Category Archives: MAISHA NA MAHUSIANO

525; HEKIMA: Ni Wewe.

Ni wewe utawajibika pale unapoingia kwenye matatizo bila kujali ni nani aliyeyasababisha.

Ni wewe utatakiwa kuchukua hatua pale mambo yanapokuwa magumu kwasababu ya uzembe unaoufanya sasa.

Ni wewe utakalipa gharama za ulaji mbovu unaokula sasa pale utakapoanza kusumbuliwa na magonjwa.

Ni wewe utakaelipa gharama ya ujinga unaoundekeza sasa hivi, unaambiwa ujifunze hutaki,

Unaambiwa uweke akiba unapuuza kwasababu sasa hivi unapata kila unachokitaka.

Unaambiwa ujenge tabia za mafanikio hutaki, unaona wewe hakuna wa kukuelekeza kwasababu tayari unakila unachotaka.

Ni wewe utakaewajibika kwa lolote litakalotokea kwenye maisha yako kutokana na uzembe au kwa namna yoyote ile.

Wale uliokuwa unawaona hawana maana wakati wakikushauri watakutoza fedha ukiwarudia kwenda kuwaomba ushauri tena.

Wale uliokuwa unaona kama wanafuatilia maisha yako, hawajielewi, wenyewe hawana maisha kama yako kwa hivyo hawawezi kukushauri chochote utawafata kwa gharama kubwa.

Sikutishi nakwambia ukweli, ile gharama unayokwepa kulipa sasa hivi utakuja kuilipa siku moja huko mbeleni, bahati mbaya sana utailipa na riba.

Kama unaona ni ngumu sana sasa hivi kuweka akiba kwasababu pesa zipo za kutosha ipo siku utaingia gharama ya kukopa mambo yakiwa mabaya.

Ni wewe ndiye utakaewajibika kwa makosa yako, sisi tutaendelea kubaki kama washauri tu.

Ni muhimu kuchukua hatua sasa kwasababu hata ukikwepa lazima utakuja kulipia gharama kwa kile ulichokikwepa.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

511; Unakimbilia Wapi? Tazama Pembeni Yako.

 Haya Ndio Maisha yetu kwenye vitu vingi tunavyopitia kila siku, Soma kisa hiki ujifunze: “Habari kaka Jacob, ninaomba ushauri wako kuhusu hili. Ni mwaka wa tatu sasa tangu nikutane na binti mmoja na nikampenda sana. Nina tabia moja huwa sikati tamaa haswa pale ninapokuwa nimekipenda kitu Fulani maishani mwangu. Nimekuwa naamini kwamba ipo siku tu kitakuwa cha kwangu.

Binti huyu kila nilipokuwa namfuatilia ili niweze kuwa nae amekuwa akinisumbua sana, kila wakati ananipiga chenga za namna mbalimbali. Nimejitahidi kumpatia kila anachokitaka, lakini alikuwa anasema anatamani tuwe marafiki tu kwani tukiingia kwenye mahusiano tutakuwa tunagombana na mwisho wake tutaachana.

Kwasababu nilimpenda kwa dhati ikanibidi nimsikilize tu. Sasa huu ni mwaka wa tatu tumekuwa karibu kama marafiki na nilijiapiza sitaingia kwenye mahusiano mengine kwakuwa niliona kama ananipima uaminifu wangu.

Wiki mbili zilizopita kanijia huku akilia machozi na kuniomba msamaha anasema ananipenda sana na yupo tayari kuwa na mimi kuanzia sasa. Anadai amegundua alikuwa anapoteza muda na watu ambao hwakuwa wanampenda bali kumtumia tu.

Hilo halikuwa shida, kubwa Zaidi ananiambia kwamba mwanaume aliekuwa nae kwenye mahusiano kwa Zaidi ya miaka 3 akijua anampenda, amempa ujauzito na kumkimbia. Huku akidai hawezi kuwa nae kwenye Maisha yake.

Naomba ushauri wako, nifanyeje, ukweli huyu binti nampenda sana, changamoto ni huu ujauzito alioniletea, sielewei kama ananipenda kweli au ni kwasababu ya matatizo aliyopitia tu. “

Kijana huyu amekumbwa na mkasa huu mzito sana kwenye Maisha yake. Ni kweli inaumiza sana, nataka na wewe ujifunze kitu kwenye huu mkasa, je ni vitu gani umekuwa ukivikimbilia ukijua ni vyako mpaka pale ulipopoteza?

Huyu binti amekua akishikamana na watu ambao hawakumpenda na akasahau kabisa kuona mtu aliekuwa karibu yake wakati wote. Inawezekana hata wewe kuna vitu umekuwa unavishikilia ukidhani ni vyako na ukasahau vile ambavyo ni vyako siku zote vipo karibu na wewe siku zote.

Embu jaribu kutazama ni nani huwa yupo karibu yako kila mara? Ukiwa na shida, ukiwa na raha yupo. Wakati wowote ukimhitaji anakuwa yupo tayari kwa ajili yako. Naomba nikwambie watu hawa ni wa thamani sana kwenye Maisha yetu. Usikubali kuwa mtu ambaye unaiona thamani yao wakati wa matatizo tu.

Kuna watu wanaweza kukwambia wanakupenda kwa maneno matamu lakini kuna watu wanakupenda kwa kufanya vitendo kwenye Maisha yako. Kuna watu ambao hujawahi kusikia wakisema NAKUPENDA lakini wamekuwa wakifanya mambo makubwa kwenye Maisha yako kuliko neno hilo na NAKUPENDA.

Jifunze kutofautisha watu wanaouhitaji mwili wako na wanaouhitaji moyo wako, jifunze kutofautisha watu wanaozihitaji pesa zako na wanaokuhitaji wewe kwenye Maisha yao. Wapo wengi wanaonekana kama wanatuhitaji sisi kumbe wanahitaji vile vitu tulivyonavyo. Ukishindwa kujua haya utaishia kutumbukia kwenye shimo kila mara.

Rafiki Yako

Jacob Mushi.

510; Ninajihisi Kama Mtu Aliekwama Kwenye Tope.

“Kaka Jacob naomba ushauri wako, sijui hata nifanyeje, huu ni mwaka wa 5 sasa nimekuwa najaribu kuingia kwenye mahusiano tofauti tofauti lakini naambulia kuachwa na kuumizwa. Mara ya mwisho nilikutana na mkaka mmoja ambaye tulianza nae mahusiano kwa haraka na motomoto sana lakini mwisho wake nikaja kuona anaanza kupunguza mapenzi taratibu, kaanza kupunguza mawasiliano na mpaka akafikia kupotea kabisa.

Yaani niseme kwamba yaani imekuwa tabia ni hiyo tu. Wanakuja kwa kasi na baada ya muda wanaondoka kama vile hatukuwahi kujuana kabisa. Sasa mpaka nakutumia ujumbe huu nimejaribu kutafakari sana sijapata majibu. Nimejaribu kuangalia labda ni mimi mwenyewe nina matatizo, labda kuna mahali nakosea, bado sijapata majibu.

Najihisi kama mtu aliekwama kwenye tope zito na kila ninaempa mkono anivute anaishia kuniacha kwenye tope hilo. Embu nishauri kaka nifanye nini? Muda unakwenda na sijawahi kudumu kwenye mahusiano Zaidi ya miezi mitatu, wengi wanaishia mwezi mmoja mpaka wa tatu.

Nifanyeje?”

Nataka nizungumze na mtu ambaye anajihisi amekwama kwenye tope la namna mbalimbali. Inawezekana na wewe unapitia hali ambayo unajihisi umekwama kwenye tope zito na unahitaji mtu wa kuja kukutoa humo.

Mara nyingi hali mbalimbali tunazopitia kwenye Maisha yetu huwa hazihitaji watu wengine kuja kututatulia bali sisi wenyewe unakuta tunahitaji kupata utulivu mkubwa wa akili ili tuweze kuona ni wapi tunakosea tuchukue hatua. Wakati mwingine ukiwa kwenye tope na mtu akaja kwenye Maisha yako akagundua kweli upo kwenye tope ni rahisi kukukimbia kwasababu anajua akijaribu tu kukusaidia na yeye atajikuta kanasa hapo uliponasa wewe.

Wakati mwingine sio kila anaekukimbia inamaanisha wewe ndio una matatizo hapana wengi hukimbia kwasababu ya woga walionao, wanahisi watanasa kwenye mtego uliokunasa.

Vitu vya Kuzingatia:

Punguza Kasi,

Ukiwa mtu mwenye kasi kubwa sana hasa mahusiano yanapokuwa mapya ni rahisi kuchokana mapema kabla hujafika popote. Lazima ujifunze kwenda taratibu na kama mtu sio sahihi utaona tu atakukimbia kwasababu yule asie na lengo la kudumu na wewe akiona wamcheleweshea anachokitaka ataamua kuondoka. Usiruhusu mtu ayajue madhaifu yako mapema wakati hamjajenga msingi mzuri ambao unaruhusu kuwekana wazi kwa baadhi ya mambo ambayo ni siri.

Soma: Acha Kutafuta Samaki Msituni

Tumia akili yako Zaidi Kuliko Hisia,

Fanya maamuzi kwa kutumia Akili, Usiruhusu Hisia Zikuongoze.

Ukitulia Ndio Utaweza Kujua Kile Unachokitaka.

Wakati mwingine Subira Hutujulisha kama ni kweli tunavihitaji vitu Fulani au vinaweza tu kupita. Ukipanda mbegu mbichi ya mahindi ni rahisi sana kuoza kuliko kuota, kwenye Maisha yetu kuna vitu vinatakiwa vipewe Subira ili viweze kukomaa ili vifae kutumia kwenye hatua nyingine. Mara kwenye mapenzi tunawahi sana kufanya vitu ambavyo vilitakiwa vipewe muda ili vikomae kwanza. Kwasababu kama havijakomaa urahisi wa kuharibika unakuwa mkubwa.

UVUMILIVU;

Uvumilivu wahitajika sana sio kuvumilia mateso hapana nazungumzia kuvumilia hasa ule wakati unakihitaji kitu na hakipo au hakipatikani kwa wakati huo. Kuweza kudhibiti hisia zako na kusema sitaingia kwenye mahusiano kwa wakati huu ambapo nipo kwenye hisia kali za kuhitaji mtu ni jambo la muhimu sana kwasababu hisia kali zaweza kukusababishia uanzishe mahusiano na mtu asiye sahihi au ambaye hatadumu tena baada ya hisia zako kuisha.

MAOMBI;

Kumuomba Mungu ni muhimu sana kwasababu yeye atakupatia muongozo na pia atakukwepesha na wale ambao hawakutakiwa kuja kwenye Maisha yako. Mungu atakuepusha na vile vitu ambavyo havikutakiwa kutokea kwenye Maisha yako.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

501; Kutafuta Samaki Msituni.

Jaribu kuvuta picha upo katikati ya msitu, unatafuta samaki. Umejipanga kila kitu unacho, una chambo za kutosha, una vifaa vya kubebea na pia una hamasa na nguvu za kutosha kutafuta samaki. Kitu kimoja ambacho kitakufanya uendelee kuwatafuta samaki Maisha yako yote ni kwamba ulikuwa huna ufahamu kwamba samaki hawapatikani msituni wanapatikana majini.

Haijalishi utakuwa na hamasa kubwa kiasi gani, haijalishi utakuwa umejipanga vya kutosha kiasi gani endapo hao samaki utakuwa unawatafuta porini ni ngumu kupata samaki. Mwisho wa siku utarudi na kusema hakuna samaki, utarudi na kusema kupata samaki sio kazi rahisi.

Hadi pale atakapotokea jamaa mmoja akwambie kuwa unakosea samaki huwa hawapatikani porini wanapatikana kwenye maji, unaweza kwenda kuwatafuta mtoni, bwawani, ziwani au baharini. Kinyume nah apo utaishia kuamini kwamba sio rahisi kupata samaki kwasababu wewe ulikuwa unawatafuta porini.

Kwenye Maisha yetu tuna watu wengi waliokuwa wanatafuta samaki porini wakakosa. Ukikutana nao hawa watakwambia na kukuhakikishia kabisa kwamba huwezi kupata samaki kwasababu wao walitumia Miaka kadhaa kuwatafuta na hawajapata. Ukikosea kidogo kuwaamini bila kujua kuwa walikuwa wanatafutia porini utaishia Njiani.

Ni vyema sana kabla hujamsikiliza mtu anaekwambia haiwezekani basi umuulize maswali ya kutosha kwasababu wengine kwao imekuwa haiwezekani kwasababu walikuwa wanatafutia samaki porini badala ya kwenye maji. Usikubali kusikiliza tu kila taarifa kwasababu wengine wanaweza kukupotosha kwa kutokuelewa kwao.

Kuna mengi tangu zamani umekuwa unaaminishwa kwamba haiwezekani au kitu Fulani huwezi kupata mpaka upitie mahali Fulani kumbe ni uongo. Na kizazi hata kizazi kimekuwa kinaamini uongo wa namna mbalimbali. Sasa mtu anasema huwezi kufanikiwa kama hujasoma, au ukifeli shule ndio Maisha yako yameharibika halafu wewe unamuamini na unakata tamaa kabisa baada ya kufeli shule. Kumbe hiyo haikuwa kweli bado una uwezo wa kwenda kutafuta kile unachokitaka endapo utajua kwamba mahali kinapopatikana ni wapi.

Naomba ujiulize sana Swali hili, Je Hiki ninachokitafuta nakitafutia sehemu sahihi?

Maana yawezekana hupati unachokitafuta kwasababu unakitafutia sehemu ambayo sio sahihi.

Mtu anapokwambia haiwezekani usikubali kirahisi hata kama ni mtu unaemuamini sana kwasababu huenda nay eye alikuwa anatafuta samaki porini bila kujua halafu akakuaminisha kwamba na wewe hutaweza kupata samaki maishani mwako.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

500; Ikatokea Umesahau Kila Kitu.

Jiunge na Mtandao Huu Uwe Unapokea makala nzuri kama hii moja kwa moja kwenye email yako

Weka email Yako hapa

Endapo itatokea umelala kisha ukaamka hukumbuki kitu chochote kuhusu wewe yaani unachoweza kufanya ni kuongea tu. Lazima utajikuta katika hali ya kujiuliza maswali mengi sana ambayo kwa haraka haraka hayatakuwa na majibu.

Swali la kwanza la muhimu utajiuliza, Mimi ni nani? Kwanini nipo Hapa? Natakiwa kufanya nini? Hutaanza kujiuliza kuhusu pesa, magari nyumba au chochote kingine Zaidi ya kutaka kujifahamu wewe kwanza. Hata ukiyaona magari huwezi kusema gari langu liko wapi kwasababu bado hata hujajua kama ulishawahi kuwepo hapa duniani. Utajaribu kukumbuka vitu mbalimbali, utawatazama watu waliokuzunguka na vitu vilivyokuzunguka labda vinaweza kukusaidia kukumbuka wewe ni nani.

Nimetaka ujaribu kuwaza hivi ili utambue vitu vya muhimu sana kwenye Maisha yako kabla ya vingine ni wewe kutambua wewe ni nani na kwa nini upo hapo ulipo. Achana na maswali nitapata wapi hela au nataka kumiliki gari, nataka kumiliki nyumba wakati bado hujajielewa wewe ni nani. Utakosea sana endapo utaanza kukimbizana na vitu ambavyo hata hujui maana yake.

Endapo utasahau kila kitu swali la muhimu na la msingi ni MIMI NI NANI? Na linalofuata ni KWANINI NIPO HAPA? Endapo ungeweza kuwa na ufahamu wa kujiuliza maswali haya wakati ule ulipozaliwa tungekuwa na dunia ya tofauti kwasababu kila mmoja angekuwa anajitambua.

Kitu cha kushukuru ni kwamba hata sasa bado una nafasi ya kujiuliza kila wakati wewe ni nani na kwanini upo hapa. Haijalishi umesahau kila kitu au unafahamu vitu vingapi. Bado una uwezo wa kujitambua wewe ni nani na kwanini upo hapa duniani.

Jiulize hili swali kama una wasiwasi na wewe. Kama unahisi inawezekana unachokifanya sio chako, unahisi labda mahali ulipo sio sahihi ulitakiwa uwe sehemu nyingine, endelea kujiuliza swali, MIMI NI NANI? Usiishie tu kujiuliza tafuta vitu ambavyo vinaweza kukupa mwongozo wa kutambua wewe ni nani. Jaribu kukumbuka vitu ambavyo vitakupa mwangaza, angali ulipokuwa mdogo ulipenda kufanya vitu gani. Jaribu kukumbuka kitu gani kilikuwa kinaleta furaha sana ndani ya moyo wako.

Utagundua tu wewe ni nani na utaacha kukimbizana na vitu ambavyo hukuzaliwa kuja kufanya hapa duniani.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako.

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

499; Njoo Uchukue Milioni Kesho.

Ikitokea Rais amesema vijana wote kesho tukutane nae pale Posta Dar es Salaam Atakuwa anagawa Tsh 1m ukafanyie chochote unachotaka, popote ulipo bila kujali unafanya nini bado nafasi ya kwenda utaipata. Huwezi kusema samahani naomba nije kuchukua keshokutwa, huwezi sema nitakuja jioni naomba unisubiri, huwezi kusema umepata dharura akutumie kwa mpesa.

Utakachokifanya ni kwenda na kuzichukua hizo hela. Utaahirisha kila ulichokuwa unakifanya ili tu ukazipate hizo milioni moja. Unajua ni kwanini? Jibu ni rahisi sana milioni moja ni ya muhimu sana kwako. Kwanini imekuwa ya muhimu sana? Kwasababu inaweza kutatua matatizo Fulani ambayo umekuwa nayo muda mrefu.

Hakuna atakaechelewa, inawezekana usafiri ukawa ni wa shida ghafla kwasababu ya wingi wa watu watakaokusanyika pale viwanjani.

Ukweli ni kwamba ile milioni moja ambayo kila mmoja anaweza kuifuata pale Posta kwa gharama yeyote inawezekana ikapatikana mara mia ya hiyo endapo tu ule umuhimu, utayari kutokutoa udhuru wala sababu ya aina yoyote ungeiweka kwenye ndoto na malengo yako.

Kinachofanya uairishe malengo yako ni nini? Kwanza hujayapa umuhimu, pili hujayaamini yaani bado wewe mwenyewe una wasiwasi kama ni kweli inawezekana. Kama ungekuwa na uhakika nayo kama ulivyokuwa na uhakika wa hiyo milioni basi kuna matokeo makubwa ungeyaona.

Kama ungeweza kuamka mapema hivyo kila siku kwa ajili ya ndoto zako miaka michache sana ungeshapiga hatua kubwa.

Embu yape umuhimu malengo yako, embu zipe umuhimu ndoto zako kwasababu miaka michache ijayo zitakuwa zinakupa milioni nyingi kila siku. Kwasababu miaka michache ijayo hizo shida zinazokufanya ukaifuate hiyo milioni pale posta zitakuwa zimeisha endapo ndoto yako itatimia.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

498; Huwezi Kunizuia Tena.

Unajua hakuna kisichowezekana kwenye dunia hii endapo utakuwa umeweka nia ya dhati ya kutaka kufanikisha. Endapo utaamua kwamba hakuna chochote kinachoweza kukuzuia tena, ukikubali kila kitakachokuja mbele yako kiwe kibaya au kizuri utaamua kukitumia kama silaha ya kukusogeza mbele.

Nikuambie kitu mimi sijazaliwa kwenye familia yenye nafuu ya aina yeyote, nimewahi kukosa ada ya shule, nimewahi kukosa nguo za kuvaa, nimewahi kulala njaa pia. Unaweza kusoma Zaidi hapa www.jacobmushi.com/kuhusu. Kuna nyakati niliwahi kukosa ada ya shule nikasema niende nikaombe msaada mahali. Nikaambiwa hatuwezi kukusaidia mwambie mama yako akusomeshe.

Hapo ndipo nilipata hasira sana nikasema sitasoma lakini nitafanikiwa, sitaenda chuo kikuu lakini lazima siku moja historia ya Maisha yangu isomwe na walioenda chuo kikuu. Na ukweli hili linakwenda kutokea, sio kwa bahati mbaya, bali ni kwasababu nilishafanya maamuzi haya miaka mingi iliyopita. Ndugu yangu wewe unakutana na changamoto unarudi nyumbani unalia unasema basi bado hujajua uchungu wa Maisha.

Changamoto yeyote inayokuja mbele yako unapaswa kusema nitaitumia kusogea mbele, sitakubali inifanye nirudi nyuma. UGUMU WA MAISHA NA MAZINGIRA YAKIKUIKANDAMIZA CHINI USIONEKANE NA WALA USISIKIKE, JITAHIDI KUTAZAMA KILA FURSA INAYOKUJA MBELE YAKO ILI UWEZE KUINUKA HATA KAMA ILIKUWA NI KUPIGA KELELE TU PIGA KWA NGUVU ZOTE. ENDELEA KUFANYA HIVI KILA WAKATI.”

Chochote kinachokuja mbele yako hata kama ni kifo kinataka kutokea usikubali kuruhusu iwe ni mwisho wako mbaya fanya kila uwezalo umalize kwa ushindi. Kamwe usiongee maneno juu yako yale usiyoyataka. Acha watu waseme maneno mabaya kwako, acha waseme huwezi, acha waseme wewe kwenu hamtakaa mfanikiwe, acha waseme wewe hujawahi kufanikisha chochote cha maana lakini kamwe wewe usijisemee maneno kama hayo. Jisemee maneno ya ushindi. Hata kama jana huweza kufanya chochote leo unaweza kufanya.

Usikubali chochote kikuzuie, unajua ukiwa umefungiwa kwenye chumba chenye giza halafu hakuna sehemu ya kutoka wakati mwingine unaweza kuwaza kukata tamaa. Lakini bado kunakuwaga na nafasi kila wakati ya wewe kutoka, na nafasi hiyo ni ile siku mpya unayoendelea kuiona kila siku. Kama umeona jua tena leo maana yake ipo nafasi ya wewe kutoka kwenye hicho chumba chenye giza.

Bado naendelea kusema, kama bado hujafa mpaka sasa, basi usikate tamaa kwenye ndoto yako.

Nakutakia Kila la Kheri

Rafiki Yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

497; Chuki Za Kijinga.

Unaweza ukashangaa sana kumkuta mama anawafurahia Watoto wa wengine na kucheka nao vizuri sana lakini wakati huo huo anamchukia sana mtoto alieko nyumbani kwasababu ni mtoto wa nje. Ulishawahi kukutana na mtu anakuchukia tu kwasababu wewe umefikia hatua Fulani ambayo yeye hajafika utafikiri labda wewe ndio sababu ya yeye kutokufika hapo.

Ni ajabu sana kwenye jamii zetu tuna watu wana tabia hizi za ajabu za chuki zisizo na maana yeyote. Chuki hizi zinasababisha mtu anaanza kupanga na kutenda mabaya juu ya wengine ambao hawana hata sababu na Maisha yao. Sasa Rafiki yangu kabla hatujaendelea embu jiulize kuna mtu yupo ndani ya moyo wako unamchukia tu bila ya sababu? Eti unafikiri kuna kitu kama hicho kumchukia mtu bila sababu? Kwanini sasa usimpende bila ya sababu?

Maisha haya ili tuweze kuyafurahia vyema ni kwa kuoneshana upendo, chuki ndio zinayafanya Maisha yawe magumu Zaidi. Chuki ndio zinaondoa amani kwenye dunia yetu. Ni ujinga sana kujifanya unampenda mtoto wa jirani halafu pale nyumbani kwenu kuna mtoto unamchukia kisa tu sio wa ukoo wenu, aliletwa kuja kuishi hapo.

Ni unafiki uliopitiliza kujifanya unaipenda ndoa ya watu Fulani hivi ambao hamna uhusiano wa damu halafu hapo kwenu unamchukia yule wifi yako au shemeji yako bila ya sababu tu. Huo ni ujinga au mimi naweza kuuita ni utoto yaani ni kwamba kuna sehemu kwenye akili yako bado haijakua bado una utoto ndani ya akili yako bila kujalisha una miaka mingapi.

Embu Rafiki yangu achana na hizi chuki za ajabu ajabu, hazina maana. Hizi ndio zinasababishaga watu waendeane kwa waganga na wengine kuwekeana sum utu. Ni ujinga mtu tena ujinga wa kiwango cha juu kusema humpendi mtu bila ya sababu. Tena unakuta mtu anasema yaani huyo naona damu zetu hazijaendana kabisa. Yaani wewe una matatizo kabisa, damu hazijaendana ndio nini. Wewe una tabia za kichawi hizo embu ziache, anza kuwapenda watu bila ya sababu. Mtu hajakufanyia chochote unamchukia tu bila ya sababu ili iweje sasa.

Kama wewe unamjua mtu mwenye chuki za aina hii embu mtumie asome apate uponyaji. Hayo ni mapepo, na ukiendekeza hautaenda mbinguni, yaani chuki ni sawa na uuaji. Kuua mtu huanza kwa kumchukia.

Nikutakie kila la kheri

Rafiki Yako Jacob Mushi.

Hii ya Kuchukia kijinga naomba uishie Njiani usiendelee nayo sawa.

www.jacobmushi.com/coach

495; Toka Kwenye Maboksi Ya Wengine.

Kuna vile unajihisi wewe haupo sawa kisa tu maisha yako hayafanani na ya fulani. Elimu yako haiendani na watu fulani, huna cheo cha maana kwenye kazi.

Naomba nikwambie hayo yote ni maboksi watu waliojitengenezea Usikubali kuishi kwenye maboksi ya wengine Tengeneza boksi lako linalokutosha.

Sio lazima uwe na elimu kubwa kama wengine, sio lazima uwe na cheo kikubwa, unaweza kuwa kitu kingine cha tofauti kabisa na ukawa mtu wa maana na mwenye heshima.

Jitambue wewe ni nani na kwanini upo hapa duniani halafu anzia hapo.

INATOSHA.

#WEWEMPYA

www.jacobmushi.com/coach