Nilikuwa napitia maisha ya mwandishi mashuhuri kutoka Brazil, Paulo Coelho aliendika vitabu vingi kikiwemo cha The Alchemist. Mojawapo ya jambo gumu alilowahi kupitia maishani mwake ni alipokuwa na umri wa ujana yaani miaka ya 18-20 aliwahi kupelekwa hospitali ya vichaa mara tatu na wazazi wake.

Wazazi wake waliziona tabia zake na kufikiri ni mtu aliechanganyikiwa na kuamua kumpeleka kwenye hospitali ya vichaa kwa nguvu. Kitu kimoja ambacho anasema yeye hawezi kuwalaumu wazazi wake wala kuwasamehe kwasababu hawajakosea chochote ni kwamba tu walikuwa hawajui. Sasa yeye anaona tu ni kama walikuwa wanataka kumsaidia.

Kiukweli hili ni jambo gumu sana katika maisha ambalo amewahi kupitia lakini pamoja na yote hayo ameweza kuwa mwandishi mashuhuri duniani mpaka sasa. Inawezekana na wewe kuna jambo linaendelea kwenye maisha yako na umefikia wakati unayona maisha yako hayana maana tena. Inawezekana umetengwa na watu, hakuna anaekujali wala kuona uwepo wako hapa duniani, yote hayo yanaweza kuwa sababu ya wewe kuona maisha hayana maana.

Inawezekana unaona maisha hayana thamani tena kwasababu ya kitendo kibaya ulichofanyiwa,mfani kuachwa, kukataliwa, kutengwa na ndugu, huenda ulibakwa na mtu ambaye hukuwahi kutarajia angekufanyia hivyo, huenda umepatwa na tatizo ambalo linakufanya uone hakuna tena hatma ya maisha yako. Yote haya na mengine mengi yanaweza kuwa sababu ya wewe kukata tamaa na kuona hakuna tena thamani wala maana ya maisha yako hapa duniani.

Rafiki yangu nataka nikwambie yupo mtu mmoja ambaye anayathamini maisha yako mtu huyo ni sio mtu wa kawaida ni Mungu. Huyu ndiye aliamua wewe uje duniani, na pia ndiye amekuacha hai mpaka sasa.

Ufanye nini Sasa?

Usipende kutumia muda mwingi kukaa peke yako.

Kama umefikia hatua hii ya kuona maisha hayana thamani tena unaweza kujikuta unajiwa na mawazo ya kujidhuru au hata kujiondoa uhai. Sasa ili uweze kuepuka haya tafuta jukumu la lazima ambalo linaweza kukurejeshea tena uhai ndani yako. Kama huna watoto na una uwezo tafuta hata mtoto alietelekezwa na wazazi uanze kuishi nae, moyo wako, akili yako, nguvu zako zote uziwekezee kwa huyo mtoto hapo tayari utaanza kupata kusudi la kuishi tena.

Tafuta kitu cha kufanya ili kuleta maana ya maisha yako.

Hapa unaweza kwenda kuwatembelea wagonjwa mahospitalini au hata kwenye vitu vya watoto yatima. Sio lazima uende na chochote, unaweza kwenda kutenga muda wa kukaa na mtu mmoja aliekata tamaa na ukamtia moyo. Ukamuonesha kwamba maisha yake yana thamani ukamtia nguvu na akaendelea kuishi. Wanasema kama wewe unafikiri unaumwa sana hebu nenda hospitali ukawaona wagonjwa wanavyoteseka.

Tafuta mtu mmoja ambaye unaweza kukaa nae na umfanye awe rafiki yako.

Huyu anaweza kuwa mtu mzima ambaye umeona unaweza kumuamini. Mfanye awe rafiki lakini katika namna ambayo unaona ataweza kukufanya uondokane na upweke na kutafakari mabaya juu yako. Mara nyingi wenzetu wazungu hupenda kununua wanyama na kuishi nao. Hawa wanyama wanakuwa wanahitaji matunzo na vyakula hivyo moja kwa moja kinakuwa ni kitu anachokifikiria sana wakati wote. Sasa huku kwetu huo unaweza usiwe utamuduni wetu au wanyama wetu sio rafiki sana nasi. Hivyo ni vyema ukatafuta mtu ambaye umeona ana ubinadamu ndani yake na ukamfanya akawa rafiki yako.

Kuwa mwandishi.

Hii nayo ni njia nyingine ambayo unaweza kuitumia kujipa maana na thamani ya maisha yako. Anza kuandika yale mambo ambayo unafikiri watu wakiyafanya hawataweza kupitia pale ulipopita wewe. Mfano tuseme ulipitia vitendo vya unyanyasaji, embu ona kwamba ukijiua wako wengine kama wewe wanaendelea kuteseka bila kujua, embu sasa anza kuandika namna wanavyoweza kuishi na kuepuka kupatwa na madhara kama ambayo wewe umepitia. Kwa kipindi hiki tuna mitandao ya kijamii unaweza kuitumia kuandika au ukawa na blog yako kama hii hapa ukaanza kuwafundisha watu namna ya kuishi.

Napenda nikwambie hakuna mtu anaweza kuindoa thamani ya maisha yako tofauti na wewe mwenyewe. Pale tu unapoanza kufikiri maisha yako hayana maana ndio umeanza kuindoa thamani wewe mwenyewe. Anza kuwapenda watu, tafuta jambo la kufanya kwenye jamii ambalo litakusaidia kuinua tena moyo wako uliovunjika.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com

6 Responses

Leave a Reply to AlphonceCancel reply

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading