Kwenye Maisha tunawahitaji watu sahihi. Watu Sahihi sio lazima wawe Wazuri kwetu wanaweza kuwa watu wabaya lakini ni sahihi. Kusudi la hao watu kwenye maisha yetu ndio litaamua usahihi wao.
Unaweza kukutana na mtu anakuchukia bila sababu halafu kwa kukuchukia kwake kukawa sababu ya wewe kusonga mbele Zaidi.
Kuna watu wakikupenda ndio wanakuharibu, badala ya kukusaidia wanakuwa wanakuharibu.
Mfano mtu wa karibu kwako ataumia akiona unateseka kumbe yale mateso yapo kwa kusudi. Yeye anaweza kukuhurumia akakusaidia kukuondoa kwenye mateso kumbe ndio amekuondoa kwenye kufikia mafanikio yako.
Mfano umepanga chumba ukafukuzwa kazi na hela ya kodi ikawa tatizo. Akili yako ikiwa katika kupambana ili upate hela akatokea ndugu yako akakwambia njoo kwangu ukae kwa muda hadi hali itakapokuwa nzuri. Kumbe wakati ule unawaza nini cha kufanya ndio ungepata suluhisho la kudumu la Maisha. Yeye kuja kukupa msaada kidogo ikawa sababu usifikiri tena.
Kuna watu Wazuri kwenye maisha yetu wanaweza kuwa sababu ya sisi kutokujitatulia Matatizo yetu wenyewe. Badala ya kufikiria suluhisho bora na la kudumu unamfikiria mtu ambaye anaweza kukukopesha hela maisha yasogeesogee kidogo.
Ndio maana ukiona watu hawakupi msaada ujue kuna kitu unatakiwa kujifunza. Nacho ni kujifunza Kusimama Mwenyewe.
Watu sahihi wanaweza kuwa watu wabaya kwetu ili kutufundisha vitu mbalimbali. Usimkimbie mtu ambaye hakuoneshi upendo wakati huo huo kuna mengi ya kujifunza kwake. Sio kila bosi atakuwa bosi mzuri.
Muhimu ni kuwa watu hawa makusudi yao kwetu yawe ni kutufanya tuwe bora Zaidi na sio kuanguka.
Unawahitaji watu sahihi na sio watu Wazuri kwako. Sio watu ambao watakuhurumia kila wakati.
Nakutakia Kila la Kheri.
Ubarikiwe sana.
Rafiki Yako Jacob Mushi
Asante sana makala nzuri sana hii.