Katika Maisha tunakutana na watu ambao wanaweza kuwa baraka sana kwenye Maisha yetu hadi tukajisahau kwamba kuna siku wataondoka. Ninaposema kuondoka simaanishi kufa namaanisha kuna siku hawatakuwa pamoja nasi kama walivyokuwa nasi mwanzo.
Kosa ambalo unaweza kulifanya na likasababisha uje kujuta Maisha yako yote ni kuwapa utegemezi mkubwa watu ambao hawadumu maishani mwako. Lazima ujifunze kwamba kuna nyakati zinafika watu hawataendelea kuwa kwenye Maisha yako haijalishi mlikuwa marafiki kiasi gani, haijalishi mlikuwa mnapendana kiasi gani, haijalishi mlifanya vitu gani kwa pamoja.
Ukishindwa kutambua hilo utabakia unaumia na kuwalaumu watu Maisha yako yote. Wote walioondoka kwenye Maisha yako tambua kwamba hawakuungana na wewe hivyo walikuwa na haki ya kuondoka.
Usikubali kuwategemea wengine kwa asilimia mia moja kihisia, furaha, fedha, na vitu vingine ambavyo vikiondoka vinaweza kusababisha Maisha yako yakayumba. Ni kweli tunategemeana lakini unapotegemea kwa asilimia kubwa lazima siku moja utaumia.
Jifunze kugawanya vile vitu vinavyofaa kugawanyika. Kuna vitu havifai kugawanyika kabisa kama kumpenda mtu upendo wa kimapenzi huwezi kuwapenda wengi kwasababu huyu mmoja ataweza kuja kuondoka. Hapo unapaswa kujua kwamba lolote linaweza kutokea mabilionea wanaachwa, watu maarufu na mashuhuri mahusiano yanavunjia hivyo hata kwako pia linaweza kutokea jambo kama hilo. Hivyo basi likitokea usiumie kiasi kikubwa kama ndio mara ya kwanza kwako.
Usikubali kutegemea sehemu moja kama chanzo chako cha pesa. Maisha yako yatayumba pale tu kile unachokitegemea kitakapoyumba. Iwe ni ajira au biashara kamwe usikubali kutegemea sehemu moja. Hakikisha una vyanzo Zaidi ya kimoja vya kipato.
Usitegemee watu kwenye kutekeleza mambo yako kwa asilimia mia. Kuna nyakati unaweza kumpa mtu kazi na unamjua huyu kazi zake anafanyaga vizuri. Ukategemea na hiyo hatakuangusha na kitu cha ajabu ukaja kushangaa sana ile siku umempa kazi ya muhimu sana ndio anafanya usichokitarajia.
Sikwambii usiwaamini watu ila nakwambia usiweke asilimia mia moja kwenye chochote ambacho hakitoki kwako. Kuna nyakati mtu anaweza kuwa sababu ya wengine kukwama.
Kuna mtu mmoja aliwahi kusema uhakika ulionao pekee ni kutokuwa na uhakika. Hivyo hata kile unachofikiri kwa asilimia mia moja kitakuwa hakiwezi kuwa vile mara nyingi kunatokea vitu ambavyo vinasababisha tusiweze kufika kule tunakopanga.
Jambo moja unalopaswa kutambua ni kwamba usikate tamaa, pamoja na hayo yote yanayoweza kutokea ya kutuvunja moyo sio mwisho wa Maisha. Ugumu wa Maisha hautufanyi tuache kuendelea kuishi bali kutafuta namna ya kuwa na Maisha bora Zaidi.
Rafiki Yako,
Jacob Mushi
#UsiishieNjiani
https://jacobmushi.com/usirudie-tena-au-usijaribu-kosa-hili-mwaka-2018/