Najua unatamani kufanikiwa, sana. Kiasi kwamba ni kitu unachowaambia watu wengi kwenye maisha kwamba utafanya, kinachokufanya ufanye kazi kwa moyo wote, kinachokufanya ufikirie usiku na mchana kuhusu kesho. Mafanikio ni rahisi sana kuyapata ukijifunza nguvu iliyopo kwenye neno moja, HAPANA.

Hapana ni neno jema na baya pia. Kama vile kisu kilivyo ukikitumia vizuri ni kizuri, ukitumia vibaya ni kibaya sana. Leo ningependa niongelee nguvu iliyopo kwenye neno hapana kwaajili ya mema.
Wiki mbili zilizopita nilifanikiwa maishani, kuna kazi ambayo mtu aliniomba nifanye, nilipoitathmini sikuona umuhimu wa mimi kufanya kwasababu wapo wengine ambao wanaweza kuifanya lakini pia sikuwa vizuri kiafya, kwa mtu ambaye hawezi kusema hapana kwa watu nilifurahi sana kwa kusema hapana kwenye ile kazi, maana ulikuwa mwanzo wa mimi kuweza kusema hapana.

Neno hapana linaweza kukusaidia sana ukilitumia vizuri, neno hapana linaweza kukupeleka sehemu ambazo haujawahi kufika kwasababu tu umelisema hilo neno kwenye mambo fulani.

Embu fikiria katika mambo yote unayoyafanya, na kazi zote ambazo akili na nguvu zako zinaenda, je ni zote ulipaswa ufanye wewe? Je ni zote unatakiwa kuzifanya? Au ni kwamba umeshindwa kusema neno hapana kwenye hizo kazi?
Ili kufanikiwa unahitaji kufanya uchaguzi wa mambo ambayo utaweka nguvu zako na akili ili hizo zikufanikishe, sio kila jambo linakuhitaji wewe.

Jifunze kusema hapana kwa:
1. Kazi zinazoweza kufanywa na wengine- Iwe kwa kuwasaidia tu wajifunze au kwa kujipunguzia wewe majukumu.

2. Vitu vinavyochukua muda wako na kukupotezea malengo yako ya maisha.

3. Kila jambo unalolifanya ambalo unajua kabisa haulihitaji huko mbele ya maisha yako,na unalifanya tu kwasababu ya watu au kwasababu unatakiwa ulifanye.

4. Watu ambao hawakuongezei vitu kwenye maisha bali kukuharibia malengo, tabia yako njema na mipango.

5. Nafasi ambazo hazipo kwenye malengo yako- kama ulipanga jambo moja halafu nafasi inatokea ya kufanya jambo jingine usifanye tu kwasababu ni nafasi kama haiendani na malengo yako iache. Sio kila jambo unapaswa kufanya wewe kwenye maisha.

Jifunze kusema hapana, jifunze kuwaambia watu hapana, na zaidi jifunze kujiambia wewe mwenyewe hapana kwenye mambo ambayo unaona kabisa hauyahitaji kwenye maisha.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Jiunge na Usiishie Njiani Academy Hapa https://jacobmushi.com/academy/

Huduma Zetu https://jacobmushi.com/huduma/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading