Haina maana yeyote kama watu watajenga picha kubwa kwako kutokana na namna unavyopenda kujionyesha halafu uhalisia ukawa ni tofauti kabisa. Ni vizuri sana ukaishi vile unavyopenda lakini ni vyema ukakubali kulipa gharama za hayo maisha kwanza ndipo uje kufurahia baadae.

Ni kichekesho sana kama utakuwa unatamani watu waone unaishi maisha mazuri wakati kwa ndani unateseka bure. Haifai na wala haina maana. Tengeneza yale maisha unayoyataka pole pole. Acha kwenda kukopa pesa za kununua maisha tengeneza maisha unayotaka polepole.

Acha kutafuta jina kwa kuishi maisha fake wakati nyuma ya pazia unateseka. Kama unamiliki gari na huwezi kulihudumia maana yake pesa  ulizonunulia ulikopa au ulizipata kwa bahati. Kama unaishi kwenye nyumba ya gharama halafu kodi inakupiga chenga maana yake umeruka hatua ya maisha.

Kuna nyakati mambo yanabadilika utashindwa tena kuficha yale ambayo unaigiza. Ukweli utakuja kuonekana baadae. Amua sasa kuwa halisi watu wakukubali na wakupende vile ulivyo na sio vile unavyotamani kuwa.

 

Wewe halisi ni wakati ukiwa peke yako ndani na siyo wakati ukiwa nje mbele za watu. Kuna picha nyingi umezijenga kwenye akili za wengine juu ya maisha yako kwasababu umekuwa unawadanganya kwa kuigiza maisha.

Labda nikushauri kitu kimoja aina yeyote ya maisha unayotaka kuyaishi kubali kuyalipia gharama. Kwenye kulipa gharama kuna muda unatakiwa upite hapo katikati hadi uanze kuona yale maisha unayotaka. Ukikwepa kulipa gharama utaishi maisha ya utumwa yaani wewe utakuwa unakopa ili uishi maisha yale unayotaka.

 

Kwenye kulipa gharama kuna changamoto zake. Kuna kudharaulika, kuonekana wewe mbahili, kuonekana unafanya biashara za hovyo na wengine watasema umefilisika lakini wewe usiyaangalie hayo. Yatazame yale maisha unayotaka kuja kuishi. Hata wote duniani wakikusifia unaishi maisha mazuri halafu uhalisia wake ukawa tofauti inakuwa haina maana.

Kubali kulipa gharama ya vile unavyovitaka kabla ya kuvivamia.

Kubali kuishi kwa uhalisia utakuwa huru.

Hakuna haja ya kuigiza maisha yatengeneze yale maisha ili uwe huru katika kuyaishi.

 

Kuwa Mwanachama Kamili wa Usiishie Njiani Bonyeza hapa.. https://jacobmushi.com/jiandikishe/

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio Hapa.. https://jacobmushi.com/patavitabu/

Jipatie Blog Bora hapa.. https://jacobmushi.com/jipatieblog/

 

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading