Wengi wetu hupenda kuutumia mwezi huu vibaya katika kufuja pesa nyingi kwenye starehe na mwisho huaanza mwezi wa kwanza bila kitu chochote. Wewe kama mwanamafanikio unatakiwa ujue namna ya kufanya ili uweze kuendelea tena mwaka ujao. Simaanishi kwamba uache kufurahia mwisho wa mwaka ila nataka nikwambie safari bado usije ukatumia vyote wakati safari inaendelea. Unaweza kuuonyesha uma umekusanya kwa kiasi gani lakini hautakusaidia chochote. Mwezi wa kwanza unapokua mgumu utakua peke yako lakini wakati huu wa kutumia mtakuwa wengi sana.
Ni vyema sana kuutumia mwezi huu kama mwezi wa kufanya tathmini ya vyote unavyovifanya katika maisha yako. Mwezi ukiutumia katika kupitia malengo yako na kuangalia ni kwa kiasi gani umerudi nyuma au umesonga mbele. Hii itakusaidia sana ili ujue unajipanga vipi katika mwaka unaokuja ili usonge mbele Zaidi.

Kitu cha pili ambacho naweza kukushauri ufanye mwezi huu badala ya kustarehe. Nenda sehemu ya mbali sana na watu wewe pekee yako au na familia ukajitafakari maisha yako ya hapa duniani.
Siku unapoondoka utaacha kitu gani?
Litazame kusudi la Mungu aliloweka ndani yako je unaliishi?
Umeshafikia kiwango ambacho kinaonyesha dira?
Umefika wapi sasa na unaelekea wapi?

Kitu kikubwa ambacho kitakuletea Amani ya moyo sio mali au vitu vyote vya ulimwengu huu ni kusudi la wewe kuwepo duniani. Ni kweli unahitaji pesa, magari, nyumba nzuri na vyoote lakini kama utavipata nje ya kusudi kamwe hauwezi kuvifurahia. Utakua ni mtu unaesaka pesa tu kila siku bila kujua unazifanyia nini. Hakikisha umetambua kusudi la wewe kuwepo duniani na umeanza kuliishi na kufikia mafanikio.
Inawezekana kuna malengo ambayo ulikua umeyaweka na hayajatimia kwa kiasi ulichokua unataka. Sio wakati wa kukata tamaa jipongeze pia kwa hatua uliyofikia kitendo tu cha kuweka malengo na kuyafanyia kazi ni hatua ya ushindi mkubwa. Usiache kuandika tena malengo yako kwa mwaka ujao angalia ni  wapi ulishindwa na jaribu kujua ni wapi pa kujiongeza ili uweze kusogea Zaidi, iwe ni kwa kusoma vitabu Zaidi, kutafuta ushauri na mengine mengi. Weka malengo makubwa ambayo akili yako haiwezi kuyatimiza, unapoweka malengo yanayolingana na uwezo wako kamwe huwezi kusogea hapo ulipo. Malengo makubwa yanafanya akili yako itafute maarifa Zaidi nah ii itakusaidia wewe kujifunza mambo mengi. Ukiweka malengo makubwa unajikuta umeweza kuutumia uwezo wako mkubwa uliojificha ndani yako. Ukiweka malengo makubwa unapiga hatua Zaidi hata kama hutaweza kuyatimiza yote.

SOMA:  SIFA 5 ZA MTU ANAELEKEA KWENYE MAFANIKIO MAKUBWA

Hizi ni sehemu kuu tatu za kuweka malengo katika maisha yako. Muhimu unatakiwa ufahamu kuna malengo ya muda mrefu na malengo ya muda mfupi tunaposema muda mfupi ni kuanzia mwaka mmoja kurudi chini hadi siku. Malengo ya muda mrefu ni kuanzia Miaka mitatu na kuandelea. Malengo yanaandikwa kwenye kitabu (NoteBook) kama huna kitabu chako cha malengo anza mapema kwenda kukinunua na uwe nacho mkononi. Ukishindwa kuandika tuwasiliane kwa msaada Zaidi.

Malengo Binafsi
Hapa unajitazama wewe kama wewe maono uliyonayo kupitia kusudi lako unataka ufike wapi. Ndani ya muda mfupi yaani mwaka ujao unataka utimize kitu gani na gani. Baaada ya miaka mitano unataka ufikie hatua gani. Unataka kusoma vitabu vingapi kwa mwaka ujao?
Malengo binafsi upande wa kiroho unataka ufike hatua gani mahusiano yako wewe na Mungu. Andika kila kitu unachotaka kukitimiza katika mahusiano yako ya kiroho ni viwango gani unatamani kupanda ndani ya muda mfupi na muda mrefu. Kama mwaka huu ulikua mlegevu katika ibada ubadilike na uende viwango vikubwa Zaidi. Kama sadaka ulikua unatoa shilingi elfu moja basi mwaka ujao upande viwango ufikie hata elfu tano.

Malengo ya Familia/Mahusiano.
Unataka ufikie kitu gani katika muda mfupi na muda mrefu kwenye familia yako na kwenye mahusiano. Unatamani uwafanyie nini wale uwapendao ndani ya mwaka ujao na miaka mitano ijayo. Inawezekana wakawa ni wazazi, wadogo zako, mke/mume wako, watoto wako, mchumba/mpenzi wako. Ni muhimu sana uwe na malengo haya maana ndio yanaongoza maisha yako. Bibilia inasema unatakiwa uanze kuonyesha upendo na kuwajali watu wa nyumbani kwako kwanza. Hivyo ni vyema pia uweke malengo ya kuwasaidia sio kifedha pekee hata kwa ushauri na kuwaongoza waweze kufikia malengo yao. Wanunulie vitabu badala ya TV au majarida. Wapelekee vitu ambavyo vinaendana na vile wanavyotaka kuja kuwa. Makala nzuri kama hizi kuwa unawatumia ili na wao wajifunze wafikie ndoto zao.

Malengo ya Biashara/Fedha.
Hapa unaweka malengo juu ya kile kinachokuingizia kipato. Inawezekana umeajiriwa au una biashara zako binafsi. Una malengo gani ya kuongeza kipato chako au kukuza biashara zako. Uko kwenye ajira una mpango gani wa kuanza biashara ili uweze kuongeza kipato chako. Weka malengo ya muda mfupi mwaka ujao ni wapi unataka ufike na miaka mitano ijayo unataka ufike wapi. Kiasi gani cha pesa unataka uwe unaingiza baada ya muda Fulani.
Kama una kipaji hicho nacho tunasema ndio biashara yako pia maana ndio inaingiza kipato. Je unataka ufike wapi? Uwafikie watu kiasi gani mwaka ujao na miaka mitano ijayo?

SOMA: MAMBO 5 YANAYOONYESHA UNACHOKIFANYA SIO KUSUDI LAKO

Hizo ndizo sehemu kuu tatu za muhimu kuwekea malengo yako na ukayafanyia kazi. Inawezekana ulishaweka malengo tayari unayo lakini ni vyema sana uandike tena maana inakusaidia kuyaingiza katika ubongo wako wa kumbukumbu. Kitu cha muhimu sana unatakiwa ufanye ni kuandaa mpango wa kuyatimiza malengo. Unataka kupata pesa kiasi Fulani je unatakiwa ufanye nini? Unataka ufikie watu laki moja kwa uimbaji wako baada ya miaka mitano je ni kitu gani cha kufanya? Mpango ndio unakuwezesha wewe kuanza kuyafanyia kazi malengo yako. Kama ni kuweka akiba, kusoma vitabu na kadhalika. Je umejua ni watu gani unatakiwa kuambatana nao? Vitabu gani vya kusoma? Huo ndio mpango wako unatakiwa uwe. Mpango ndio unakupa njia na vitu vya kufanya ili uweze kutimiza malengo.

 

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading