Mwaka 2004 ulikuwa ni mwaka ambao ungeweza kuwa sababu ya wewe kutokusoma hiki ninachokiandika leo wala kufahamu kama niliwahi kuwepo kwenye ramani ya dunia hii. Lakini kwasababu ya kusudi la Mungu ambalo aliweka ndani yangu akaweza kunipa kibali nikapata tena nguvu ya kuendelea kuishi na sasa unaweza kunisikia na kusoma Makala ninazoandika.
“Ilikua ni jioni moja baada ya kutoka shuleni nikaingia kwenye majukumu yangu ya kila siku ya nyumbani. Siku hiyo nilitakiwa kwenda shambani kutafuta kuni kwa ajili ya kupika. Kama mtoto ilikua ni muhimu kutekeleza majukumu yangu kwanza ndipo mambo mengine yaendelee.
Kwa bahati mbaya sana siku hiyo nilipoingia shambani tu nikakutana na mti umejaa matunda ya korosho (mabibo) yakanivutia macho.
Nikaamua kuacha lile lililonipeleka kule shambani na nipanda juu ya mti kula matunda. Matunda yaliponinogea sana nikajisahau hata namna ya kukanyaga matawi ya miti.
Ghafla sana nikajikuta nipo chini sijielewe nimefikaje!
Nikijaribu kuinuka siwezi, kujaribu kunyanyuka siwezi kumbe shati langu limeshikwa na mti.
Nikapeleka mkono nyuma nitoe shati lilipokwama mkono wangu ukarudi umejaa damu tele na hapo ndipo nikagundua kumbe niliumia sana.
Nilipoanguka mgongo wangu ulitua juu ya kisiki cha mti ambao umepasuliwa kuni na kubaki ncha ncha tu. Ncha ile ilitoboa karibu na uti wa mgongo.
Nikashindwa kujua cha kufanya nikaishia kupiga kelele na watu wakaja kuniokoa. Baada ya muda nikapelekwa hospitali.
Mungu ni mkubwa sana niliweza kuhudumiwa na baada ya muda nikarudi nyumbani lakini sikuweza kabisa kutembea mwenyewe nilibebwa kama mtoto mdogo.
Mungu ni mkuu baada ya miezi miwili nikapona kabisa na nikaweza kuendelea na masomo yangu shuleni”
Kwanini nimekupa kisa hiki cha ukweli kuhusu Maisha yangu?
Kuna jambo nataka ujifunze hapo. Kwanza ni ukuu wa Mungu juu ya Maisha yangum namna alivyoweza kuniokoa na kifo. Kwa hali ya kawaida pale nilipodondoka nisingeweza kutoka salama. Lakini ni kwa makusudi ya Mungu mimi kuwepo hai mpaka sasa.
Ni muhimu sana wewe uliepo hai mpaka sasa ukalijua kusudi la Mungu juu kwenye Maisha yako. Kusudi la Mungu ndio ulinzi kwenye Maisha yako. Kuna mengi sana yanaweza kupangwa kwa ajili ya kukudhuru lakini kwa sababu ya kusudi la Mungu ukatoka salama.
Ni muhimu sana kuishi Maisha yenye maono. Unapokuwa na maono unaweza kujua ni wapi unakwenda. Unaweza kuweka vipaumbele vyako. Unaweza kuchagua vitu vya kufanya na ambavyo si vya kufanya. Kama huna maono unakuwa mtu usie na muelekeo.
Soma: Nilichojifunza Kwenye Maisha ya Watu 2017
Kitu kingine unapaswa kujifunza ni kwamba mara nyingine kuna mambo yanatokea kwenye Maisha yako baada ya wewe kuacha lile jukumu ulilopewa na kwenda kudandia mambo mengine.
Kuna mambo mengi sana unaweza kujikuta unashindwa kufikia malengo yako na unajikuta katikati ya changamoto kwasababu katika njia yako ulivutiwa na vitu vingine vilivyokuwa nje ya njia ukaacha njia na kuvifata.
Rafiki Yako,
Jacob Mushi
#UsiishieNjiani