Category Archives: MBINU ZA MAFANIKIO

512; Mimi Ni Mtenda Dhambi Kuliko Wewe.

Siku Moja nilikuwa nawaza hivi, “Siku Nikifa Nikakuta hakuna Mungu Nitacheka Sana”, Sauti nyingine ndani yako Ikasema, “Hapo Utakapokuwa Unachekea ni Nani Huyo Atakuwa Amekutengenezea” Ndugu Yangu Mungu Yupo, Ukatae Ukubali…………………

Kuna ule mtazamo wa kuwaona watu ambao wamefanya mambo makubwa, na wale wenye ushawishi mkubwa sana kuwa hao ni watu wasio na makossa kabisa. Na hiyo hupelekea pale wanapokosea kitu cha kawaida kabisa mfano ndoa kuvunjika, tunawaona kama vile ni wamefanya makossa makubwa sana.

Wakati huo huo kuna watu wengi sana kila mara ndoa zao zimekuwa na matatizo makubwa na wanaishia kuachana bila hata kujulikana.

Rafiki napenda ufahamu kwamba kila mmoja ana jambo ambalo huwa ni udhaifu wake. Kila mmoja kuna kitu ambacho kimekuwa kinamshinda mara kwa mara hata wewe ukijitafakari utaona kunai le dhambi ambayo kila mara hukuangusha. Hata kama hakuna anaeijua basi wewe mwenyewe na Mungu wako ndio mnaijua vizuri.

Kama kwako kuna kitu kama hicho basi ina maana kwamba kila mtu kuna jambo ambalo limekuwa likimsumbua pia. Kila mmoja kuna ka udhaifu Fulani huwa kinamwangusha. Ndio maana katika wanafunzi 12 wa Yesu bado kulikuwa na mmoja Yuda Iskariote aliemsaliti Yesu kwa tamaa ya fedha. Bado pia kuna Petro ambaye alimkana Yesu mara tatu, kuna mwingine huyu anaitwa Thomaso alishindwa kabisa kuamini kama Yesu amefufuka mpaka amshike kwa mikono yake.

Sasa kama Yesu mwenyewe alijua amechagua watu 12 wazuri na bado wakaonekana wenye madhaifu mimi ni nani niseme sina dhambi hata kidogo? Ndio maana nataka kukwambia mimi ni mtenda dhambi kuliko wewe, Neema ya Mungu tu ndio hunisaidia, napenda ulijue hili ili usije kunihukumu siku moja ukisikia makosa niliyoyatenda. Vilevile hata wewe kuna kitu najua ni udhaifu wako, unakusumbua mara kwa mara, umekuwa unajaribu kuacha lakini unakwama.

Nataka uwe na mtazamo chanya kwenye mambo ya wengine uweze kuchukuliana na kila mtu kwasababu kila mmoja ana jambo ambalo linamsumbua sana ndani yake hata kama hatakwambia. Na haya mambo ndio mara zote huwaga ni siri za ndani ya watu.

Unaweza kuwa unasema sasa Jacob unataka kusema kila mmoja awe huru kufanya dhambi ile ambayo inamshinda? Hapana hapo utakuwa umenielewa vibaya, maana yangu hapa ni kuwa wewe utambue mtu akiwa hai na akakosea kwa chochote kile bado ana nafasi ya kutubu mbele za Mungu wake.

Inawezekana Mtu ametenda uovu ukasambaa sana akatubu kwa Mungu akapata msamaha na wewe ukaendelea kumhukumu, kumsema vibaya, kumuandika vibaya, ikatokea umekufa ukaenda kuhukumiwa kwa kutenda dhambi ya kuhukumu wengine. Maana yangu hapa kama wewe huna nafasi ya kwenda kumshauri au kumsaidia mtu aliekosea usipoteze muda wako kumsema na kumzungumzia kwasababu huenda unasema yule ni mtenda dhambi sana, kumbe alishatubu siku nyingi na kusamehewa.

Hakuna haja ya kuzungumza mabaya ya mtu kama huwezi kuzungumza mazuri yake. Hakuna haja ya kumchukia mtu alietenda maovu bali twapaswa kumuombea Mungu amsaidie. Na wewe binafsi ukishaujua udhaifu wako basi ni jukumu lako, kuhakikisha unakaa mbali na vile vitu ambavyo vinakupelekea kuitenda dhambi. Ukishatambua kile ambacho kinakuangusha kirahisi ni jukumu lako kutafuta msaada kwa watu wenye uwezo kwenye tatizo lako wakusaidie uweze kujidhibiti.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

489; Hizi Ndio Fikra Zinazokufanya Usiendelee Kwenye Maisha.

Ndani ya jiji lenye watu wengi kuliko miji mingine ndani ya Tanzania jiji la Dar es Salaam, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya Usafiri. Hivyo basi serikali pamoja na watu binafsi wamekuwa wakiwaza kila siku ni njia gani inaweza kuwa suluhisho la tatizo hili.

Katika kufikiri huko kukatokea watu wawili ambao walikerwa sana tatizo hili la usafiri wa kugombania hasa kwenye daladala. Watu hawa walikuwa hawafahamiani lakini kwa wakati mmoja walipitia matatizo yanayofanana. Kwa wakati mmoja wakawaza kujiondoa kwenye tatizo hili la usafiri.

Kila mmoja alifikiri kwa namna yake, mmoja aliamua kuchukua mkopo akanunua gari ndogo ambayo itamsaidia kufika kwenye shughuli zake kwa urahisi na haraka zaidi, na yule mwingine akaamua kununua daladala yake mwenyewe ili aweze kupunguza adha ya usafiri kwake na kwa watu wengine Zaidi.

Watu wote hawa wana mawazo mazuri ya sana ya mabadiliko na kupanda viwango. Utofauti walionao ni katika fikra tu. Mmoja alijifikiria yeye mwenyewe na akaamua kujitatulia tatizo peke yake, na mwingine aliwaza mbali kabisa akaona hili sio tatizo tu bali ni fursa. Kama watu ni wengi kuliko daladala maana yake nikiongeza daladala zangu hapa nitawasaidia watu na pia nitatengeneza pesa.

Watu wengi tuna fikra kama za huyu jamaa alienunua gari yake binafsi ya kutembelea ili awahi haraka kwenye shughuli zake. Ni wazo zuri sana, ni maendeleo mazuri sana lakini haya ni ya kibinafsi na pia hayatakusaidia sana kama huyu aliewaza kwenda kununua daladala zake.

Kuna matatizo mengi yapo kwenye jamii na watu wanawaza kuyatatua lakini changamoto ipo kwenye aina za suluhisho tunazotaka kuleta kwenye matatizo yetu. Mara nyingi mawazo yanayotujia huwa ni ya kibinafsi Zaidi na ndio maana tunakuwa wengi tuna Maisha ya wastani na hatuendelei na kufikia utajiri mkubwa.

Ukiwa na fikra za kujifikiria wewe mwenyewe tu katika kutatua matatizo sio rahisi kuona picha kubwa kwenye matatizo unayopitia. Lazima ubadilishe mtazamo wako uanze kuwaza namna gani utawasaidia na wengine wanaopitia kwenye tatizo kama lako na sio utafute njia rahisi ya wewe binafsi kuepuka tatizo.

Mfano mwingine tuna wanafunzi wengi waliomaliza vyuo wako mitaani hawana ajira na katikati ya wanafunzi hao kuna watu wenye fikra za kibinafsi na wenye fikra pana Zaidi katika kutatua matatizo ya wengine. Wenye fikra za kibinafsi wanaweza kukimbilia kujiajiri tu mahali ambapo watapata pesa za kuendeshea Maisha yao. Wenye fikra pana za kutatua tatizo sio kwa binafsi tu bali hata kwa wengine wenye tatizo linalofanana watawaza kuleta makampuni ambayo yatapunguza tatizo la ajira. Watawaza kuja na aina mbalimbali za suluhisho ambazo zinatawasaidiwa wengi na wao watafaidika pia.

