Unaweza kuwadanganya wengine lakini huwezi kujidanganya wewe mwenyewe. Ndani ya nafsi yako unajua ukweli ni upi. Ndani ya nafsi yako unajua kama Maisha unaigiza au ni kweli kile ambacho unakionesha.
Mojawapo ya vitu vinavyowatesa wengi ni kujaribu kujidanganya wenyewe, unakuta unajua kabisa Matendo yako hayaashirii kabisa kile ambacho unataka lakini unajitia moyo wa uongo kwamba upo siku utafanikiwa.
Unasema utafanya jambo Fulani lakini Matendo yako ni tofauti kabisa na Maneno yako. Unasema utafanya mazoezi lakini ukifika wakati wa mazoezi unaleta sababu nyingine Nyingi zisizo za msingi. Unasema utasoma kitabu lakini kila wakati unajikuta husomi.
Anza kujitazama hivi ni kweli unazo bidii ambazo watu wanakusifia au huwa unajidanganya? Ni kweli wanapokuita wewe ni mpambanaji ukijiangalia kweli Matendo yako yanaridhisha kuitwa mpambanaji? Mbona kama ni uongo hivi? Mbona kama wanasema tu ili kukutia moyo?
Wewe mwenyewe moyo wako unakubali zile juhudi unazoweka? Kama wewe moyoni hujaona kama umefanya vizuri wengine nje wakikusifia basi inakuwa haina maana sana. Wewe mwenyewe ndio una majibu ya ukweli hasa kwenye sifa ambazo wanakupa wengine.
Kuwa mkweli kwako Rafiki usikubali Matendo yako yadanganye. Ukisema unasoma kitabu soma, ukisema unafanya mazoezi nenda kafanye mazoezi. Fanya kile ambacho unasema utafanya, Usiishie kusema tu chukua hatua.
Kila mtu anataka na anatamani kuwa mtu Fulani lakini ni wachache sana wanafanya ili wewe yule mtu ambaye wanatamani kuwa. Usikubali kuishia kutamani na kutaka, ingia katika hawa wachache ambao wanachukua hatua za ukweli kila siku ili kuzifanya Ndoto zako ziwe kweli.
Usije kuishia kua mtu wa Maneno badala ya mtu ambaye wengine watakuja kutamani kufika pale ambapo umefika. Usikubali kujidanganya, usikubali kuridhika na juhudi kidogo ambazo umeweka. Nenda hatua ya ziada, tumia uwezo Mkubwa ndani yako.
Mafanikio yanawakuta wale wachache ambao wanamua kujitenga na wengi ambao ni waoga lakini wana maneno mengi sana. Achana na watu wenye Maneno kaa na watu ambao wanachukua hatua. Una nguvu una uwezo, una kila sababu ya kufanikiwa.
Ubarikiwe sana,
Rafiki Yako, Jacob Mushi
Mafanikio sio lelema, sio bahati ambayo kama ipo utakutana nayo Njiani.