Ukiwa na Shilingi elfu moja mfukoni unaweza kuiona ni pesa ndogo sana isiyotosha kufanya kitu chochote cha maendeleo zaidi ya kula tu.
Lakini nikwambie kitu cha Ajabu sana shilingi elfu moja inaweza kuwa ni mwanzo wa wewe kuwa tajiri.
Kuna watu kutokana na fikra zao zilivyo wanaweza wasiamini na hivyo wakaendelea kubaki pale pale walipo.
Shilingi elfu moja unaweza kuinunulia vocha ukaingia kwenye mitandao ya kijamii ukachati na kufuatilia Habari hadi kifurushi kikaisha.
Unaweza pia kununua matunda ukala ukashiba siku ikapita.
Lakini mwenzako mwenye simu kama yako anaweza kuitumia elfu moja kutafuta wateja wa bidhaa ambazo zipo dukani akaziuza na akatengeza faida.
Nikupe mfano hai; Siku Moja nikiwa Arusha nipo nyumbani mfukoni nina tsh elfu moja tu.
Nilipata wazo la kufanya biashara ya dagaa wa mwanza. Sikuwa na mtaji wa kuanzia. Nikiwa katikati ya mawazo, Akanipigia Rafiki Yangu mmoja anataka Laptop. Kwasababu nimesomea mambo ya IT akaniomba nimsaidie kutafuta Laptop used.
Nikamuuliza ana shilingi ngapi akasema ana laki tatu, nikamwambia subiri kidogo. Ile elfu moja nikaamua kujiunga kifurushi nikaingia kupatana nikatafuta laptop used. Baada ya dakika kadhaa nikaipata tena ilikuwepo maeneo yale yale ya Arusha. Kumbuka mimi sikuwa dalali wala sikumfahamu yeyote anauza laptop.
Laptop ile muuzaji alikuwa anauza tsh 250,000, nikambana akashuka mpaka 220,000 nikampigia rafiki yangu na kumwambia laptop imepatikana tuma hela.
Akatuma laki tatu mimi nikanunua ile laptop na kumpelekea huku mfukoni nimebakiwa na tsh 80,000, hela hii ilitosha kuanzia biashara ya dagaa na kubaki pesa kidogo.
Nataka nikwambie wewe unavyoichukulia elfu moja ndio hivyo hivyo itakuletea matokeo. Ukiiona ndio pesa iliobakia ya kula, itakuwa ya kula. Ukiiona inaweza kufanya mabadiliko ni wewe binafsi.
Mtazamo wako una nafasi kubwa sana katika Mafanikio. Fikiri Chanya kila wakati, ona Uwezekano hata ule wakati unaohisi kushindwa.
Wakikwambia matajiri wana siri nyingi ambazo hawatakaa waziseme waambie hata ukizijua bado zinaweza zisikusaidie. Kama Umeshindwa kufanyia kazi kidogo ulichonacho mkononi usitegemee kuweza kufanyia kazi Vikubwa.
Nakutakia Kila la Kheri.
Ubarikiwe sana.
Rafiki Yako Jacob Mushi.