Kuridhika na Mafanikio ya Jana.
Habari Rafiki, Leo ni siku nyingine tena ambayo tumepewa kama zawadi kwa ajili ya kwenda kuyafanya Maisha yetu yawe bora Zaidi.
“NACHUKUA HATUA, NAJIFUNZA, NAWEKA JUHUDI NA BIDII, NAVUMILIA.
MAFANIKIO NI HAKI YANGU, EEH MUNGU NIWEZESHE.”
Mojawapo ya tabia ambazo zinawafanya watu wengi kushindwa kufanikiwa au kupoteza kile ambacho wamekuwa wakikitafuta kwa muda mrefu ni kuridhika na mafanikio wanayopata. Mwanzoni mwa jambo lolote kunakuwa na hamasa kubwa sana lakini baada ya muda mtu anapozoea anaanza kuwa wa kawaida.
Unapoanza mahusiano mwanzoni kila mmoja anamfurahia mwenzake, kila mmoja anakuwa haoni mabaya ya mwenzake. Lakini baada ya muda kunatokea kuzoeana, na hii inakuwa kama sumu kwasababu kila mmoja anaanza kumuona mwenzake wa kawaida.
Unapoanza biashara unaweza kuwa na hamasa kubwa sana, katika kuhudumia wateja, kuzungumzia bidhaa zako lakini inapotokea umeanza kupata mafanikio kidogo unaanza kuzoea ile hali na kuwa wa kawaida.
Wanasema hata unapoendesha gari kuna mwendo ambao hujawahi kuufikia ukifika hapo utakuwa unaogopa na kutetemeka lakini baada ya muda unaweza kuuona ni kawaida.
Ni hatari kubwa sana pale mambo yanapokuwa ya kawaida kwenye Maisha yako. Ni hatari sana pale unapoyachukulia mafanikio kama mazoea Fulani hivi. Unakuwa unakaribisha anguko lako mwenyewe.
Unapaswa kujua ili uweze kukua na kuongezeka lazima ukubali kubadilika. Lazima ukubali kujaribu vitu vipya kila siku ambavyo vitakufanya usiwe mtu wa kuzoea hali moja kila wakati.
Inashauriwa angalau kila siku uweze kufanya jambo moja hata kama ni dogo sana lakini ambalo limekuwa linakuogopesha sana. Kama wewe ni Mwandishi umekuwa unaandika maneno 500 kwa siku jaribu kujipa zoezi la kuongeza kwa kuandika maneno elfu moja au Zaidi. Kama unaimba jaribu kufanya kitu cha ziada kila siku kwenye uimbaji wako. Kama unafanya kazi jaribu kwenda Hatua ya ziada kwenye kazi yako.
Usikubali kile ulichokifanya jana kiwe ndio unakizungumzia saana bali kila siku iwe ni mpya kwako kwa kufanya vitu vingine vipya ambavyo vitakuongezea uwezo wako wa kufikiri na kujaribu vitu. Ili uongeze ujasiri ni lazima ukubali kufanya vile vitu ambavyo vinakupa hofu. Unaweza kuongea na mtu ambaye umekuwa unaogopa sana kuongea nae. Kuna mtu umempenda jaribu kumwambia hata kama moyo wako unasitasita na unakuwa na hofu.
Chochote kile ambacho unahisi kinakupa hofu na kina manufaa kwenye Maisha yako nenda kakifanye na uone kinaleta matokeo gani.
Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi
#UsiishieNjiani
“Chukua Hatua, Timiza Ndoto Yako.”
Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio… https://jacobmushi.com/patavitabu
Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog ….. https://jacobmushi.com/jipatieblog
Karibu Usiishie Njiani Academy https://jacobmushi.com/whatsapp/