Unaweza kufanya mambo makubwa kwenye Maisha yako na ukashindwa kusogea mbele tena kwasababu moja ya kulewa na yale matokeo. Jambo ambalo tayari umeshalifanya na ukashinda halitakiwi liwe ndio jambo unaloliongelea sana kwamba umelifanya. Waachie wengine walizungumzie wewe nenda katafute jambo jingine kubwa Zaidi la kufanya.

Sijasema usifurahie matokeo uliyopata bali nasema usifurahie sana hadi ukasahau kwamba bado upo safarini. Mafanikio ni vita, unaposhinda pambano moja usifurahie sana ukasahau kujiandaa kwa pambano linalokuja mbele.

Unatakiwa uwe na kiasi katika kufurahia ili uweze kujipanga tena kwa pambano jingine. Fahamu pia kuna wengi hawajafurahia mafanikio yako na wataanza kutafuta kila namna ya kukurudisha chini. Kama utakuwa umejisahau kwenye kufurahia utajikuta umeshindwa kujipanga kwa vita nyingine inayokuja.

Unapovuka hatua yeyote ya mafanikio usikubali kubaki kwenye hiyo hatua muda mrefu. Tafuta kusogea mbele kwa hatua nyingine tena. Hata kama mambo yako sawa na huna shida yeyote usikubali kubaki na hali ile ile jiongeze jaribu kusogea mbele Zaidi. Hii ni moja ya njia ambayo inawafanya waliofanikiwa waendelee kufanikiwa Zaidi. Hawakubali kubakia na yale matokeo waliyoyapata jana, kila leo wanajaribu vitu vipya vya kuwafanya waendelee kusonga mbele.

Angalia Zaidi kule mbele unapokwenda kila siku kuna mabadiliko mapya yanakuja ya aina mbalimbali. Ukikaa sehemu moja muda mrefu unaweza kuchelewa kuyapokea mabadiliko na hivyo kujikuta umekwamia hapo hapo ulipokaa muda mrefu.

Kila wakati penda kuangalia mbele na kuona ni mabadiliko gani yanaweza kuja na yataathiri vipi kile unachokifanya. Usikubali kuona wewe tayari ndio umefika na hakuna anaeweza kukutoa hapo. Mambo yanabadilika na unaweza kujikuta umebaki hapo na huna chochote.

Rafiki bila kujalisha wewe ni wa pekee kiasi gani na vitu vyako unavifanya kwa upekee kwa namna gani bado kuna watu watakuja wajaribu kuiga kile unachokifanya. Na kama sasa wewe umelala na umesharidhika na ule ushindi ulipata jana utajikuta wale waliokuja kukuiga wameweka mambo mapya na wakakuacha pale pale ulipokuwa umelalia.

Songa mbele, piga hatua kila wakati usikubali kuishia njia.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading