Vile unavyoianza siku yako inaweza kuwa sababu ya kuwa na siku mbaya sana au siku nzuri sana. Kuna makossa unaweza kuwa unayafanya bila kujua wakati unapoamka na yakaigharimu siku yako nzima.
Kwanza lazima uamke mapema sana ili kuweza kuwa na siku nzuri. Unapochelewa kuamka na kuanza kukimbia kimbia kwasababu muda umekupita unakosa umakini wa kufanya maamuzi bora asubuhi. Unaweza kufika sehemu yako ya kazi ukajikuta umesahau vitu vya muhimu kwasababu ya haraka zako.
Ili uweze kuamka mapema ni vyema pia ukalala mapema. Tukisema kulala mapema ni angalau ikifika saa tano usiku uwe umeshalala na sio upo kitandani unachezea simu. Kwa kawaida ukilala saa tano saa kumi au kumi na moja unaweza kuamka vizuri ukiwa na nguvu.
Hapa ndipo unapoanza kutengeneza siku yenye ushindi kwenye kila unalokwenda kulifanya.
Jipatie Kitabu USIISHIE NJIANI
Mara zote Zungumza Vitu chanya kuhusu Siku yako.
Ukiamka asubuhi na kuanza kulaumu na kusema hii siku mbaya sana, pamekucha vibaya n.k, lazima uanze kukutana na mabaya ya siku hiyo. Anza kunena mambo chanya tangu unapoamka hata akitokea mtu anataka kukuharibia siku usimruhusu.
Tenga lisaa Limoja la Kufanya mambo ya Muhimu sana Kwenye Maisha yako.
Unapoamka asubuhi hakikisha una muda wa lisaa limoja ambalo utatumia kufanya mambo ambayo ni ya muhimu sana kwenye Maisha yako.
Hapa utafanya mazoezi kwa ajili ya kuwa na afya bora. Hakikisha unatoka jasho kwa zoezi utakalofanya asubuhi.
Omba Mungu, Mshukuru kwa kukupa nafasi tena ya kuiona siku nyingine. Ombea kazi zako zote utakazofanya siku hiyo. Ikabidhi siku yako mikononi mwake.
Pitia maono yako na ndoto zako. Kadiri unavyorudia rudia kitu kwenye akili yako ndio unakipa nafasi ya kukumbukwa. Kama utakua unasoma maono yako kila siku asubuhi baada ya muda Fulani utakuta ndio yamekaa Zaidi kwenye akili yako kuliko chochote. Hii itakusaidia kuweza kuyatekeleza.
Soma kitabu. Kama utaanza siku yako kwa kuweka kitu kipya kwenye akili yako utakuwa na siku bora sana. Jitahidi usome kurasa kadhaa kila siku asubuhi.
Ni mimi Rafiki Yako,
Jacob Mushi
USIISHIE NJIANI
Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.