BARUA MAALUMU KWA VIJANA AMBAO BADO HAWAJAOA AU KUOLEWA.

jacobmushi
10 Min Read

Habari za leo Rafiki, ni matumaini yangu kila mmoja anaendelea vyema kwenye Maisha yake na kupambana ili kupata matokeo bora Zaidi. Nina Imani kabisa unalifahamu kusudi la wewe kuwepo hapa duniani. Hujazaliwa kwa bahati mbaya, kila mwanadamu amekuja na uwezo ambao anatakiwa autumie hapa duniani ili aweze kuishi Maisha bora na yenye mchango kwa wengine

Wewe kama kijana mwenye umri kuanzia miaka ya kujitegemea yaani 18+ na bado hujaoa au kuolewa ni jukumu lako sasa kutambua kusudi lako mapema sana kabla hujafanya maamuzi ya kutaka kuoa au kuolewa. Kulitambua kusudi ulipaswa utambue mapema sana tena kabla hata hujaanza kwenda shuleni. Lakini kwsababu ya mazingira haya tuliyokulia bado unayo nafasi hata sasa. Nina amini pia kwa umri wako umefikia nyakati ambazo unaanza kukaa mbali kidogo na wazazi wako. Inawezekana upo chuoni au upo kwenye shughuli zako binafsi hivyo wazazi wako hawana sauti kubwa kwako kwa kipindi hiki.

Utakuwa unakosea sana kama muda utakuwa unakwenda, unaendelea kusoma Makala katika mtandao huu wakati bado hujalitambua kusudi la wewe kuwa hai hapa duniani. Usikubali kuishi hapa duniani kama Wanyama wengine wa kawaida. Kama ng’ombe aliumbwa na uwezo wa kuzaliana basi wewe kuzaa watoto hapa duniani sio kitu cha kujivunia sana. Nina amini unacho kikubwa Zaidi ya kuzaa, kula, kujenga nyumba na kulelea watoto. Ndege anatengeneza kiota chake, panya anaweza kuchimba shimo ambalo ndio nyumba yake, na wadudu wengine unaowafahamu.

Itakuwa ni aibu sana kama na wewe utakuja hapa duniani na ukaondoka ukiwa umefanya mambo ambayo hata Wanyama wasio na uwezo wa kufikiri wamekushinda. Itakuwa ni aibu sana kama utaondoka hapa duniani bila ya kuacha kitu cha tofauti na Wanyama wengine.

Ni wakati wa kujitafakari mpaka sasa umeanza kufanya kitu gani ili uache alama ndani ya dunia hii.

“Chanzo kikuu cha maovu yanayoendelea kutokea hapa duniani ni watu kutokutambua makusudi ya wao kuwepo hapa duniani.”

Sidhani kama kuna mwanadamu alizaliwa ili aje kuwa jambazi, aje kuuza mwili wake, aje kuwa shoga, aje kuwa mbakaji na vitendo vingine vyote unavyojua havifai. Yoote hayo yanasababishwa na watu kukosa kujua makusudi ya wao kuwepo hapa duniani. Utaendelea kuwaona vijana wadogo wenye umri kama wako wameweza kufanya mambo makubwa kwasababu wamegundua mapema kusudi la wao kuwepo hapa duniani na wakaamua kufanyia kazi hadi wakafikia viwango vya juu.

Vilevile utaendelea kuwaona wasiojua wanachokifanya hapa duniani kazi yao kubwa imekuwa ni kuwa wachangiaji na watoa maoni kwenye mafanikio ya wenzao huku wao hawajui wanapoelekea. Kijana mwenzangu usikubali kuwa mtu wa aina hii. Unapoteza muda, huo muda utumie kufanya kazi kwa bidii ili uondokane na umaskini. Huo muda utumie kujifungia ndani huku ukijinoa ili utoke kwenye lile kusudi ambalo Mungu ameweka ndani yako.

“Hakuna binadamu aliezaliwa aje kuwa mshangiliaji wa mafanikio ya wenzie tu kila mmoja ana cha kwake anachopaswa kushangiliwa nacho pia.”

Ni sawa kabisa kushangilia mafanikio ya wengine na kufurahi pamoja na wanaofurahi. Lakini ni vyema sana ukapenda kujiuliza wewe utakuwa lini? Ni lini na sisi tutajiunga tusherehekee mafanikio yako? hapa sizungumzii kuoa na kuolewa haya ni mambo ya kawaida sana. Nazungumzia tuje kushangilia pale ulipoweza kuliishi kusudi lako hadi viwango vya juu.

SOMA: MAMBO 20 UNAYOPASWA KUYAFAHAMU KIJANA MWENYE UMRI KATI YA 20-30.

Beba Majukumu Yako Yote.

Tambua kwamba unahusika kwa lolote linalotokea kwenye Maisha yako sasa hivi na lolote ambalo halijatokea pia. Kama ulitakiwa ufikie hatua Fulani ya Maisha na hujaifikia unahusika katika kusababisha usifikie hapo. Hapo sasa hivi jaribu kujitazama je kuna mtu huwa unamtupia lawama mambo yako yakiwa mabaya?

Kuna mtu huwa unamfikiria akusaidie kifedha unapokwama kimaisha? Kama yupo na huyo mtu sio wewe basi bado hujabeba majukumu ya Maisha yako yote. Haijalishi wewe ni mwanaume au mwanamke bado unapaswa kubeba majukumu yako mwenyewe. Hasa wasichana hii itakusaidia kuepuka kuja kufanya mambo yasiyofaa ili kutimiza mahitaji yako ya kimwili.

Msichana.

Ni aibu sana kwa msichana ambaye hujaolewa kutoa nguo yako ya ndani kwa mwanaume kwasababu una shida za kipesa. Ni aibu sana kuuza mwili wako kwa mwanaume wa mtu ili tu upate mahitaji yako ya Maisha. Ipo siku utakuja kuwa mke wa mtu, ipo siku utakuja kuwa mama wa watoto embu jiulize utapendelea wanao wajue hayo? Utapendelea wanao wakike waje wafanye kama wewe ulivyofanya?

Ni aibu sana kukaa nyumbani kwenu umri umekwenda, huna unachofanya unasubiria uolewe. Wewe umekuwa mmoja wa watu wa ajabu sana kwenye dunia hii. Wapo wenzako wanaofanya mambo makubwa sana hapa duniani. Badala ya wewe kuomba hadi pesa ya kupaka kucha rangi ondoka hapo ulipo nenda kajitume.

Unawafundisha nini watoto wako? Utakuja kuwaambia nini siku moja? Amka sasa hivi uanze kupambana kwa mikono yako na kile ambacho Mungu ameweka ndani yako. Ninaamini kabisa kama unaweza kuuza mwili wako basi kuna bidhaa nyingi halali unaweza kuziuza. Kama unaweza kujipamba ukapendeza na kumvutia mwanaume basi kuna bidhaa nyingi unaweza kutengeneza na zikawavutia wateja vilevile.

Nina amini kama unaweza kutengeneza sauti nzuri ya kimahaba ya kumtega mwanaume kwenye simu basi unaweza kutengeneza sauti nzuri ya kumvutia mteja anunue bidhaa uliyotengeneza. Ninaamini kama unaweza kuvaa nguo nusu uchi na kutembea mwendo ambao unawafanya wanaume wageuka basi unaweza kuitembeza bidhaa uliyotengeneza na watu wakaipenda vilevile.

Anza sasa chukua hatua acha uvivu, tumia akili kufikiri sio viungo vyako vya uzazi. Dunia inabadilika sana unachokifanya sasa hivi kinarekodiwa miaka mitano ijayo utakuja kuonyeshwa, miaka mitano ijayo watoto wako watakuja kuona ulichokuwa unakifanya.

Wewe kama binti unaejitambua hakikisha unaweza kujihudumia mwenyewe kwa pesa zako. Hapo utaweza kujiepusha na wanaume wanakuja kwa ajili ya kukutumia na kukuacha. Ukishakuwa na shida ya pesa vishawishi vinakuwa vingi sana. Unapokuwa huna cha kufanya yaani huna chochote kinachokuweka busy unajitengenezea mazingira ya kujiingiza katika mambo yasiyofaa. Hakikisha, chakula, mavazi na malazi unaweza kujihudumia mwenyewe.

Kumbuka muda wenu ni mchache sana baada ya muda utakuwa huna hiyo sura uliyonayo sasa hivi. Baada ya muda utakuwa huna hilo umbo unaloringia sasa hivi. Baada ya muda wale waliokuwa wanakusifia wewe ni mrembo watakuwa wameshaanza kutembea na wadogo Zaidi yako. utabaki wewe na Maisha yako sasa amua kuendelea kuchezea muda wako kufanya upumbavu au kuliishi kusudi lako hapa duniani.

Hakikisha umeweza kugundua kile Mungu alichoweka ndani yako na uko bize kukifanya ili kikuletee matokeo.

Kijana wa kiume

Ni aibu sana kutembea na kila mwanamke kwasababu tu ya tamaa zako za kimwili. Uanaume haupimwi kwa idadi ya wanawake uliolala nao. Uanaume wako ni namna gani unaweza kubeba majukumu ya kiuanaume. Usikubali kuwa tegemezi kwa mtu yeyote iwe kifedha au kwa namna yeyote. Ni kweli binadamu tunategemeana lakini sio kwa kumbebesha mwingine majukumu yako. jua linalokupasa kufanya na ulitekeleza kwa wakati. Jua unapokwenda ili upate watu wa kukufuata huko.

Ni aibu sana kumtongoza mwanamke na huku hujielewe wewe ulikuja duniani kufanya nini. Ni aibu san asana kuendelea kujiona wewe ni mwanaume HB kwa kuvaa vizuri badala ya kujua kusudi lako hapa duniani kuliishi na kuwa na maono makubwa. Achana na hayo mambo sasa tafuta kujua kwanini ulikuja hapa duniani.

Haijalishi kwenu ni matajiri au ni maskini bado wewe kama wewe una jukumu la kutengeneza Maisha yako mwenyewe. Zile mali kule kwenu ni za baba yako, ule umaskini kule kwenu ni wa baba yako sio wa kwako. Bado na wewe una nafasi ya kuonyesha kwamba hukuja kutembea hapa duniani. Una nafasi ya kuonyesha hukuja kuzaa tu na kuondoka bali umekuja kuacha alama. Umekuja kulitimiza kusudi la kuzaliwa kwako.

Wewe kama mwanaume una majukumu makubwa sana kwenye Maisha yako, kwanza wewe ni kiongozi wa Maisha yako na familia utakayokuja kuwa nayo. Umebeba Maisha ya wengine ndani yako hivyo ni hatari sana kama utayachezea. Umebeba vizazi vingi ndani yako usikubali kuchezea hovyo hovyo.

Maisha yako ni kile ulichokiishi hapa duniani, mabaya na mazuri yote uliyoyatenda yatakuja kusemwa wakati ukiwa haupo. Usikubali kuishi Maisha ya hasara yaani umeondoka na ukasahaulika kabisa kama Wanyama. Unacho kitu kikubwa sana ndani yako.

Kila mmoja kwa jinsia yake ni jukumu lake kwanza kutambua ni kwanini yeye alizaliwa hapa duniani kabla hata hujaanza kufikiria ni nani utakuwa nae maishani mwako. Kila mmoja ni jukumu lake kuwa na maono makubwa juu ya Maisha yake. Haijalishi ulikosea wapi kikubwa ni kutambua makossa yako na kuyaacha na kuanza kuifuta njia ya kweli.

Ni kusihi sana usome kitabu cha SIRI 7 ZA KUWA HAI LEO ili ujifunze Zaidi ya haya niliyoandika leo kwa ajili yako.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
3 Comments

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading