Habari Rafiki, Ni muda mrefu umepita bila kunisikia kwenye uwanja huu wa Makala. Ninayofuraha kukwambia leo niandaa Makala bora sana kwa ajili yako.

Kinachowafanya watu waendelee kufanikiwa kwenye Maisha yao na kuwa na furaha ni pale wanapoweza kuwa bora kila wakati. Mfano kampuni ya simu ili iweze kuendelea kuuza bidhaa zake ni lazima iwe inatoa matoleo mapya yaliyoboreshwa kila wakati bila hivyo watu watachoka bidhaa na kuhamia kwa washindani wengine. Hivyo pia wewe ili uweze kuendelea kufanikiwa na kukua Zaidi ni lazima uzingatie kuwa mtu bora kila wakati. Lazima uweze kujiboresha ili ufanye mambo yako kwa ufanisi a ifikie mafanikio Zaidi.

Zipo njia Tano nimeandaa unaweza kujifunza leo na zikakusaidia sana kuwa mtu bora.

Jifunze kwenye Kila Kitu.

Ninapokuwambia kujifunza kwenye kila kitu namaanisha kwenye kila kitu kweli kwasababu hata jambo baya sana lina funzo ndani yake. Kuwa mtu ambaye chochote kinachotokea kwenye Maisha yako usikubali kikuache hivi hivi hakikisha kwamba unaondoka na funzo. Hata kama umepatwa na changamoto za kupoteza au kuumizwa usikubali zikuachie maumivu bali tu hakikisha unajifunza na unakuwa bora ili usije kurudia makosa yaleyale.

Unawezaje kujifunza kwenye kila kitu? Jipe utaratibu wa kuandika mambo uliyojifunza kila siku inapoisha. Leo imefika jioni andika mambo Matano tu uliyojifunza siku nzima. Hii itaifanya akili yako iweze kutafuta funzo kwenye kila ulilopitia siku nzima.

Chukua Hatua kwenye yale unayojifunza

Kujifunza kwenye kila kitu pekee haitoshi lazima uwe mtu wa kufanyia kazi yale ambayo umejifunza. Kama ulipoteza fedha kwa ajili ya uzembe ukapata funzo la kuwa makini na kufanya mambo kwa kufikiria basi tutarajie kuwa utafanya hivyo kwenye siku zako za mbele. Hatutatarajia tena kuona umerudia kwenye kosa au uzembe ule ule.

Chukua hatua kwenye yale ambayo umeona kabisa haya nikifanyia kazi nitakuwa mtu bora Zaidi. Umejifunza kuweka akiba anza kuweka akiba kwenye kila kidogo unachopata. Chochote kinachotokea kwenye Maisha yako kiwe kibaya au kizuri lazima kina funzo ndani yake basi usikubali yale ambayo yanakufundisha yakaishia hivi hivi yatumie ili uwe bora Zaidi. Kwenye Makala hii tayari umeshajifunza usiyaache tu anza kufanyia kazi kwenye Maisha yako kila siku.

Kubali kukosolewa

Kama kweli unataka kuwa mtu bora Zaidi kila wakati lazima pia uwe mtu ambaye upo tayari kukosolewa. Hii itakusadia sana kuwa bora Zaidi kwasababu hakuna aliekamili, kama  kampuni itapuuza kukosolewa pale wanapotengeneza bidhaaau huduma mbaya basi itapoteza wateja wengi sana, hivyo pia na wewe kama hutokubali kukosolewa utapoteza nafasi ya kuwa mtu bora Zaidi kila siku.

Ni kweli unaweza kuona hii inakuwa ngumu kwako lakini itakusaidia sana kujiboresha kwasababu kuna nafasi kubwa sana kwenye wale wanaotuona kuliko tunavyojiona. Sio kila anaekukosoa anakuonea wivu na hata kama anakuonea wivu basi itumie hiyo nafasi kuendelea kuwa bora Zaidi.

Ni kweli sio vyema kuchukua kila ushauri unaopewa lakini lazima ukubali kwamba kuna watu wanaojua kuliko wewe, kuna watu walishapita unapopita sasa hivi na wanaweza kuwa na mchango mkubwa sana kwenye safari yako ya mafanikio na kuwa mtu bora Zaidi.

Kubali kukosolewa na usichague nani wa kukukosoa na usichagua namna gani ya kukosolewa, lolote linalokuja litumie kama funzo kama tuliyoona kwenye pointi ya kwanza ya kujifunza kwenye kila kitu.

Nenda Hatua ya Ziada

Kama unataka kuwa mtu bora kila wakati, kwenye kufanya mambo yako lazima ukubali kufanya kwa hatua ya ziada. Lazima uwe mtu unaefanya yale ambayo hujawahi kufanya usikubali kuendelea kufanya vitu vile vile kila siku.

Hii itakufanya kugundua vitu vipya na kujua nguvu na uwezo uliopo ndani yako. Hata kama kazi yako inakulazimisha kufanya vitu vile vile kila siku lazima ukubali kuwa unafanya vitu nje ya kazi yako ili kuweza kufanya kwa hatua ya ziada.

Jipe jukumu la kujaribu vitu vipya mara kwa mara hata kama una hofu na woga kwasababu hii itakuongezea ujasiri hasa pale unapopata matokeo bora. Watu wote waliovunja rekodi duniani ni wale waliochukua hatua ya kwenda hatua ya ziada kufanya mambo ambayo watu wanaona hayawezekani.

Ukitaka kuvunja rekodi amua kuwa mtu anaefanya yale ambayo wengine wanaona haiwezekani.

Jipongeze Unaposhinda

Unachukua hatua na ukapata matokea chanya ni vyema kujipa pongezi hata kama ni kidogo. Umeweka lengo la kuinua mtaji kwenye biashara yako kutoka kiwango Fulani hadi kiwango Fulani na ukafanikiwa basi ni vyema sana ukajipongeza. Hii itakupa hamasa ya kufanya tena na ten ana kuendelea kuwa mtu bora kwenye yale unayoyafanya kila wakati.

Umeweka malengo yako ya mwaka, weka pia na kitu cha kujipongeza pale unapoyatimiza kwa asilimia Fulani. Sio lazima ujipongeze kwa kufanya mambo makubwa unaweza kujipa pongeza kwa zawadi ndogo ndogo tu ambazo zinakupa hamasa Zaidi.

Mfano umeweka lengo la kutengeneza faida kwenye biashara yako kutoka milioni moja hadi milioni kumi kwa mwezi. Unapofikia lengo hili basi angalia kwenye Maisha yako ujinunulie zawadi gani nzuri ambayo ukiitazama utakumbuka ulitimiza lengo Fulani.

Nami nikupongeze kwa kusoma Makala hii hadi mwisho.

Nakutakia Mafanikio katika safari ya kuwa mtu Bora kila siku.

Note: Makala Hii Haijaandikwa na ChatGPT.

Unaweza kupata vitabu vyangu hapa https://jacobmushi.com/shop/

Rafiki Yako.

Jacob Mushi

2 Responses

  1. ahsante sana mr jacob. nimefurahi mno kwa mafundisho yako .ila nikuombe kitu kimoja: naomba unisaidie mimi nimejaribu mara nyingi kupanga malengo na kuzingatia ila kila wakati ninajikuta nimesahawu . k.m ninahitaji sana namna yakujipia decision nakuyitimiza!

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading