Jiunge na Mtandao Huu Uwe Unapokea makala nzuri kama hii moja kwa moja kwenye email yako
Weka email Yako hapa
Habari Rafiki, natumaini unaendelea vyema na kupambana ili Ndoto yako itimie. Usikubali kabisa kuishia njiani, wako wengi wanakutazama na watakuja kunufaika sana na hicho unachokifanya. Leo tunajifunza mambo sita ambayo yamekuwa yanaiba furaha yako bila ya wewe kujua. Tumekuwa tunafanya mambo mengi na wakati mwingine hatujafahamu ni nini hasa kinatufanya tusiwe na furaha.
Pata Kitabu: USIISHIE NJIANI, TIMIZA NDOTO YAKO HAPA.. www.jacobmushi.com/vitabu
Furaha inaletwa na vitu vidogo vidogo sana, lakini watu wengi huchanganya hili, hufikiri labda pesa nyingi ndio chanzo cha furaha. Au kwa kuwatazama watu kwa nje Maisha wanayoishi hufikiri ndio wana furaha ya kweli. Kuna tofauti kubwa sana kati ya mtu anaeishi Maisha ya anasa au Maisha yenye matumizi makubwa ya pesa na mtu anaeishi Maisha ya furaha.
Unaweza kuwa na pesa nyingi sana, na jambo lolote lile linalohitaji pesa lisiwe tatizo kwako lakini bado usiwe mtu mwenye furaha. Unaweza usiwe na vitu vingi sana lakini bado ukaishi Maisha yenye furaha na Amani sana hapa duniani. Sijasema wenye pesa hawana furaha, wako matajiri wanaoshi Maisha yao vizuri sana. Wapo maskini ambao wanaishi kwa wasiwasi na mashaka. Hivyo usichanganye mambo hapo.
Unatakiwa kutambua furaha inajitegemea yenyewe. Kuwa na furaha hakutegemei wewe una nini au huna nini. Unaweza kuamua kuwa na furaha vile ulivyo sasa hivi. Kwanza tambua kwamba furaha ndio chanzo cha mambo makubwa kwenye Maisha yako.
Tuyaangalie Mambo Yanayoiba Furaha Zetu.
Kuchukia Wengine.
Unapokuwa mtu uliyejenga chuki ya aina yeyote ndani ya moyo wako moja kwa moja huwezi kuwa mwenye furaha. Chuki ni mzigo mzito sana ambao unafanya wengi waishi Maisha ya mateso. Namshukuru sana Mungu ameniwezesha siwezi kabisa kumweka mtu moyoni mwangu. Ukishindwa kuwaondoa watu ndani ya moyo wako yaani kuwasamehe hutakaa uweze kuishi Maisha ya furaha.
Vinyongo/Visasi
Kamwe usiweke kinyongo au kisasi kwenye moyo wako. Huwezi kufanya jambo likaleta maendeleo katika Maisha yako kama hutaweza kuondoa visasi na vinyongo. Samehe wengine ili uweze kuishi Maisha ya furaha. Usikubali kabisa kubeba vinyongo na visasi.
Kutarajia Makubwa Kutoka Kwa Wengine.
Unapokuwa unatarajia mambo kutoka kwa wengine utajikuta unapata chini ya matarajio yako na hilo linaweza kuwa sababu ya kuondoa furaha yako. Usiweke matarajio kwa watu. Kwako pekee ndio unaweza kutarajia mambo makubwa. Haijalishi ni nani yako awe mpenzi wako, au watu wa karibu kiasi gani tarajia madogo yakija makubwa utakuwa na furaha Zaidi. Ukitarajia makubwa yakaja madogo utajisikia vibaya.
Maisha ya Kuigiza.
Usiishi Maisha ambayo sio yako. Ukisema unataka kuwa kama Fulani anza kujitengeneza uweze kufika hivyo viwango kwanza. Usiigize Maisha ya kitajiri wakati huna utajiri. Usiazime magari ili kuwaonyesha watu na wewe una uwezo. Ukweli hao unaowaonyesha wala hawajali chochote kuhusu wewe.
Jitendee haki kabisa kwa kuishi Maisha yako. Unapokuwa peke yako ndio una majibu halisi ya yale Maisha ambayo watu wanafikiri wewe unayo.
Kutaka Kumridhisha Kila Mtu.
Huwezi kumridhisha kila mtu na hata ukisema ufanye chochote ili watu wafurahi au wakuone wewe ukoje utajikuta unaumia. Furaha yako ni ya muhimu sana. Kuwa mwema kwa wengine lakini usiwe mtu unaetaka kufanya mambo ili wengine waridhike huku wewe unaumia ndani ya moyo wako. Chochote unachokifanya kuna watu hawatakaa wakuelewe. Elewa hivyo na usonge mbele kufanya yale yaliyo sahihi.
Kujilinganisha na Wengine.
Ulishawahi kukutana na mtu ambaye mmesoma pamoja na ukaona yeye ameshapiga Hatua sana kwenye Maisha kuliko wewe? Huwa unajisikiaje? Wengi huumia na kuanza kuwaza sana. Ukweli ni kwamba hilo linatakiwa liwe changamoto kwako tu na sio sababu ya wewe kupoteza furaha. Unapowatazama wenzako wanavaa vizuri sana kuliko wewe au wana aina ya Maisha Fulani mazuri kuliko wewe unaweza jikuta unakosa raha na kusononeka. Usipoteze furaha, elewa hayo ni Maisha yao walipambana wakafika hapo walipo. Ni jukumu lako na wewe kupambana na sio kukosa furaha. Hatuwezi kufanana, tengeneza utofauti.
Mitandao Ya Kijamii.
Mitandao ya kijamii imekuwa ni sehemu ambayo inakutanisha watu wa aina mbalimbali na wengi hupenda kuonyesha Maisha yao. Watu wengi huumia sana na kupoteza furaha kwasababu huishia kutazama picha zinazoonyesha aina ya Maisha ya watu wanayoishi. Usipokuwa makini utajikuta unaishi Maisha ya kitumwa kwasababu unapoteza muda wako kufuatilia Maisha ya wengine badala ya kutengeneza furaha yako.
Ubarikiwe sana,
Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi
Nzuri sana hii makala
Ujumbe huu umekuja kwa mda muafaka kwa upande wangu! Ubarikiwe br
Karibu sana Rafiki
Daah! Katika ujumbe ulionigusa huu ni nambari moja.Kazi nzuri Mungu aendelee kukutunza kwa ajili yetu kijana wa Yesu.Ubarikiwe
Amina