Inawezekana unayatazama Maisha ya watu waliofanikiwa na kujikuta unatamani sana kuishi kama wao na kujiona wewe unaishi Maisha ambayo ni duni sana. Ukweli ni kwamba kuna ambao wanatamani wangekuwa na Maisha ya kawaida kama yako kwasababu ya changamoto kubwa wanazokutana nazo sehemu ambazo wapo.

Kama unafikiri utaweza kuvumilia kuandikwa vibaya kwenye magazeti kwa habari ambayo mtu aliamua tu aandike mawazo yake juu yako endelea kutamani nafasi hiyo. Kama unafikiri utaweza kuvumilia kukosolewa na watu ambao hawana cha kufanya wapo kitandani wamelala wanatoa maoni juu ya nguo uliyoivaa, kiatu ulichovaa hakifai, wengine watasema hata wasioyajua kabisa.

Ni kweli kila mmoja anatamani kuwa mtu mkuu lakini wale wanaoweza kuvumilia changamoto ndio huweza kudumu. Sio rahisi na nakwambia utapingwa na hata watu ambao hawajawahi kukuona. Utakutana na watu ambao ndio mara ya kwanza wamekuona na watakuchukia.

Utakutana na watu ambao hata hawajui umewezaje kufika hapo ulipo na wataanza kusema uliiba, ulitoa kafara, umehongwa na wengine watadiriki kutengeneza vita kabisa kukuangusha. Haya mambo yapo yanatokea na yanaendelea tunayaona kila siku ni lazima ujifunze na ujipange sawasawa kupambana nayo.

Mafanikio ni vita unakwenda kupambana na watu ambao wanataka wafaidi kile ambacho umekifanyia kazi miaka na miaka bila ya wao kutoa gharama kubwa. Unakwenda kupambana na watu walioshindwa Maisha na kitu pekee walichobakia nacho ni kukukosoa kwa kila unachokifanya hadi nguo unazovaa.

Hii ndio maana waliofanikiwa ni wachache, walioanza ni wengi lakini wanaoweza kuvumilia mpaka mwisho ni wachache. Wanaoweza kuvumilia na kuzishinda changamoto ni wachache. Jiandae kuwa tayari kukabiliana na lolote ambalo utakutana nalo katika safari yako. Washindi ni wale walioweza kushinda pambano.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading