Katika mambo tunayofanya kila siku kwenye Maisha yetu pamoja na kuwa na imani kubwa, hamasa na matarajio makubwa hakuna mwenye uhakika asilimia mia moja kwamba mambo yatakuwa sawa. Ndio mambo yanaweza kuwa vile ulivyopanga lakini sio asilimia mia. Unachopaswa kujua ni kwamba kwa kila maamuzi unayofanya ni hatari unachukua hivyo tarajia chochote kile kinaweza kutokea.
Ukiweza kuwa na mtazamo huu ni mara chache utakuwa mtu wa majuto na kulalamika. Nimekutana na watu wengi wameingia kwenye biashara au vitu walivyoshawishiwa sana kwasababu walikuwa na mtazamo mmoja pekee wakaishia kupata maumivu makali yalipokuja matokeo tofauti.
Unachopaswa kutambua ni kwamba hakuna mwenye uhakika hata kama atakuhakikishia kwa kuapa. Ni muhimu sana ukajitengenezea mtazamo huu utakusaidia yanapotokea mambo ndivyo sivyo usitumie muda mwingi kulalamika na kukata tamaa bali ujue hatua za kuchukua haraka ili uendelee na mambo mengine.
Inawezekana ulianza biashara mambo yakaharibika ukapata hasara kubwa lakini wakati unaanza ulijijengea matarajio makubwa sana kiasi kwamba ukajiona hakuna linaloshindikana. Baada ya kuanza ukakutana na mambo tofauti kabisa hali hiyo inaweza kukufanya upooze kabisa na uone biashara haifai kabisa.
Nimekutana na watu wengi wameumizwa na biashara Fulani walizozifanya wakiwa na matarajio makubwa sana mwisho wake wakaumizwa baada ya mambo kuwa tofauti kabisa. Ndugu yangu endelea kusonga mbele ila elewa kwamba kwenye dunia hii mabaya na mazuri yapo kila mahali na yanatokea kila siku.
Wakati wewe unashangilia faida uliyopata kuna mwenzako ameondoka akiwa na masikitiko ya kutokuuza chochote leo. Sasa ukijua kwamba yanaweza kutokea hata kwako pia siku moja hutaweza kuumia kiasi cha kushindwa kuendelea au kuichukia biashara.
Ukiona umefikia mahali pa kuichukia biashara Fulani kwasababu tu ilikuumiza ujue bado hujakomaa vya kutosha. Ni sawa na uchukie kuishi kwasababu watu wanakufa.
Endelea kujifunza namna ya kuchukulia mambo mabaya yanayotokea kwako kila siku badala ya kuumia na kukata tamaa tafuta kitu cha kujifunza kwayo.
Badala ya kufikia mahali unawalaumu watu waliokushauri uanze biashara hiyo anza kuona kwa macho ya ziada kwamba kuna kitu umepata Zaidi ya hasara na ulichopata ni somo.
Tatizo lipo pale unapoangalia upande wa maumivu pekee na kusahau upande wa somo ulilopata.
Biashara unayoifanya sasa hivi huna uhakika asilimia mia hivyo chochote kinaweza kutokea unatakiwa ukichukulie kama mawimbi kwenye bahari. Usiseme kwanini mimi kwasababu mawimbi huwa hayajui kama kuna boti iliyobeba watu ipo mbele. Unachopaswa ni kushukuru kwa uzima na kile ulichobakia nacho.
UKIJIJENGEA MTAZAMO HUU NI RAHISI SANA KUWEZA KUSONGA MBELE ZAIDI.
Jacob Mushi
USIISHIE NJIANI
“Piga Hatua”