Mwaka 2004 nikiwa shule ya msingi Mdawi tulichelewa kuingia darasani mimi na wanafunzi wenzangu na tukachapwa sana viboko. Sababu ambayo ilitufanya tuchelewe kuingia darasani ilikua ni matunda ya mizambarau iliyokuwa nyuma ya shule bondeni.

Mizambarau hii ilikuwa imezaa sana na kulikuwa na miti ya mizambarau Zaidi elfu moja kwenye bonde lile la shule yetu ya msingi. Kwa kuwa ndio ulikuwa msimu wa mizambarau wanafunzi wengi waliacha kula chakula cha mchana na kuishia kula zambarau.

Siku hiyo baada ya mimi kujiingiza katika kundi la wanafunzi ambao tulienda bondeni au mtoni kula zambarau hizo nikapokea kipigo cha fimbo kutoka kwa Mwalimu mkuu ndipo nikaikumbuka hadithi ya zambarau zile.

Kumbe zambarau zile zilioteshwa na wazazi wetu kipindi wanasoma katika shule ile. Wengine waliotesha zambarau zile kama adhabu baada ya kuchelewa kufika shuleni au kufeli masomo darasani.

Baada ya kukumbuka hili nikasema Kumbe kile amacho unakifanya sasa hivi unaweza kuona kama ni adhabu Fulani lakini Kumbe miaka 20 ijayo kuna kizazi chako kitafaidi sana matunda ya kazi yako unayofanya leo.

Kuna vitu unavifanya leo kwako unaona kama ni Mzigo mzito, kwasababu huona matunda yake kwa wakati huo. Inawezekana huoni kama leo au kesho unaweza kupata faida lakini miaka ijayo kizazi chako kitafurahia matunda yake.

Ni vyema kuangalia yale tunayofanya kwa sasa yanaleta matunda gani kwa kizazi kijacho. Unaweza ukaona mbona napoteza muda lakini Kumbe kazi yako ya sasa ni maandalizi ya chakula kwa ajili ya kizazi kinachokuja miaka 50 mbele. Usiogope hata kama kazi yako haionekani ya maana sasa ipo siku unaweza usiwepo hata huku duniani lakini watu wakasema kulikuwa na mtu mmoja anaitwa Jacob Mushi aliandika kitabu hiki.

Usikatishwe tamaa na watu ambao labda hawaoni mchango wa kile unachokifanya sasa. Inawezekana sio kwa ajili yao, inawezekana wewe umezaliwa uandae kitu kwa ajili kizazi kijacho. Kuna mahali Mungu anataka utengeneze miaka ijayo ili watu waje waone faida yake.

Siku zote penda kuwatazama wengine kuliko wewe mwenyewe ni lazima utafanikiwa. Angalia wengine wanafadikaje kuliko hata wewe unavyofaidika kwasababu wao wakifaidika ndipo na kwako pia kunaongezeka sana.

Nakutakia Wakati Mwema.

#TAFAKARI360

#USIISHIENJIANI

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

https://jacobmushi.com/huduma/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading