Category Archives: MAFANIKIO MAKUBWA

525; HEKIMA: Ni Wewe.

Ni wewe utawajibika pale unapoingia kwenye matatizo bila kujali ni nani aliyeyasababisha.

Ni wewe utatakiwa kuchukua hatua pale mambo yanapokuwa magumu kwasababu ya uzembe unaoufanya sasa.

Ni wewe utakalipa gharama za ulaji mbovu unaokula sasa pale utakapoanza kusumbuliwa na magonjwa.

Ni wewe utakaelipa gharama ya ujinga unaoundekeza sasa hivi, unaambiwa ujifunze hutaki,

Unaambiwa uweke akiba unapuuza kwasababu sasa hivi unapata kila unachokitaka.

Unaambiwa ujenge tabia za mafanikio hutaki, unaona wewe hakuna wa kukuelekeza kwasababu tayari unakila unachotaka.

Ni wewe utakaewajibika kwa lolote litakalotokea kwenye maisha yako kutokana na uzembe au kwa namna yoyote ile.

Wale uliokuwa unawaona hawana maana wakati wakikushauri watakutoza fedha ukiwarudia kwenda kuwaomba ushauri tena.

Wale uliokuwa unaona kama wanafuatilia maisha yako, hawajielewi, wenyewe hawana maisha kama yako kwa hivyo hawawezi kukushauri chochote utawafata kwa gharama kubwa.

Sikutishi nakwambia ukweli, ile gharama unayokwepa kulipa sasa hivi utakuja kuilipa siku moja huko mbeleni, bahati mbaya sana utailipa na riba.

Kama unaona ni ngumu sana sasa hivi kuweka akiba kwasababu pesa zipo za kutosha ipo siku utaingia gharama ya kukopa mambo yakiwa mabaya.

Ni wewe ndiye utakaewajibika kwa makosa yako, sisi tutaendelea kubaki kama washauri tu.

Ni muhimu kuchukua hatua sasa kwasababu hata ukikwepa lazima utakuja kulipia gharama kwa kile ulichokikwepa.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

512; Mimi Ni Mtenda Dhambi Kuliko Wewe.

Siku Moja nilikuwa nawaza hivi, “Siku Nikifa Nikakuta hakuna Mungu Nitacheka Sana”, Sauti nyingine ndani yako Ikasema, “Hapo Utakapokuwa Unachekea ni Nani Huyo Atakuwa Amekutengenezea” Ndugu Yangu Mungu Yupo, Ukatae Ukubali…………………

Kuna ule mtazamo wa kuwaona watu ambao wamefanya mambo makubwa, na wale wenye ushawishi mkubwa sana kuwa hao ni watu wasio na makossa kabisa. Na hiyo hupelekea pale wanapokosea kitu cha kawaida kabisa mfano ndoa kuvunjika, tunawaona kama vile ni wamefanya makossa makubwa sana.

Wakati huo huo kuna watu wengi sana kila mara ndoa zao zimekuwa na matatizo makubwa na wanaishia kuachana bila hata kujulikana.

Rafiki napenda ufahamu kwamba kila mmoja ana jambo ambalo huwa ni udhaifu wake. Kila mmoja kuna kitu ambacho kimekuwa kinamshinda mara kwa mara hata wewe ukijitafakari utaona kunai le dhambi ambayo kila mara hukuangusha. Hata kama hakuna anaeijua basi wewe mwenyewe na Mungu wako ndio mnaijua vizuri.

Kama kwako kuna kitu kama hicho basi ina maana kwamba kila mtu kuna jambo ambalo limekuwa likimsumbua pia. Kila mmoja kuna ka udhaifu Fulani huwa kinamwangusha. Ndio maana katika wanafunzi 12 wa Yesu bado kulikuwa na mmoja Yuda Iskariote aliemsaliti Yesu kwa tamaa ya fedha. Bado pia kuna Petro ambaye alimkana Yesu mara tatu, kuna mwingine huyu anaitwa Thomaso alishindwa kabisa kuamini kama Yesu amefufuka mpaka amshike kwa mikono yake.

Sasa kama Yesu mwenyewe alijua amechagua watu 12 wazuri na bado wakaonekana wenye madhaifu mimi ni nani niseme sina dhambi hata kidogo? Ndio maana nataka kukwambia mimi ni mtenda dhambi kuliko wewe, Neema ya Mungu tu ndio hunisaidia, napenda ulijue hili ili usije kunihukumu siku moja ukisikia makosa niliyoyatenda. Vilevile hata wewe kuna kitu najua ni udhaifu wako, unakusumbua mara kwa mara, umekuwa unajaribu kuacha lakini unakwama.

Nataka uwe na mtazamo chanya kwenye mambo ya wengine uweze kuchukuliana na kila mtu kwasababu kila mmoja ana jambo ambalo linamsumbua sana ndani yake hata kama hatakwambia. Na haya mambo ndio mara zote huwaga ni siri za ndani ya watu.

Unaweza kuwa unasema sasa Jacob unataka kusema kila mmoja awe huru kufanya dhambi ile ambayo inamshinda? Hapana hapo utakuwa umenielewa vibaya, maana yangu hapa ni kuwa wewe utambue mtu akiwa hai na akakosea kwa chochote kile bado ana nafasi ya kutubu mbele za Mungu wake.

Inawezekana Mtu ametenda uovu ukasambaa sana akatubu kwa Mungu akapata msamaha na wewe ukaendelea kumhukumu, kumsema vibaya, kumuandika vibaya, ikatokea umekufa ukaenda kuhukumiwa kwa kutenda dhambi ya kuhukumu wengine. Maana yangu hapa kama wewe huna nafasi ya kwenda kumshauri au kumsaidia mtu aliekosea usipoteze muda wako kumsema na kumzungumzia kwasababu huenda unasema yule ni mtenda dhambi sana, kumbe alishatubu siku nyingi na kusamehewa.

Hakuna haja ya kuzungumza mabaya ya mtu kama huwezi kuzungumza mazuri yake. Hakuna haja ya kumchukia mtu alietenda maovu bali twapaswa kumuombea Mungu amsaidie. Na wewe binafsi ukishaujua udhaifu wako basi ni jukumu lako, kuhakikisha unakaa mbali na vile vitu ambavyo vinakupelekea kuitenda dhambi. Ukishatambua kile ambacho kinakuangusha kirahisi ni jukumu lako kutafuta msaada kwa watu wenye uwezo kwenye tatizo lako wakusaidie uweze kujidhibiti.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

501; Kutafuta Samaki Msituni.

Jaribu kuvuta picha upo katikati ya msitu, unatafuta samaki. Umejipanga kila kitu unacho, una chambo za kutosha, una vifaa vya kubebea na pia una hamasa na nguvu za kutosha kutafuta samaki. Kitu kimoja ambacho kitakufanya uendelee kuwatafuta samaki Maisha yako yote ni kwamba ulikuwa huna ufahamu kwamba samaki hawapatikani msituni wanapatikana majini.

Haijalishi utakuwa na hamasa kubwa kiasi gani, haijalishi utakuwa umejipanga vya kutosha kiasi gani endapo hao samaki utakuwa unawatafuta porini ni ngumu kupata samaki. Mwisho wa siku utarudi na kusema hakuna samaki, utarudi na kusema kupata samaki sio kazi rahisi.

Hadi pale atakapotokea jamaa mmoja akwambie kuwa unakosea samaki huwa hawapatikani porini wanapatikana kwenye maji, unaweza kwenda kuwatafuta mtoni, bwawani, ziwani au baharini. Kinyume nah apo utaishia kuamini kwamba sio rahisi kupata samaki kwasababu wewe ulikuwa unawatafuta porini.

Kwenye Maisha yetu tuna watu wengi waliokuwa wanatafuta samaki porini wakakosa. Ukikutana nao hawa watakwambia na kukuhakikishia kabisa kwamba huwezi kupata samaki kwasababu wao walitumia Miaka kadhaa kuwatafuta na hawajapata. Ukikosea kidogo kuwaamini bila kujua kuwa walikuwa wanatafutia porini utaishia Njiani.

Ni vyema sana kabla hujamsikiliza mtu anaekwambia haiwezekani basi umuulize maswali ya kutosha kwasababu wengine kwao imekuwa haiwezekani kwasababu walikuwa wanatafutia samaki porini badala ya kwenye maji. Usikubali kusikiliza tu kila taarifa kwasababu wengine wanaweza kukupotosha kwa kutokuelewa kwao.

Kuna mengi tangu zamani umekuwa unaaminishwa kwamba haiwezekani au kitu Fulani huwezi kupata mpaka upitie mahali Fulani kumbe ni uongo. Na kizazi hata kizazi kimekuwa kinaamini uongo wa namna mbalimbali. Sasa mtu anasema huwezi kufanikiwa kama hujasoma, au ukifeli shule ndio Maisha yako yameharibika halafu wewe unamuamini na unakata tamaa kabisa baada ya kufeli shule. Kumbe hiyo haikuwa kweli bado una uwezo wa kwenda kutafuta kile unachokitaka endapo utajua kwamba mahali kinapopatikana ni wapi.

Naomba ujiulize sana Swali hili, Je Hiki ninachokitafuta nakitafutia sehemu sahihi?

Maana yawezekana hupati unachokitafuta kwasababu unakitafutia sehemu ambayo sio sahihi.

Mtu anapokwambia haiwezekani usikubali kirahisi hata kama ni mtu unaemuamini sana kwasababu huenda nay eye alikuwa anatafuta samaki porini bila kujua halafu akakuaminisha kwamba na wewe hutaweza kupata samaki maishani mwako.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

500; Ikatokea Umesahau Kila Kitu.

Jiunge na Mtandao Huu Uwe Unapokea makala nzuri kama hii moja kwa moja kwenye email yako

Weka email Yako hapa

Endapo itatokea umelala kisha ukaamka hukumbuki kitu chochote kuhusu wewe yaani unachoweza kufanya ni kuongea tu. Lazima utajikuta katika hali ya kujiuliza maswali mengi sana ambayo kwa haraka haraka hayatakuwa na majibu.

Swali la kwanza la muhimu utajiuliza, Mimi ni nani? Kwanini nipo Hapa? Natakiwa kufanya nini? Hutaanza kujiuliza kuhusu pesa, magari nyumba au chochote kingine Zaidi ya kutaka kujifahamu wewe kwanza. Hata ukiyaona magari huwezi kusema gari langu liko wapi kwasababu bado hata hujajua kama ulishawahi kuwepo hapa duniani. Utajaribu kukumbuka vitu mbalimbali, utawatazama watu waliokuzunguka na vitu vilivyokuzunguka labda vinaweza kukusaidia kukumbuka wewe ni nani.

Nimetaka ujaribu kuwaza hivi ili utambue vitu vya muhimu sana kwenye Maisha yako kabla ya vingine ni wewe kutambua wewe ni nani na kwa nini upo hapo ulipo. Achana na maswali nitapata wapi hela au nataka kumiliki gari, nataka kumiliki nyumba wakati bado hujajielewa wewe ni nani. Utakosea sana endapo utaanza kukimbizana na vitu ambavyo hata hujui maana yake.

Endapo utasahau kila kitu swali la muhimu na la msingi ni MIMI NI NANI? Na linalofuata ni KWANINI NIPO HAPA? Endapo ungeweza kuwa na ufahamu wa kujiuliza maswali haya wakati ule ulipozaliwa tungekuwa na dunia ya tofauti kwasababu kila mmoja angekuwa anajitambua.

Kitu cha kushukuru ni kwamba hata sasa bado una nafasi ya kujiuliza kila wakati wewe ni nani na kwanini upo hapa. Haijalishi umesahau kila kitu au unafahamu vitu vingapi. Bado una uwezo wa kujitambua wewe ni nani na kwanini upo hapa duniani.

Jiulize hili swali kama una wasiwasi na wewe. Kama unahisi inawezekana unachokifanya sio chako, unahisi labda mahali ulipo sio sahihi ulitakiwa uwe sehemu nyingine, endelea kujiuliza swali, MIMI NI NANI? Usiishie tu kujiuliza tafuta vitu ambavyo vinaweza kukupa mwongozo wa kutambua wewe ni nani. Jaribu kukumbuka vitu ambavyo vitakupa mwangaza, angali ulipokuwa mdogo ulipenda kufanya vitu gani. Jaribu kukumbuka kitu gani kilikuwa kinaleta furaha sana ndani ya moyo wako.

Utagundua tu wewe ni nani na utaacha kukimbizana na vitu ambavyo hukuzaliwa kuja kufanya hapa duniani.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako.

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

499; Njoo Uchukue Milioni Kesho.

Ikitokea Rais amesema vijana wote kesho tukutane nae pale Posta Dar es Salaam Atakuwa anagawa Tsh 1m ukafanyie chochote unachotaka, popote ulipo bila kujali unafanya nini bado nafasi ya kwenda utaipata. Huwezi kusema samahani naomba nije kuchukua keshokutwa, huwezi sema nitakuja jioni naomba unisubiri, huwezi kusema umepata dharura akutumie kwa mpesa.

