Kwa kijana ambaye umefanikiwa kuwepo kwenye karne hii ya 21 ukisema kwamba huna njia ya kufanikiwa utakuwa unajiaibisha.

Mabadiliko makubwa sana ya kiteknolojia yaliyopo sasa hivi na yatakayoendelea kuwepo yanarahisisha sana mtu aweze kufikia mafanikio makubwa kwa kutumia vifaa vya kisasa na mitandao ya kijamii.

Kama kijana unapaswa kujua ni namna gani unaweza kuitumia mitandao hii ya kijamii badala ya mitandao hii kukutumia wewe. Badala ya kuitumia kuangalia vitu vinavyoendelea kutokea sehemu mbalimbali duniani unaweza kuitumia mitandao hii kutengeneza jukwaa lako ambalo utalitumia kukuza kile ambacho kipo ndani yako.

Vitu Vya Msingi Kuvifahamu Kwanza.

Fahamu Unachokitaka.

Hakuna mafanikio yeyote yaliyotokea bila mtu kutambua anachokitaka. Yeyote unayemuona anafanya kazi kwa bidii kuna jambo ambalo analifanyia kazi kwa bidii kuna kitu anataka kubadilisha kwenye Maisha yake. La sivyo angekaa nyumbani apumzike.

Hivyo basi ni muhimu wewe kama kijana kujua ni nini unataka kwenye Maisha haya. Bila kujua unataka nini unaweza kujikuta umezungukwa na fursa za kila namna lakini usiweze kuzitumia. Kama upo vitani unapambana na maadui lazima utakuwa unawaza namna ya kupambana. Ukiona kitu chochote ambacho unaweza kukitumia kama silaha basi unakitumia.

Ni muhimu ujiulize unataka nini? Na upate majibu yake.

Umezungukwa na nini?

Ndio, umezungukwa na vitu gani ambavyo ukivitumia vinaweza kukupa nafasi ya kufikia unachokitaka. Moja wapo ya vitu vilivyokuzunguka ndio inaweza kuwa kifaa cha kiteknolojia, kama simu janja au kompyuta. Vifaa hivi au vitu vingine ambavyo vimekuzunguka ndio vinakuwa ni nyenzo muhimu kwako kuweza kufikia kile unachokitaka.

Inawezekana una simu janja nzuri sana na ya bei ghali unaitumia kufuatilia vitu visivyo kusaidia chochote kwenye mitandao na bado unalalamika Maisha magumu na huna cha kufanya. Endapo utafahamu unachokitaka na umezungukwa na nini ikiwemo hiyo simu basi utaweza kuacha kulalamika na kupata kitu cha kufanya.

Unatumiaji Teknolojia/Intaneti?

Kama unajua kusoma na kuandika pekee unaweza kutumia Mtandao wa internet au teknolojia yeyote kwa kuamua tu kujifunza. Hadi umeweza kukifikia kitabu hiki na kukisoma ina maana kwamba una uwezo Mkubwa wa kufikia mafanikio yako.

Kwa kupitia Mtandao wa internet unaweza kuwafikia mamilioni ya watumiaje wake na ukawaonesha kile unachokifanya kama ni bidhaa zako au kipaji ulichonacho na watumiaji hao wakakulipa wewe fedha na Maisha yako yakabadilika.

Kinachohitajika ni wewe kutambua una nini ndani yako, vitu gani vimekuzunguka na unavitumiaje kuweza kufanyia kazi kile kilichopo ndani yako. Badala ya kulalamika kwa kusema huna hiki wala kile tumia kila fursa iliyopo mbele yako ili uweze kufanikiwa. Fursa kubwa iliyopo mbele yako sasa ni mitandao ya kijamii na teknolojia mpya zinazokuja kila siku.

Teknolojia inarahisisha mambo mengi sana ikiwemo upatikanaji wa maarifa. Kama utaweza kumia vizuri simu yako unayoitumia kwa intaneti basi unaweza kujifunza mambo mengi sana ambayo yatakupa nafasi ya kusonga mbele. Inawezekana hapo ulipo kuna malighafi ambazo ungeweza kuzitumia kutengeneza bidhaa na ukaziuza lakini hujui namna ya kutengeneza kwa kutumia teknolojia unaweza kuangalia wengine wanatengeneza vipi na wewe ukapata ujuzi.

Umetengeneza bidhaa zako na unafikiri hujui pa kuzipeleka ingia kwenye mitandao ya kijamii onyesha zile bidhaa zako Wateja watajitokeza kwako na utaweza kuuza bidhaa zako.

Chagua Vitu Vichache Ambavyo Ungependa Vikutambulishe kwenye mitandao ya kijamii na uvifanyie kazi kila siku hadi vianze kukuletea matokeo. Mimi niliamua kutumia kipawa cha uandishi kwa njia Mtandao wa intaneti na hadi sasa umeweza kunisoma kwenye kitabu hiki.

Unaweza kuchagua kile ambacho kipo ndani yako, labda unataka kutengeneza bidhaa Fulani uiuze basi hakikisha unaifahamu vizuri sana na unaifanya kwa ubora huku ukilikuza jina lako. Kwa kupitia bidhaa ile miaka michache utakuwa ni mtu ambaye umewafikia watu wengi sana.

Miliki Tovuti Yako Ikiwezekana, mimi namiliki tovuti yangu ya mafunzo iitwayo www.jacobmushi.com hii imebeba kazi zangu Nyingi sana za miaka kadhaa ya nyuma tangu nilipoanza kuandika. Wewe kwa kile ambacho unataka kufanya unaweza kumiliki tovuti ambayo itakutambulisha na watu wataitembelea kuona kazi zako. Kumiliki tovuti ni gharama nafuu sana kwa mahali tulipo sasa na unaweza kujifunza kuendesha kwasababu si kazi ngumu sana hasa kama unajua kusoma na kuandika.

Fanya Kila Siku, kile unachokiweka kwenye Mtandao hakikisha ni bora sana na ukifanye kila siku, usitegemee matokeo ya haraka. Chochote kikubwa kinaanza taratibu na kuwekewa msingi imara, msingi imara ni uaminifu kati yako na wale ambao unawahudumia. Hakikisha unatengeneza uaminifu kwasababu watu wakishakuamini na wakaona ubora wa kile unachokifanya watakuwa Wateja wako wa kudumu.

Kama kijana utaweza kutumia Teknolojia vizuri basi unaweza kufikia Ndoto yako na kile kilichopo ndani yako. Usiendelee kukaa chini na kulalamika wakati kila siku zinakuja njia mpya za kukurahisishia wewe kufanikiwa.

Usiishie Njiani Chukua Hatua sasa na Utimize Maono Yako.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading