakini wamekuwa wakifanya mambo makubwa kwenye Maisha yako kuliko neno hilo na NAKUPENDA.

Jifunze kutofautisha watu wanaouhitaji mwili wako na wanaouhitaji moyo wako, jifunze kutofautisha watu wanaozihitaji pesa zako na wanaokuhitaji wewe kwenye Maisha yao. Wapo wengi wanaonekana kama wanatuhitaji sisi kumbe wanahitaji vile vitu tulivyonavyo. Ukishindwa kujua haya utaishia kutumbukia kwenye shimo kila mara.

Rafiki Yako

Jacob Mushi.

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
2 Comments

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading