Habari za leo Rafiki yangu na msomaji wa mtandao wa USIISHIE NJIANI? Ni matumaini yangu kuwa bado hujaishia njiani kwenye safari yako ya mafanikio. Kila siku kuna hatua unapiga kutokana na yale unayojifunza hapa kila siku.

Leo tunakwenda kuona ni jinsi gani ya kujijengea tabia ya kujisomea vitabu kila siku. Mojawapo ya changamoto kubwa inayowakumba wengi ni namna ya kutenga muda mzuri ambao utaweza kujisomea kitabu angalau kila siku.

Kutokana na mambo mengi tuliyonayo tunajikuta tunajisahau kabisa kuweka ratiba hii ya kujisomea vitabu. Kwa kupitia Makala hii utakwenda kuona namna ambayo utaweza kutengeneza tabia ya kujisomea na mwaka ujao uwe bora Zaidi kwako.

Kusoma vitabu ni lazima kama vile ambavyo unakula chakula kila siku au kuoga. Hii ni kwasababu akili zetu ili ziweze kuzalisha mawazo mapya lazima tuweke vitu vipya ndani yake. Na njia ya kuweka vitu vipya kwenye akili kwa ajili ya mawazo bora ni kwa kujisomea vitabu.

Ili uweze kuanza vizuri tengeneza utaratibu wa kupata angalau dakika 10 hadi 30 za kujiosomea kurasa chache za kitabu kila siku unapoamka na kabla hujalala. Kama unaweza kupata muda wa kutazama Tv, na kusoma magazeti basi hii ya kusoma vitabu unaweza pia.

Soma:  KITABU SIRI 7 ZA KUWA HAI LEO

Chagua kitabu ambacho utataka kukisoma hadi ukimalize na chagua kurasa ambazo unaweza kuanza kusoma kwa dakika zile za asubuhi na kuendelea jioni. Kwa kawaida chagua kurasa chache  angalau kuanzia tano hadi kumi.

Ni vyema ukatambua kwamba kama hujabeba kitabu utakutana na vitu vingine ambavyo vitakuvutia kufuatilia hasa wakati umechoka au umekosa cha kufanya. Unapokuwa na kitabu moja kwa moja unapopata dakika kadhaa unapitia kitabu chako. Ukiwa kwenye foleni unasoma, ukiwa unasubiri jambo mahali unasoma kitabu chako.

Kuna vitabu vilivyopo kwenye mfumo wa sauti ambapo badala ya kusikiliza mziki kwenye gari yako au simu yako utaweka vitabu hivi na kusikiliza muda wowote ambao utawasha gari au kusikiliza kwenye simu. Vitabu hivi kadiri unavyoirudia kusikiliza kila siku ndipo utaona mabadiliko kwenye tabia yako ya kusoma. Utaanza kukutana na mambo ambayo hukuwahi kuyajua kabla.

Unaweza kupata Audio Books hapa…

Ili uweze kujenga tabia hii lazima ujitenge kidogo na mitandao ya kijamii. Mara nyingi imekuwa ni tabia ya wengi kila wanapoamka wanakimbilia simu zao na kuanza kupekua yaliyojiri. Unapoanza kutaka kujenga tabia ya kusoma lazima uzime data kwenye simu yako. Kwenye mitandao hii unaweza kupoteza masaa mengi na kumbe hakuna cha maana ulichokuwa unapata huko.

Unapopanga ratiba ya siku au wiki hakikisha umejiweka muda wa kusoma vitabu. Hii itaonyesha ni kiasi gani ulivyoamua kujitoa kwenye kusoma. Haiwezekani ikawa tabia tu kirahisi kama hujaamua kujitoa kuitengeneza iwe tabia yako.

Wakati mwingine weka na alamu kabisa ya kukuamsha mapema ili uweze kusoma kitabu kabla ya kufanya mambo mengine.

Kwenye Maisha yetu ya kila siku kuna mambo mengi, na kuna wengi wanataka tujishughulishe kwenye mambo yao. Kama utakuwa unakubali kila linalokuja unaweza kuja kukuta hakuna la maana ulilofanya kwenye Maisha yako.

Sema hapana kila wakati ili uweze kupata muda wa kusoma vitabu. Yakatae yale mambo yasiyo na uzalishaji kwenye Maisha yako.

Wale watu ambao wanakuita kwenye starehe sasa waambie hapana ili uweze kupata muda wa kusoma.

Soma: Barua Kwa Vijana ambao Hawajaoa au Kuolewa.

Kusoma vitabu inapokuwa tabia yako utaanza kuona faida kubwa kubwa za kusoma vitabu. Amua sasa inawezekana kabisa na usiishie njiani.

 

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Jiunge na Usiishie Njiani Academy Hapa https://jacobmushi.com/academy/

Huduma Zetu https://jacobmushi.com/huduma/                                               

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading