Katika Muda mchache ambao nimekuwepo hapa duniani, kuna aina ya watu mbalimbali ambao nimeshakutana nao. Kuna aina ya tabia ambazo nimeziona zimekuwa zinanishangaza sana na wakati mwinginze zimekuwa zinasikitisha sana.

Kuna aina ya tabia ukiwa nazo unaweza kujikuta umeuza utu wako na ukakosa kabisa umiliki wa Maisha yako. Wapo watu wengi ambao ninawafahamu wamekuwa na vipaji vizuri sana, na wamefika mbali sana kimafanikio (upande wa kufahamika na watu). Watu hawa wamejikuta wameingia katika mitego mibaya sana ambayo wakisema wajitegua basi ndio mwisho wao.

Yote hayo yanasababishwa na tabia mbalimbali ambazo mtu anaweza kuzijenga bila kujua kwamba zinaweza kuja kumletea madhara na kumfanya awe mtumwa kwa wengine.

Uvivu.

Unapokuwa mvivu siku zote unajiweka kwenye nafasai ya kutaka kupata urahisi Fulani kwenye jambo unalolifanya. Unapokuwa na kitu thamani ndani yako ukaleta uvivu watakuja watu wanaoweza kukitumia vizuri na watakuingiza kwenye mtego ambao watakuwa wanakufaidi kwenye kile kilichopo ndani yako.

Unaweza kujikuta unatumika na wengine wanafaidikia kwenye nguvu zako kwasababu ulikuwa mvivu. Na wakati mwingine unajikuta umejitengenezea mtego ambao haufai kutoka kabisa. Maisha yako yote yanakuwa ni utumwa kwa ajili ya mwingine aliekuwa na akili kukuzidi.

Kutaka Mafanikio ya Haraka.

Hii imekuwa ni hatari sana kwetu sisi vijana, unataka vitu ambavyo tunaviita mafanikio kama magari, nyumba nzuri, na pesa za kutumia. Cha ajabu sasa ni kwamba unavitaka vitokee kama mtu aliepanda tikiti miezi michache tu amevuna.

Kuna watu wakishaona kwamba unapenda vitu vya haraka wanajitokeza na wakupa kisha wanakuweka katika sehemu ambayo utakuwa mtumwa wao na kamwe unakuwa huwezi kutoka. Endapo utajaribu kutoka basi unakuwa umepoteza kila kitu ambacho walikuwa wamekupa.

Kukwepa Kulipa Gharama Unayostahili.

Kitu chochope unachokitaka hakikisha unalipia gharama inayostahili, usipende kuhurumiwa sana. Mfano ukienda kununua simu na ukajikuta unataka za bei rahisi sana mwisho wa siku unauziwa feki. Sasa kwenye Maisha ukitaka kukwepa kulipia gharama inayostahili utajikuta unakuwa mtumwa wa wengine.

Wapo watu wametafuta kazi kwa kutoa rushwa ya ngono na mwisho wake wakaambuliwa kuwa watumwa wa ngono kwa mabosi wao. Wapo waliotumia rushwa ili wapande vyeo na baadae wakajikuta wanapata aibu kubwa sana ya Maisha yao.

Chochote unachokitaka Maishani mwako ifahamu gharama unayotakiwa kulipia na pambana ulipie. Usikubali kupokea vya bure kwasababu vina gharama kubwa sana.

Bure ni ghali sana na wakati mwingine kwasababu ulipenda vya bure unaweza kujikuta bure imegharimu Maisha yako. Napenda kuwaambia watu kwamba kama kuna mtu asiekujua anataka kukupa kitu cha bure na sio ndugu yako. Basi hakikisha anachokupa unaweza kukilipia hata kama hutamlipa.

Ni bora mara mia uishi Maisha ya kawaida kuliko kutamani Maisha ambayo hujui undani wake ulivyo na hujui gharama zake za kulipia. Chochote unachokipenda kubali kukilipia gharama mwenyewe, usipende offa hasa kwa watu usiowajua vizuri.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading