Kwa muda mrefu nimekuwa nikiona watu wanafanya vitu mbalimbali kama ujasirimali, biashara fulani, kazi Fulani, ili tu kuwathibitishia watu fulani waliokuwa wanawaona wao hawafai. Mfano mtu aliambiwa wewe hujawahi kuweza kitu hutaweza biashara. Anaingia kwenye biashara kwa hasira ili tu amthibitishie yule mtu kwamba anaweza.

Unaweza kuambiwa wewe huwezi kupata kazi Fulani kwasababu huna elimu ya kutosha halafu ukaanza kupambana kufanya vitu mbalimbali ili tu uweze kuipata ile kazi watu wajue kwamba hata wewe unaweza.

Hii ni mbaya sana kwasababu unaweza kujikuta unatumiwa bila kujijua. Mfano mtu atakuja akwambie huwezi kufanya kitu Fulani ukafanikiwa kwasababu anataka ukifanye halafu wewe ukafanya ukaweza na yeye akajikuta ametimiza lengo lake. Wewe utaona umeweza kumwonesha kwamba unaweza lakini yeye anakucheka kwasababu ameshakutumia.

Hasara nyingine ni kwamba unaweza kujikuta unafanya hata vitu visivyo sahihi ili tu upate ile kazi au ufanikiwe kwenye ile biashara ambayo uliambiwa huwezi na ikawa ni madhara makubwa kwako. Unaweza kujikuta umetoa rushwa kwasababu unataka kwa haraka yale mafanikio ili kuwakomesha wale watu waliosema hutaweza. Unaweza kutoa rushwa ya ngono ili upate kazi ambayo uliambiwa na marafiki zako kuwa wewe huwezi ipata.

Kitu kingine ambacho ulikuwa hukijui ni kuwa unakuwa umedhibitiwa na yule mtu aliekwambia huwezi. Unajikuta unafanya kwa kupitia ushawishi wake alioweka ndani yako kwa kusema huwezi. Hivyo basi yule mtu anakuwa amekudhibiti. Kwa kifupi unakuwa ni mtumwa wake, inawezekana hata yeye asijue kwamba alikufanya mtumwa. Kibaya Zaidi ni pale anapokuwa amejua halafu akaamua tena kukutumia.

UFANYEJE?

Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ni kutoka nje ya lengo la Maisha yako. Hujaja hapa duniani kuwaonesha wengine kuwa unaweza. Umekuja hapa duniani kuishi ishi Maisha yako vile unavyotaka, usipoteze muda hata kidogo kufanya chochote ili tu kumthibitishia mtu unaweza.

Akitokea mtu akakwambia huwezi kitu Fulani, au unachokifanya hakitakaa kikuletee mafanikio mpuuze, mwambie hajui kwanini unakifanya. Kaa mbali kabisa na mtu anaekwambia ni kitu gani huwezi, kaa karibu Zaidi na wale wanaokuonesha ni vitu gani unaweza.

Wapuuze wote na wala usifanye chochote kuwaoneshea kwamba umeweza kwani utajikuta unakimbia mbio ambazo hazina mwisho na wala faida zozote. Malengo uliyojiwekea mwenyewe ndio ya muhimu kuliko mengine. Hata mtu akija kukwambia hutayatimiza mwambie haikuhusu nisipotimiza ni juu yangu mwenyewe.

Hakuna atakaekuchapa usiponunua gari, hakuna atakae kufukuza usipotimiza malengo yako, kwa kifupi wewe mwenyewe ndio utawajibika na kuumia kwa kutokutimiza kile ulichokuwa unakitaka hivyo basi hakikisha unafanya kile ambacho moyo wako unataka.

ACHA, FANYA KILE UNACHOKIPENDA BILA YA MSUKUMO WA KUTAKA KUWATHIBITISHIA WENGINE KUWA UNACHOKIFANYA NI SAHIHI, AU WALIVYOSEMA UTAFELI WALIKOSEA.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading