Kinachofanya ukwame ni vile unapoteza muda kurekebisha makossa ambayo uliyafanya. Kinachokurudisha nyuma ni pale unapotaka kubadilisha mambo ambayo uliharibu. Njia pekee ya kubadili au kuwa mbali na historia mbaya ya Maisha yako ni wewe kuamua kuanza kufuata hatma mpya ya Maisha yako baada ya kulijua kusudi la Maisha yako.
Unapowezekeza muda wako kwenye kusudi lako na kule unakotaka kufika unajikuta taratibu unaanza kuiacha mbali historia mbaya ya Maisha yako. Kuna mahali utafika utaanza kujishangaa kama ni wewe kweli kwasababu kusudi la Maisha yako limekubadilisha kabisa na ukawa mtu mpya.
Mzimu ni picha za kutisha ambazo tumekuwa tunajengewa na wazazi wetu tangu tukiwa wadogo. Mara Nyingi zinaweza zisiwe na ukweli lakini kwasababu ya Imani ambayo unakuwa umeshaijenga inakusababishia uanze kuona mauzauza hata ya uongo.
Siku moja kwasababu ya Imani hizi za mzimu nilijikuta Napata hofu sana kutoka nje usiku kujisaidia kwasababu kuna bibi kizee mmoja nilikua namuone amesimama nje ya Nyumba. Nilikua nikiamini kwamba bibi kizee huyu atakuwa ni mojawapo ya mizimu ile ambayo tumekuwa tunaambiwa.
Siku moja nikachoka kuaogopa na nikaamua kuufata mzimu ule na kumulika na tochi. Maajabu ni kwamba nilikutana na kisiki cha mti ambacho kimewekewa takataka na nguo za zamani yaani zilizochakaa. Kuanzia hapo nikaanza kupata akili mpya kwamba Kumbe vitu vingi tunavyoogopa tulidanganywa.
Sasa ukiachana na mizimu ya aina hiyo kuna mizimu mingi uliambiwa na bado huwa unaiona kwenye Maisha yako. Uliambiwa kwenu ni maskini wote hivyo haiwezekana kufanikiwa. Usipokula kuua mzimu huu utaendelea kukutesa hadi siku unaondoka hapa duniani.
Umaskini wa kwenu haukuhusu wewe, unapaswa kujua kwamba Maisha yako yana sababu zake. Wewe umezaliwa kwa kusudi unachopaswa kufanya hapa duniani ni kuliishi kusudi lako. Achana na umaskini wa kwenu. Njia pekee ya kubadilisha Maisha yako ni kutumia kile ambacho Mungu ameweka ndani yako kwa kiwango cha juu sana kuliko mwanadamu mwingine yeyote. Ukiweza kufikia kiwango hiki basi wewe umeshabadilisha kila kitu hadi umaskini wa wajomba na mashangazi zako.
Mzimu wa Kujikataa. Unajikataa kwa kujilinganisha na wengine, ukiwaone watu wanafanya vizuri kuliko wewe, au wamesoma kuliko wewe, wametoka kwenye familia zenye pesa kuliko wewe unajikuta unajikataa. Unajiona huwezi, unajiona hustahili. Huu nao ni mzimu unapaswa kuuawa lazima ukubali kuuzika kabisa. Ili upone tatizo hili unapaswa kukubali kufanya mauaji kwa mzimu huu.
Mzimu wa soma kwa bidii uje uishi Maisha mazuri. Ndio huu nao ni mzimu mwingine ambao umekuwa unawatesa wengi sana. Ukweli hii picha umekuwa unajengea tangu ukiwa chekechea hadi umefika chou ni hatari sana. Umekuwa unaambiwa unataka kuwa kama kina Fulani ambao wako mtaani tu. Soma kwa bidii elimu ndio itakutoa. Ukweli ni kwamba wengi tumetoka shuleni na vyeti na sio elimu.
Umemaliza chou ukitegemea kuishi yale Maisha ambayo wazazi wako walikuwa wanakwambia lakini mpaka sasa hujaweza kuyaona. Ukweli unapaswa kuua mzimu huu, ili upone unapaswa kukubali kwamba ulidanganywa. Kubali kwamba jamii yako ilidanganywa na ikaendelea kukudanganya. Mtu yeyote anaweza kuwa na Maisha mazuri kama ataamua kuyatafuta na sio kwasababu amesoma.
Ubaya ni kwamba mzimu huu umewashika wote waliosoma na ambao hawajasoma. Waliobaki mtaani waliambiwa ukishafeli shule ndio huna Maisha tena. Sasa mzimu huu ukawa unawafanya wajione kwamba tayari ndio wameshaharibu hawana njia ya kufanikiwa tena. Wakaamua kuendelea na Maisha yao ya kawaida ya kimaskini kama wale ambao walikuwa wanawaambia.
Mzazi wako anakwambia ukichezea elimu utakuja kuishi Maisha mabovu kama yangu, ukimuangalia ndio ukata tamaa kabisa. Sasa cha ajabu ni kwamba picha wanayoijenga juu ya waliosoma si ya kweli ni picha ambayo wamajitengenezea na wakakutengenezea wewe pia.
Ukikaa wewe ambaye hujasoma unawaona waliosoma wanaishi Maisha mazuri sana. Na wale ambao wamesoma Maisha wanayoishi yanakatisha tamaa kwasababu walijengewa picha ambayo haikuwa ya kweli.
Ukweli ni kwamba Maisha mazuri hayaletwi na elimu peke yake lazima ukubali kufanya kazi kwa bidii na kufanya kazi kwa bidii ni kwa mtu yeyote yule anaejua nini anataka. Ukisoma kwa bidii soma lakini ondokana na picha hii ya Maisha mazuri yanaletwa na kwenda shule.
Rafiki yangu ipo mizimu mingi ambayo umejengewa na inatembea ndani ya kichwa chako imekufanya uishi kama mtu aliechanganyikiwa. Kuna mizimu inakusumbua kuhusu mahusiano yako bila kuiua hutakaa uishi kwa amani.
ZOEZI LA KUFANYA:
Baada ya kusoma Makala hii maana yake wewe unakwenda kupona. Sasa chukua kitabu chako cha kuandika mambo ya muhimu uanze kuandika yale mambo ambayo yanakutesa yote. Ukimaliza nataka uanze kuchambua moja baada ya jingine.
Ni wapi ulidanganywa? Kama ni mahusiano yanakutesa ni kwamba kuna matarajio ulikuwa nayo basi ulipoingia ukakutana na matarajio mengine hapo ndipo penye shida.
Kama ulidanganywa maana yake kuna ukweli ulifichwa unapoujua ukweli basi unakuwa huru. Tafuta ukweli ni upi katika lile jambo ambalo limekuwa linakusumbua. Ufanyie kazi ukweli na utakuwa huru.
Tazama chanzo cha kila tatizo tafuta suluhisho ni lipi. Ukiwamba njoo tuongee Zaidi njia za kutatua na kuondoa kabisa mzizi wa tatizo lako. Kuna mengi huwezi kuyaondoa mwenyewe lakini pale tu unapopata kiongozi wa kukusaidia uweze kuyaondoa matatatizo yako.
Hakikisha Unapowasiliana nami uwe umeandika yote ambayo yamekuwa yanakutesa.
Rafiki Yako,
Jacob Mushi