Unapowaza kuuza pekee kwenye biashara unakosa vitu vingine vya muhimu sana. Biashara ni kutatua matatizo ya wengine. Biashara ni kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora Zaidi ya yalivyo kuwa. Biashara ni kugusa maisha ya wengine.

Usikae kwenye biashara kwa lengo la kuuza tu. Embu ona unatatua jamii yako inayokuzunguka. Ona ukiyafanya maisha ya wengi kuwa bora. Ona ukiwarahisishia maisha wengine. Unapokuwa na mtazamo huu ndipo utaweza kufanya vizuri kuliko wengine. Unapokuwa na mtazamo huu utaweza kufanya bila ya kuchoka.

Shida kubwa ipo pale unapokuwa unafanya biashara kwa ajili ya kuuza peke yake upate pesa na maisha yako yasonge mbele. Hapo unakosa sababu za muhimu Zaidi za kukufanya wewe kuendelea kufanya biashara yako.

Watu wengi sana wanachokijua ni kwamba wapo kwenye biashara kutafuta pesa basi. Hawajui hata kama wanatatua tatizo gani. Hawajui kama wanasaidia watu kwa kile wanachokifanya na ndio maana wengi wanashindwa kufanya wanachokifanya hadi mwisho. Wengine wanakata tamaa kwasababu wao mtazamo wao uko kwenye pesa pekee.

Ukibadili mtazamo ukawaza mbali Zaidi utapata sababu nyingi za kukufanya wewe uendelee mbele Zaidi kwenye kile unachokifanya.

Kuuza ni sehemu ya biashara na ni sehemu ya muhimu sana. Na hii ni kwasababu ndio sehemu pekee inayofanya biashara yako ikue. Kama hakuna unachouza huwezi kusema upo kwenye biashara. Lakini kuuza inapokuwa sehemu ya pekee na ya muhimu haitakiwi kuwa sababu ya sehemu nyingine kusahaulika. Huduma bora kwa wateja. Kutambua kusudi la wewe kuwepo kwenye biashara (kwanini yako). Kama huijui kwanini yako utajikuta huna unapokwenda. Hakikisha unaijua kwanini yako.

Kama kwanini yako itakuwa kubwa ndio itategemea muda utakaodumu kwenye biashara yako. Kwanini yako ndio itaamua namna unavyofanya biashara yako. Kwanini yako inatakiwa iwe inagusa maisha ya watu wengine. Kwanini yako ikiwa inakugusa wewe pekee utashindwa kufanya vizuri inavyotakiwa.

Mfano wewe unafanya biashara ili uweze kupata ada ya kusomesha watoto. Kama ungekuwa huna watoto maana yake usingekuwa na biashara. Ukishapata ada ya watoto biashara unaweza usiifanye vizuri tena. Unaweza usiwahudumie wateja vizuri kama mwanzo. Kwasababu kwanini yako imeshajitosheleza.

Kwa mfano kwanini yako ikawa ni kufanya maisha ya watu kuwa bora kupitia bidhaa zako au huduma zako. Huwezi kuchoka hata siku moja kwasababu kila iitwapo leo kuna mtu anatakiwa apande viwango awe bora Zaidi ya alivyokuwa jana. Hivyo utakuwa kila siku unatamani kubuni njia mpya ya kuboresha maisha ya wengine.

Chukulia mfano wa makampuni makubwa na maarufu duniani kama wao wangekuwa na kwanini ndogo wasingeweza kufika hapo walipo sasa hivi. Wangekuwa wanafanya kwasababu zao binafsi au mahitaji ya familia zao labda wangeishia kujulikana kwenye miji yao pekee.

Badilisha mtazamo wako Ubadilishe biashara yako.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading