Ukiona kuna mtu ana muda mwingi sana wa kufuatilia unachokifanya na siku zote anakuja na mawazo hasi tu na wala hujamwajiri afanye hivyo basi ujue tu huyu Ameshapoteza Muelekeo wa Maisha Yake Mwenyewe.

Huo ndio ukweli kama yeye Maisha yake hana muda nayo ndio anapata muda wa kufuatilia Maisha yako maana yake yeye ameshayapoteza Maisha yake. Usitegemee ushauri wake utafaa kwa chochote kwasababu angekuwa mtu anaejielewa huo muda wa kukufuatilia kila unachokifanya angeuwekeza kwenye Maisha yake binafsi.

Hivi unajua kwamba mtu aliekutangulia mbele yako sio rahisi sana awe anakuona unavyokuja nyuma yake? Na kama ni hivyo ukiona anatumia muda mwingi kukufuatilia wewe ulieko nyuma yake na kukuzuia basi ujue ameshakuogopa anahisi utakuja kumpita na kumuacha. Sasa cha ajabu ni kwamba kila mtu ana Maisha yake na malengo yake. Mtu akikupita haikupunguzii wewe chochote.

Kamwe usikubali Maneno ya watu wa aina hii yakupotezee kasi na mwelekeo wako katika kuyatimiza malengo yako na maono yako makubwa. Hawa ni watu waliokata tamaa au wanaoogopa yale mambo makubwa ambayo unataka kuyafanya.

Usikatishwe tamaa na mtu aliekata tamaa. Usirudishwe nyuma na mtu alieko nyuma yako. Songambele watazame wale ambao wameshakutangulia usiwatazame wale ambao walishindwa. Muda wako ni thamani sana usije kuutumia kujali walioshindwa wamesema nini juu yako.

Rafiki yangu nataka ukumbuke kwamba yeyote anaepoteza muda wake kukuzuia basi hana mwelekeo wa Maisha yake, ni muoga, anahisi utakuja kumpita Kumbe wewe hata hushindani na mtu mwingine, anajaribu kukuvuta ufanane nae.

Kama yote hayo ni hivyo kwanini ujali? Kwanini uumie eti kisa kuna mtu mmoja anataka kukukwamisha wakati umeshajua huyu ameshayasahau Maisha yake anatumia muda mwingi kuangalia Maisha ya wengine? Bila kujali ni nani kwako usipoteze muda wako kuumia maana utakosa mwelekeo katika mambo yako ya muhimu.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading