Mara nyingi fursa za kubadilisha maisha yetu huja katika sura ambazo hatuzipendi na wala hazivutii kufanya.Kwasababu watu hupendelea vitu vizuri na vyenye heshima hujikuta wanapishana na fursa za kubadilisha maisha yao.
Kuna hadithi moja niliwahi kuisoma, Kulikuwa na watoto wawili walikwenda kumtembelea bibi yao wakati wa siku kuu.Sasa wakati wanaondoka bibi aliwaandalia zawadi.
Zawadi hizo zilikuwa ni mifugo ambayo aliifunga kwa kamba na kuziweka ndani ya chumba. Zile kamba zilikuwa mbili, moja ilikuwa kamba chakavu na nyingine ilikuwa mpya.
Akawaleta wale wajukuu zake na kuwaambia wachague zawadi zao. Mmoja alikimbilia ile kamba mpya na aliebaki ikabidi achukue kamba iliyochakaa.
Wakati wanazitoa zawadi nje ndipo kila mmoja akabaki anashangaa, kama mpya ilikuwa imefunga kuku na ile chakavu ilikuwa imefunga Kondoo alienona.
Mwanzoni yule wa kamba mpya alifurahi sana kwasababu alipoona upya wa kamba alijua na zawadi itakuwa nzuri. Mwenye kamba iliyochakaa alijua ndio amekosa.
Maisha yetu ndivyo Yalivyo, unaweza kukutana na mchumba ukadhani umepata kwasababu anaonekana mrembo au smart kwa nje baadae unakuja kugundua ana tabia zisizovumilika.
Usikimbilie kutazama nje kwasababu vitu vizuri huwa havinaga muda wa kujipendezesha nje ili kuvutia watu.
Jifunze kuangalia ndani na kufanya maamuzi kwa kutumia akili na sio hisia.
Sisemi wewe ukae hovyo hovyo tu eti kwasababu u mzuri ndani hapana. Sisemi uchague vilivyo hovyo hovyo kwasababu vitakuwa vizuri ndani hapana. Nataka tu usiwe mtu wa kushawishiwa na muonekano wa nje.
Usije ukasema ndio huyu, hii ndio ile fursa, kwa kuangalia nje pekee. Ingia ndani zaidi ujue vya kutosha kabla hujafanya maamuzi.
Nakutakia Kila la Kheri.
Ubarikiwe sana.
Rafiki Yako Jacob Mushi.