Utakachokifanya ni kwenda na kuzichukua hizo hela. Utaahirisha kila ulichokuwa unakifanya ili tu ukazipate hizo milioni moja. Unajua ni kwanini? Jibu ni rahisi sana milioni moja ni ya muhimu sana kwako. Kwanini imekuwa ya muhimu sana? Kwasababu inaweza kutatua matatizo Fulani ambayo umekuwa nayo muda mrefu.

Hakuna atakaechelewa, inawezekana usafiri ukawa ni wa shida ghafla kwasababu ya wingi wa watu watakaokusanyika pale viwanjani.

Ukweli ni kwamba ile milioni moja ambayo kila mmoja anaweza kuifuata pale Posta kwa gharama yeyote inawezekana ikapatikana mara mia ya hiyo endapo tu ule umuhimu, utayari kutokutoa udhuru wala sababu ya aina yoyote ungeiweka kwenye ndoto na malengo yako.

Kinachofanya uairishe malengo yako ni nini? Kwanza hujayapa umuhimu, pili hujayaamini yaani bado wewe mwenyewe una wasiwasi kama ni kweli inawezekana. Kama ungekuwa na uhakika nayo kama ulivyokuwa na uhakika wa hiyo milioni basi kuna matokeo makubwa ungeyaona.

Kama ungeweza kuamka mapema hivyo kila siku kwa ajili ya ndoto zako miaka michache sana ungeshapiga hatua kubwa.

Embu yape umuhimu malengo yako, embu zipe umuhimu ndoto zako kwasababu miaka michache ijayo zitakuwa zinakupa milioni nyingi kila siku. Kwasababu miaka michache ijayo hizo shida zinazokufanya ukaifuate hiyo milioni pale posta zitakuwa zimeisha endapo ndoto yako itatimia.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

498; Huwezi Kunizuia Tena.

Unajua hakuna kisichowezekana kwenye dunia hii endapo utakuwa umeweka nia ya dhati ya kutaka kufanikisha. Endapo utaamua kwamba hakuna chochote kinachoweza kukuzuia tena, ukikubali kila kitakachokuja mbele yako kiwe kibaya au kizuri utaamua kukitumia kama silaha ya kukusogeza mbele.

Nikuambie kitu mimi sijazaliwa kwenye familia yenye nafuu ya aina yeyote, nimewahi kukosa ada ya shule, nimewahi kukosa nguo za kuvaa, nimewahi kulala njaa pia. Unaweza kusoma Zaidi hapa www.jacobmushi.com/kuhusu. Kuna nyakati niliwahi kukosa ada ya shule nikasema niende nikaombe msaada mahali. Nikaambiwa hatuwezi kukusaidia mwambie mama yako akusomeshe.

Hapo ndipo nilipata hasira sana nikasema sitasoma lakini nitafanikiwa, sitaenda chuo kikuu lakini lazima siku moja historia ya Maisha yangu isomwe na walioenda chuo kikuu. Na ukweli hili linakwenda kutokea, sio kwa bahati mbaya, bali ni kwasababu nilishafanya maamuzi haya miaka mingi iliyopita. Ndugu yangu wewe unakutana na changamoto unarudi nyumbani unalia unasema basi bado hujajua uchungu wa Maisha.

Changamoto yeyote inayokuja mbele yako unapaswa kusema nitaitumia kusogea mbele, sitakubali inifanye nirudi nyuma. UGUMU WA MAISHA NA MAZINGIRA YAKIKUIKANDAMIZA CHINI USIONEKANE NA WALA USISIKIKE, JITAHIDI KUTAZAMA KILA FURSA INAYOKUJA MBELE YAKO ILI UWEZE KUINUKA HATA KAMA ILIKUWA NI KUPIGA KELELE TU PIGA KWA NGUVU ZOTE. ENDELEA KUFANYA HIVI KILA WAKATI.”

Chochote kinachokuja mbele yako hata kama ni kifo kinataka kutokea usikubali kuruhusu iwe ni mwisho wako mbaya fanya kila uwezalo umalize kwa ushindi. Kamwe usiongee maneno juu yako yale usiyoyataka. Acha watu waseme maneno mabaya kwako, acha waseme huwezi, acha waseme wewe kwenu hamtakaa mfanikiwe, acha waseme wewe hujawahi kufanikisha chochote cha maana lakini kamwe wewe usijisemee maneno kama hayo. Jisemee maneno ya ushindi. Hata kama jana huweza kufanya chochote leo unaweza kufanya.

