Wanaweza Kusema yule jamaa alifeli shule hajaweza kufika hata chuo hawezi chochote.

Wanaweza kusema yule dada kila mahusiano yamemshinda hawezi kutulia na mwanaume.

Wanaweza kusema pia pombe zitakuja kukuua siku moja.

Wanaweza kusema wewe ni mtu wa maneno maneno sana na huwa unaongea vitu visivyoeleweka.

Hayo yote na mengine ambayo wanaweza kusema juu yako ni maoni yao juu ya Maisha yako. Bado wewe binafsi una nafasi ya kufanya yaliyo mema na kubadili historia ambayo watu wanayo. Usikubali hata siku moja maoni ya wengine yakawa ni uhalisia wa Maisha yako.

Wanaweza kukupa kila aina ya majina lakini wewe ukiyakataa na kujipa yale ambayo unayotaka utaweza kufikia ushindi mkuu. Kikubwa sana ambacho unapaswa kutambua ni kwamba Mungu anakuwazia mema, hata kama wanadamu watakuita wewe ni jambazi, Malaya, mchawi na mengie yote mabaya ambayo unayofahamu bado yeye anakuwazia mema.

Usikate tamaa wala kurudi nyuma kwasababu ya maoni ya watu wengine. Maisha yako sio maoni yao, Maisha yako hayaendeshwi na mawazo yao. Lile Mungu alilopanga juu yako lazima litimie amua kukaa katika mstari na njia ambazo amekuelekeza na utaanza kuona matunda.

Unapoamka asubuhi hakikisha unasema maneno chanya juu yako. Bila ya kujali ni kitu gani kinaendelea kwenye Maisha yako wewe sema kile ambacho unataka kitokee. Kama unaumwa na unataka kuwa mzima sema mimi ni mzima, kama huna pesa na unataka kuwa na pesa sema nina pesa nyingi, biashara zangu zinaleta faida nyingi leo, halafu nenda kafanye kazi.

Chochote unachokisema juu yako, yule anaehusika katika kuvileta atavisogeza karibu yako. Ukisema leo nimeamka vibaya utashangaa siku nzima imekuwa mbaya. Usikubali kusema neon lolote baya juu yako, usikubali pia maneno yeyote mabaya yaliyosemwa juu yako yakatae kwa kusema maneno mazuri ambayo unayataka.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading