Kuna mtu mmoja aliniambia Jacob naona mnataka kuwabadilisha watu waanze kufikiri kwamba ugumu wa Maisha yao wameusababisha wenyewe. Mbona kama mnataka kuwadanganya? Kuna vitu vingi sana vinahusika kuyafanya Maisha yawe magumu sio mtu binfsi pekee.
Mimi sijakataa hilo lakini nataka ufahamu kwamba pamoja na watu wengine kusababisha ugumu wa Maisha yako, pamoja mifumo mibovu, pamoja na vitu vingi ambavyo unaweza kusema sio wewe umesababisha bado inabaki pale pale wewe ndiye unaebeba majukumu ya Maisha yako. Wewe ndiye unapaswa kutatua matatizo ya Maisha yako unaemtupia lawama inawezekana hata hajui kama upo duniani.
Ni kweli Maisha ya wengi ni magumu na wanaishi katika hali za kutia huruma sana, ni kweli unaweza kusema unahitaji kuhurumiwa na mtu Fulani sana. Kabla hujawaza kusaidiwa na mtu mwingine hakikisha wewe binafsi kuna juhudi unafanya.
Unaweza kuendelea kulaumu lakini lawama hazitabadili chochote. Unaweza kukaa chini na kuanza kuangalia ni nani kakusababishia matatizo yako lakini hilo haliwezi kuwa suluhisho la matatizo. Njia pekee ya kutatua matatizo yako ni kukubali kuwajibika nayo. Yale ambayo unaweza kuyatatua yabebe mwenyewe hata kama unasema sio wewe umesababisha.
Unaweza kusema wazazi hawajakusomesha ndio maana una Maisha magumu, maneno hayo hayaondoi ugumu wa Maisha yako. Unaweza kusema serikali imeweka sera mbovu ndio maana watu hawapigi Hatua, sasa ukikaa unasubiria sera nzuri zitakuja lini? Wewe chukua Hatua kwenye kila ambacho kinawezekana kwa upande wako.
Acha kupoteza muda wako kutafuta mtu wa kumbebesha matatizo yako. Acha kupoteza muda kutafuta mtu wa kumtupia lawama juu ya ubovu wa Maisha yako. Chukua Hatua wajibika kwa Maisha yako, hakuna mtu mwingine anaewaza juu ya Maisha yako kama ambavyo unatakiwa wewe kuwaza. Chukua Hatua fanya kila linalowezekana ili usonge mbele.
Rafiki Yako,
Jacob Mushi
#UsiishieNjiani
Jiunge na Usiishie Njiani Academy Hapa https://jacobmushi.com/academy/
Huduma Zetu https://jacobmushi.com/huduma/