Habari za Leo. Ni furaha yangu kuwepo pamoja na ninyi hapa siku ya leo.

Kabla hata hujaweka malengo yako ya mwaka huu jiulize maswali haya ya muhimu. Umeshajua kwanini Upo duniani? Una Maono gani juu ya hilo lililokuleta hapa duniani?

Ukishapata majibu ya maswali hayo mawili tunaweza kuendelea kujifunza kwenye somo letu la kuweka malengo.

Malengo ni mgawanyo wa vipande vipande hadi kuifikia ndoto au maono yako ndio maana swali likauliza una maono gani? Ndoto yako ni ipi? Kwasababu malengo yetu tunayopanga kila mwaka lazima yawe yanalenga Zaidi katika maono yetu na ndoto zetu kutimia.

Kuna malengo ya muda mfupi na muda mrefu. Muda mfupi ni kuanzia mwaka mmoja kurudi nyuma hadi siku moja. Muda mrefu inaweza kuanzia miaka 3 hadi miaka 20. Ni wewe mwenyewe utakavyoamua kugawanya malengo kutokana na ndoto na maono uliyonayo.Malengo lazima uyagawanye katika sehemu kuu tano.

Mahusiano

Kitu cha kwanza unatakiwa uweke malengo kwenye upande wako wa mahusiano. Mwaka huu unataka kuwa na mahusiano gani na marafiki zako, ndugu zako, na wote wale unaowapenda. Unatamani uwafanyie nini? Unatamani wao wafikie hatua gani katika Maisha yao? Tupo hapa duniani ili kufurahi na watu waliotuzunguka hivyo ni muhimu sana kujenga mahusiano bora na wengine. Kwenye mahusiano wengi hufikiria Zaidi Kuhusu uchumba na ndoa lakini uchumba na ndoa unaingia katika watu unaowapenda na kuwajali. Hivyo weka malengo yako juu ya watu wote hao ni mahusiano ya aina gani unataka kua nayo kati yako na wao. Ni watu gani wa kuondoa kwenye Maisha yako mwaka huu? Sio kila aliekuwa rafiki yako mwaka 2016 anafaa kwenda nae tena mwaka huu angalia ni mchango gani ameleta kwenye Maisha yako kama alikua anakurudisha nyuma basi ni wa kukimbiwa huyo.

Afya

Sehemu ya pili ni Afya.

Afya imegawanyika katika makundi matatu. Afya ya Kiroho, Mwili na Akili.

Afya ya mwili.

Mwaka huu  unataka uwe na afya ya namna gani? Inawezekana labda ni mnene kupindukia unatamani upunguze uzito weka malengo mapema. Na hakikisha umejua kabisa kwa mwaka huu unataka upunguze kilo ngapi. Labda una ulaji mbovu wa chakula unaoharibu afya yako. Ni wakati wako sasa wa kuandaa mfumo mzuri wa kula ili ufikie malengo ya afya bora katika maisha yako. Mafanikio yeyote unayoyataka kama huna afya bora utateseka. Wakati mwingine mpenzi wako anaweza kuwa hafurahii muundo wa mwili wako kutokana na kuzidi mafuta sana. Jitengenezee malengo ya kufikia aina ya mwili ambao unautaka. Weka malengo ya kufanya mazoezi kila siku na utaona matokeo bora. Jua ni vyakula gani hutakiwi kula kwa wingi na vipi ni vya muhimu kwa afya yako.

Afya ya Roho.

Mwaka huu unataka uwe na mahusiano gani na Mungu? Unataka ufikie kiwango gani cha kuwa karibu na Mungu wako? Unatamani uilishe roho yako neno la Mungu kwa kiwango gani? Roho yako imjue Mungu kwa Kiasi gani? Yapo mengi sana jitahidi kuongezea kadiri ya ulivyo kihiduma katika kanisa unaloabudu.

Afya ya Akili

Mwaka huu unataka uwe na maarifa ya aina gani? Kulingana na maono yako kuna vitabu unatakiwa usome ili kukuza ufahamu wako. Yapo mengi sana ya muhimu ya kuweka kwenye akili ili uweze kuwa na Maisha yenye maana. Vitabu vingapi unataka usome mwaka huu? Hakikisha umevijua na majina kisha uanze kuvitafuta.

Kazi na Biashara

Sehemu ya tatu ni kazi na biashara. Hapa inategemea unachokifanya ni kitu gani kama umeajiriwa basi weka malengo kwamba unataka ufikie viwango gani katika upande wa ajira yako. Kama ni biashara hakikisha unajua unataka ufikie mtaji wa shilingi ngapi. Wateja wangapi? Na umepanua wigo wako wa kujulikana kiasi gani? Kama ni kipaji lazima ujue unakitumiaje kipaji chako kutengeneza kipato na mwaka huu unakwenda kufanya nini ili ufikie watu kadhaa.

Hapa pia tunalenga kwenye kusudi la wewe kuwepo duniani kwani hii ndio kazi yako haswa nay a muhimu sana kuliko nyingine. Hii ndio inaweza kukupatia utajiri wa aina zote unaoutaka ukiweza kuishi vyema katika kusudi lako. Jiulize je unataka mwaka huu upige hatua gani katika kuifikia ile picha uliyokuwa unaiona. Inawezekana wewe unatamani kuja kuwa mwanamke Mjasiriamali mkubwa sana. Je picha hiyo unaifikiaje? Mwaka huu unataka uifikie kwa hatua ipi?

Fedha

Sehemu ya nne ni fedha. Unataka mwaka huu utengeneze kipato cha shilingi ngapi? Weka malengo ya kifedha na ujue unaipaje hiyo pesa kutokana na kile unachokifanya. Unaweka akiba ya kiasi gani mwaka huu? Unataka kuwekeza pesa kiasi gani mwaka huu? Hapa kwenye pesa yapo mengi sana.

Jamii

Sehemu ya tano ni jamii. Unataka jamii ipate mchango wa aina gani kutokana na kile unachokifanya? Mwaka huu unatamani kuwasaidia watu wangapi wasiojiweza? Andika idadi ya watu unaotamani kuwagusa Maisha yao kutokana na kile uanchokifanya.

Baada ya hayo yote lazima uweke mpango mkakati wa kutimiza malengo yako maana hayakwendi kujitimiza yenyewe. Kuna vitu vya kufanya kila siku ili uweze kusogelea malengo yako yam waka huu. Hakikisha umejua ili uwe na afya bora ya kiakili, kimwili na kiroho ni vitu gani wapaswa kufanya kila siku. Ili uwe na mahusiano bora na wengine ni vitu gani hasa unapaswa kuanza kufanya kila siku.

Biashara au kazi yako ili ikue na ufikie malengo ni vitu gani haswa vya kuanza kufanya. Ili ufikie malengo ya kifedha ni yapi ya muhimu kufanya ni mauzo kiasi gani unapaswa kuzidisha?

Yote hayo yanawezekana kwa vitendo vyako vya kila siku. Kila jambo unalotamani litokee mwaka huu litakuja kutokana na matendo yako.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

4 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading