KONA YA BIASHARA: Mabadiliko Yanakuja Utabaki Salama?

Kwenye chochote kile ambacho unakitegemea katika kukuletea pesa iwe ni biashara au ajira  ni vyema kujiuliza swali hili kwamba, kutokana na mabadiliko yanayokuja kila wakati hasa ya kiteknolojia je nitabaki salama kwa muda gani?

Kama ni biashara basi angalia jinsi unavyoiendesha biashara yako sasa hivi na namna ambavyo mambo yanabadilika je unabadilika au unaendelea kutumia mifumo ya zamani?

Je endapo likatokea badiliko lolote la kuondoa mfumo ninaoutumia nitabakia salama?

Unatakiwa ujue kwamba kila siku kuna binadamu wanawaza namna gani wanaweza kuyafanya maisha yawe marahisi kwa kurahisisha upatikanaji wa vitu na huduma mbalimbali. Mojawapo ya vitu vinavyoangaliwa ni biashara yako pia.

Ni vyema ukajitengenezea tabia au mfumo wa kutotegemea aina moja ya uendeshaji ili usije kuanguka kibiashara. Kwasababu mabadiliko yakija hayakuhurumia kama ulijiandaa au hukujiandaa. Kama utatokea mfumo rahisi wa wateja wako kupata huduma au bidhaa unayoiuza halafu wewe pekee ukawa ndio hauna huo mfumo ujue unaweza kuangushwa kibiashara.

Lazima uangali mbele uone ni mabadiliko gani yanakuja na yanawezaje kuathiri kile unachokifanya. Ukiweza kutazama mbele vizuri unaweza kuwa na maandalizi ili lolote linaweza kutokea likuletee athari chanya kwenye biashara yako.

Ni hatari sana kubaki kwenye mfumo wa zamani huku ukidharau mabadiliko madogo madogo yanayokuja. Ni sawa na wale ambao walibaki na farasi zao wakadharau waliokuwa wanatengeneza magari mwisho wa siku unabaki na farasi wako wengi na hakuna wa kumuuzia maana wote wanataka magari.

Tazama mbele ona mabadiliko, jiandae.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

This entry was posted in KONA YA BIASHARA and tagged on by .

About jacobmushi

Jacob Mushi ni Mwandishi wa makala, nukuu na vitabu vya Maisha na Mafanikio, Kocha wa Maisha na Mjasiriamali. Kiu yake kubwa ni kuona wewe unakuwa mtu bora, unatimiza ndoto zako na unaishi Maisha ya mafanikio. Kazi yake kubwa ni kuhakikisha wewe hauishii Njiani kwenye lile kusudi ambalo Mungu ameweka ndani yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *