Katika kazi yetu hii ya kushauri, kutia moyo, na kuhamasisha watu huwa tunakutana na changamoto. Mojawapo ya Changamoto kubwa ni pale mtu anapokuuliza wewe umeshafanya nini mpaka unataka kunihamasisha mimi?

Yaani mtu anasema ili aweze kusikiliza kile unachomwambia na kukifanyia kazi hadi aone umefanya kitu fulani. Labda tayari una gari, au una maisha fulani hivi ya Kuonekana kama una mafanikio.

Kinachonishangaza sana ni kwamba watu wa aina hii unakuta ukiwaambia mbona Mengi hajakufanya ufanikiwe mpaka sasa? Mbona wako wahasishaji wakubwa tu tangu zamani nini kinafanya usichukue hatua kwenye kile wanachofundisha?

Sasa Rafiki kama wewe ni mmoja wa watu wenye fikra hizo Naomba ufahamu hili. Tatizo sio Mhamasishaji tatizo ni wewe.

Kama maisha yako mwenyewe hayakuhamasishi kufanikiwa una matatizo zaidi yanayohitaji msaada.
Kama utakuwa unasubiri mpaka mtu afanikiwe ndio wewe uanze kuchukua hatua ndugu yangu utachelewa sana, halafu pia wewe hujielewi, hujui kwanini upo hapa duniani.

Kama ni watu waliofanikiwa kwenye kila aina ya fani wapo kila mahali, hivi ni kweli utakuwa umekosa mtu mmoja wa kukuhamasisha kweli?

Rafiki Yangu una tatizo, Anza kuchukua hatua sasa. Hayo ni maisha yako, usisubiri fulani afanye ndio wewe ufanye. Ukiwa mtu wa kutaka kuona kama Thomaso utakuja kujikuta muda umeenda na unachokitaka hukijui.

Anza kufanyia kazi unayojifunza na Usiishie kuhamasika tu.

Anza kuwa na ndoto kubwa, malengo makubwa ambayo yanakuhamasisha kuliko hata wahamasishaji.

Kuwa na malengo makubwa ambayo yatakulazimisha usome vitabu, utafute hamasa mwenyewe.

Usiwe kama mmoja wa hao wanaosema nasubiri nione ulichofanya wewe ndio unihamasishe. Utaachwa hapo kwasababu hakuna mtu ana muda wa kukuridhisha wewe kila mtu anapambana atimize Ndoto yake.

Nakutakia Kila la Kheri.
Ubarikiwe sana.
Rafiki Yako Jacob Mushi.
www.jacobmushi.com

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading