Ili maisha yetu yaweze kwenda vyema ni muhimu mtu kuwa na maana ya maisha yake anayoyaendesha. Kama maisha yako hayana maana unakuwa unapoteza muda wa kuishi hapa duniani.
Maana hii inatakiwa ianzie kwenye kujitambua wewe ni nani na unataka ukamilishe nini kabla hujaondoka hapa duniani. Hapo ndipo ulipo msingi mkuu wa maana ya maisha yako.
Watu wengi wamekuwa wakiishi maisha ya kawaida ambayo yanafanana na kila mtu. Yaani unafanya jambo kwasababu umeona watu wengi wanalifanya. Unaingia kwenye biashara Fulani kwasababu umeona kuna watu wamefanikiwa. Sio vibaya kufanya hivyo ila unatakiwa utambue pia kuna gharama wamelipa wakapata yale waliyonayo.
Hakuna maisha mabovu ambayo unaweza kuyaishi kama yale ya kusema bora mkono uende kinywani. Yaani hapo maana yake wewe unaishi ili ule! Na hayo maisha ndio watu wengi wanayaishi maisha ya kukata tamaa na yasiyo na mwelekeo. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema maisha yao hayana maana.
Amua leo kuacha kusema unafanya haya kwa ajili ya watoto wako na badala yake anza kujua kwanini upo duniani. Maana hata hao watoto wasingekuwepo bado kuna jambo ungetakiwa ufanye. Ni vizuri sana kupambana ili watoto wetu waishi maisha bora lakini inatakiwa tuende mbele Zaidi ili tuweze kufanya yale ambayo tumekusudiwa kuja kuyafanya hapa ulimwenguni.
Anza Leo Kutengeneza Maana kwenye Biashara Yako.
Ni kitu gani unatamani uone biashara yako inafanyia maisha ya wengine? (Thamani)
Ni Kwa kiwango gani hasa cha watu unatamani uwaguse na biashara yako? (Faida)
Unataka ifike kiwango gani kwa kujulikana?
Ukiweza kujiuliza maswali haya utapata maana Fulani ambayo itakuongoza kwenye kila unachokifanya haijalishi ni biashara au huduma Fulani unaitoa. Ukijua unataka uguse maisha ya watu wangapi kwa idadi kamili inayoeleweka (usiseme wengi) kama unataka watu elfu moja sema na anza kufanyia kazi uwafikie hao elfu moja. Kama unataka watu milioni moja sema andika chini weka na mipango ya kufanyia kazi kila siku ili uwafikie hao milioni moja.
Soma: Kuhitaji na Kutaka
Tengeneza maana ya Maisha yako unayoyaishi hapa duniani. Unataka uache alama gani? Watu wakikuona wewe wanasema nini? Watu watakukumbuka kwa kitu gani ulichokifanya hapa duniani? Kuna watu wameandika vitabu, wengine wameimba nyimbo, wengine wameigiza, wengine wamegusa maelfu ya watu kwa kuwapa ajira. Wewe unataka uguse vipi maisha ya wengine?
Kama bado una tatizo mpaka sasa hujajua ni wapi unaelekea na umepata nafasi ya kusoma Makala hii usikubali kuondoka hivi njoo tujifunze pamoja. Ukiwa na kitabu cha Siri 7 za Kuwa Hai Leo utajifunza mambo mengi sana ambayo yatakufanya uishi maisha yenye maana.
Your Partner in Success
Jacob Mushi