Usikubali chochote kikuzuie, unajua ukiwa umefungiwa kwenye chumba chenye giza halafu hakuna sehemu ya kutoka wakati mwingine unaweza kuwaza kukata tamaa. Lakini bado kunakuwaga na nafasi kila wakati ya wewe kutoka, na nafasi hiyo ni ile siku mpya unayoendelea kuiona kila siku. Kama umeona jua tena leo maana yake ipo nafasi ya wewe kutoka kwenye hicho chumba chenye giza.

Bado naendelea kusema, kama bado hujafa mpaka sasa, basi usikate tamaa kwenye ndoto yako.

Nakutakia Kila la Kheri

Rafiki Yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

495; Toka Kwenye Maboksi Ya Wengine.

Kuna vile unajihisi wewe haupo sawa kisa tu maisha yako hayafanani na ya fulani. Elimu yako haiendani na watu fulani, huna cheo cha maana kwenye kazi.

Naomba nikwambie hayo yote ni maboksi watu waliojitengenezea Usikubali kuishi kwenye maboksi ya wengine Tengeneza boksi lako linalokutosha.

Sio lazima uwe na elimu kubwa kama wengine, sio lazima uwe na cheo kikubwa, unaweza kuwa kitu kingine cha tofauti kabisa na ukawa mtu wa maana na mwenye heshima.

Jitambue wewe ni nani na kwanini upo hapa duniani halafu anzia hapo.

INATOSHA.

#WEWEMPYA

www.jacobmushi.com/coach

494; Endapo Maisha Yote Uliyoishi Mpaka Sasa Yangekuwa ni Ndoto.

Habari Rafiki, leo naomba ujiulize swali hili la msingi sana. Iwapo umeamka asubuhi halafu ukajitazama ukakuta umerudi nyuma miaka 10 au ishirini iliyopita. Yaani kumbe yote yaliyotokea kwenye Maisha yako miaka kumi iliyopita ilikuwa ni ndoto tu ulikuwa unaota usiku wa jana.

Swali la msingi la kujiuliza je hiyo ndoto itakuwa inatamanisha kuwa kweli? Je ungependa hiyo ndoto uliyoiota iwe kweli miaka kumi ijayo? Hayo Maisha uliyoyaona kwenye ndoto ndio unayoyataka? Majibu ya wengi naamini yatakuwa ni HAPANA.

Hapana kwasababu Maisha ya wengi yamekuwa ni magumu na ya kubahatisha. Huenda hujapata ile elimu uliyokuwa unataka, huenda kwenye Maisha uliyoishi mpaka sasa imekuwa ni maumivu kila wakati. Huenda umepitia magumu yasiyoelezeka kiasi kwamba ukiwambiwa uyarudie hayo Maisha hutakubali hata kidogo.

Naomba nikwambie kitu kimoja, UNAWEZA KUYAFANYA YAWE KAMA NDOTO NA UKAANZA UPYA LEO. Maisha yako yote uliyoishi tangu jana kurudi nyuma unaweza kuamua tu yawe kama ni ndoto na ukaanza upya leo kutengeneza ile ndoto unayoitaka kwenye Maisha yako. Ni kweli itakuwa ngumu kidogo kwasababu mengi yameacha alama kabisa kwenye Maisha yako. Yameacha alama ambazo hazitaweza kuwa ndoto tena. Lakini ukiamua kutokushikilia yale yaliyopita ndio utaweza kushikilia yale yanayokuja na kuyatimiza.

Achilia yaliyopita yapite uendelee kufanyia kazi ile ndoto yako. Ukweli ni kwamba kama bado upo hai mpaka sasa na umeweza kusoma Makala hii una nafasi ya kutengeneza upya yale Maisha ya ndoto yako. Ni kweli kuna vitu havitafaa kurekebisha tena  lakini hivyo havikuhusu viache tengeneza vile vinavyofaa kutengeneza. Fanyia kazi vile ambavyo vipo kwenye uwezo ambao Mungu amekupa.

Nakutakia kila la Kheri katika Kutengeneza Maisha ya Ndoto Yako.

Rafiki Yako

Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach