Kwenye Safari yetu ya mafanikio mara nyingi pale inapotokea unataka kufanya kitu cha tofauti ambacho hujawahi kukifanya kabla unaanza kukutana na hofu ndani yako. Hofu mojawapo ni ya kukataliwa au kupingwa.
Unaweza kupata wazo zuri sana la biashara au la kuboresha kile unachokifanya lakini ukakutana na hofu ndani yako ambayo inakuzuia na kukutisha kwamba wazo lako litakataliwa.
Usikubali kabisa hofu hii ikakushinda kwani itakuwa sababu ya wewe kuishia na mawazo mazuri sana ndani ya kichwa chako.
Hofu hii imewasabisha wengi wakabakia na mawazo na mipango mizuri sana ndani ya vichwa vyao, wakashindwa kutoka pale walipo.
Kiukweli hofu hii ilishanikumba sana hasa mimi wakati naanza kuandika Makala. Lakini niliishinda na hata sasa nimeweza kuandika hadi kitabu.
Hofu hii inaweza kusababishwa na mtu kukosa uzoefu Fulani, mtu anajitazama anajiona hawezi kutokana na elimu yake ndogo au mazingira aliyokulia.
Unaweza kuishinda hofu hii kwa kuchukua hatua ya kufanya bila woga. Na inapotokea unapata hofu ya namna hii jitamkie maneno ya kujihamasisha na kujitia moyo.
Jiambie mimi ni mshindi, ninakwenda kufanikiwa kwenye wazo hili, ninaifkia ndoto yako, ninashinda changamoto na vikwazo vyote, siogopi kukataliwa au kupingwa.
Nikueleze tu jambo moja kama wazo lako litapingwa au kukosolewa unatakiwa uweze kulichukulia kwa pande mbili. Upande wa kwanza ni ukweli kwamba kuna sehemu halipo sawa kama ni hivyo lirekebishe. Upande wa pili ni wale wanaokupinga na kukukosoa kukuonea wivu na kutaka ushindwe. Ni lazima uweze kujua kwanini wamenipinga ili ulete matokeo bora na usonge mbele.
Kama walikupinga au kukukosoa kwasababu zao binafsi za wivu au chuki nakuhakikishia wazo lako linakwenda kukuletea matokeo makubwa sana ukichukua hatua.
Soma: Mafanikio ni Hatua
Ni muhimu sana ukatumia hekima kuchambua sababu za kukosolewa au kupingwa ukizichanganya unaweza kwenda kichwakichwa na ukaanguka huko mbele kumbe walipokukosoa walimaanisha urekebishe njia zako na sio kukukwamisha.
Jacob Mushi,
Author | Trainer | Entrepreneur