Rafiki yangu nataka uache fikra za kibinafsi katika matatizo unayopitia.

Anza kuwafikiria wengine kama wewe mnaopitia tatizo linalofanana na uone ni namna gani unaweza kuwasaidia ili na wewe ujisaidie. Ukiishia kufikiria wewe tu kwenye kila tatizo unalopitia mwisho wa siku utaishia kuwa na Maisha ya wastani, hutaweza kufanya jambo lolote kubwa hapa duniani. Watu wote waliofanikiwa na kufikia kuitwa mabilionea waliwaza katika namna ya kutatua matatizo ya watu kuliko kufikiria Zaidi wao binafsi.

Badili fikra zako kuanzia sasa. Tatizo lolote unalopitia sasa hivi kuna wengi wanapitia embu anza kuwatazama katika namna ya tofauti ona zile ni hela, yaani kwamba kila mmoja anaepitia tatizo kama lako ukiweza kulitatua basi atakulipa pesa nzuri. Zidisha hiyo pesa kwa idadi ya watu unaowaona wanapitia tatizo kama lako halafu utaona ni kiasi gani utakuwa unatengeneza.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

#usiishienjiani

www.jacobmushi.com/coach

SURA YA 440: Usichanganye na Maji.

Miaka kama 10 iliyopita Kulikuwa na bibi mmoja kijijini kwetu alikuwa anauza maziwa fresh.
Maziwa yake yalikuwa ni matamu sana na pia masafi hivyo kusababisha watu wengi kuyapenda na kuyasemea vizuri.

Kadiri watu walivyoyasemea vizuri ilifika wale waliokuwa wanauza maziwa kama yeye ikabidi wafunge kwa kukosa wateja. Watu Karibu mtaa mzima ulihamia kwake.

Bibi yule alizidiwa na wateja. Kiasi cha maziwa alichokuwa anatoa kilikuwa kidogo kulinganisha na idadi ya wateja.

Ikabidi bibi huyu aazimie jambo moja. Alianza kuchanganya maziwa yake na maji.

Kidogo kidogo maziwa yalianza kutosha lakini yakaanza kupungua ubora. Wateja wakashtukia mmoja akaanza kuwaelezea wengine na Habari zikasambaa kwamba maziwa yanachanganywa na maji.

Tabia ile ikampotezea bibj yule wateja. Mmoja mmoja Wakaanza kupungua. Ikafika wakati akawa hauzi kabisa.

Bahati mbaya Hakujua wateja walimkimbia kwasababu ya kuchanganya na maji maziwa yake. Aliamini amelogwa.

Bibi akaanza kuwachukia wale wauzaji wenzake kwani walianza kufungua upya biashara zao na wateja wakahamia kwao.

Bibi akaamua kwenda kwa mganga kutafuta dawa. Kumbe ndio anaharibu kabisa, badala ya kupata dawa akajikuta ameua na ng’ombe zake zote kwa dawa za mganga.

Unajifunza nini?

Njia pekee ya wewe kuendelea kuhudumia watu wengi ni kutokukubali kushusha viwango vyako.

Ni Bora uhudumie watu wachache kwa ubora kuliko watu wengi kwa ubovu.

Ni Bora uongeze bei kuliko kupunguza viwango.

Hata mahindi hupanda bei pale yanapohitajika sana.

Kubali kwamba changamoto unazopitia wakati mwingine ni wewe umezisababisha.

Achana na imani za kishirikina hazina msaada wowote kwenye biashara yako.

Rafiki Yangu naamini Umejifunza kitu kikubwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Jacob Mushi, Mwandishi na Mjasiriamali.

SURA YA 428; Ukitegemea Hiki Pekee Utachoka Haraka.

Mwanadamu pekee aliekuwa na akili sana kuliko wanadamu wengine ni Adamu na yeye alipewa uwezo huo kwasababu alikuwa peke yake. Hivyo kwa akili na uwezo aliokuwa nao ukamuwezesha kuyaendesha Maisha yake kwa urahisi. Kwasasa kila unachotaka kukifanya kwa kiasi kikubwa kinategemea wengine, inawezekana ni vifaa, au hata watu wengine utawahitaji ili uweze kuwa na ufanisi Zaidi.

Usikubali kutumia nguvu zako mwenyewe na kila kitu mwenyewe wakati kuna uwezekano wa kutumia wengine na ukafanikiwa. Jifunze ni kwa namna gani hicho unachokifanya sasa hivi ukiongezea kitu kutoka kwa wengine utaweza kufanikiwa Zaidi.

Usizitegemee akili zako mwenyewe, jifunze kwa wengine, muombe Mungu.

Usitegemee Nguvu zako mwenyewe, jifunze kuzitumia nguvu za wengine pia.

Usitegemee muda wako pekee jifunze namna ya kutumia muda wa wengine ili kuongeza uzalishaji wa haraka kwenye kile unachokifanya.

Usitegemee pesa zako mwenyewe jifunze namna ya kutumia pesa za wengine na kuzizalisha ili upate faida Zaidi.

Ipo siku utachoka, ipo siku utakuwa na majukumu mengi Zaidi hivyo ni muhimu kutengeneza mfumo wa kuweza kuwatumia wengine ili mambo yako yawe na uwezo wa kuendelea kwenda hata kama haupo. Iwe ni biashara au hata kipaji chako bado kuna namna unawahitaji wengine ili uweze kuwa na matokeo bora Zaidi.

Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

SURA YA 427; Njia Rahisi ya Kuwavuta Watu Sahihi Kwako.

Tupo kwenye dunia ambayo ni ngumu sana kumjua mtu kwasababu wengi wamevaa mavazi yanayofunika uhalisia wao. Wamevaa tabia za kuigiza ambazo sio za kweli na wala hawana kabisa. Wamevaa Maisha ambayo ni uongo na ndani yake wanateseka huku wakifurahia kuona watu wanawasifia.

Sasa ili uweze kuwavuta watu sahihi na kuwaacha hawa waliojivalisha mavazi ya uongo ili kufunika ule uhalisia wao inakupasa wewe uwe HALISI. Hakuna njia nyingine ukishaanza kuwa wewe, ukavaa vile unavyopenda na sio jamii inavyokulazimisha ukaishi Maisha ambayo wewe binafsi ndio unayataka kulingana na kipato chako. Ukaanza kuishi kile kilichopo ndani yako na kuisimamia haki na ukweli utawakimbiza kabisa watu wanafiki na kuwaacha watu sahihi ambao watakupenda kwa jinsi ulivyo.

Nimewahi kukutana na mtu ananiambia Jacob wewe ni mtu mkubwa sana, unapaswa uwe unavaa suti ili watu wakikuona wakuheshimu. Nilicheka nikamwambia kama mtu anataka kunikubali kwasababu nimevaa suti wapo wengi sana wanaovaa suti aende akawakubali hao. Kama mtu hawezi kunikubali kwa vile nilivyo na kile ambacho ninapenda mimi siwezi kufanya jambo lolote kumlazimisha akubaliane na mimi. Naamini pia ni sawa kabisa watu wasiponikubali, naamini hawawezi kunikubali wote na pia hawawezi kunikataa wote.

Usiishi Maisha ambayo yanaendeshwa kwa maoni ya wengine, usiishie kufuata kila ambacho watu wanataka ufanye utageuka kuwa mtumwa wao. Utakuwa ni mtu unaewaridhisha wengine huku moyo wako unaumia kwasababu hufanyi kile unachokipenda.

Ili uwavute watu sahihi kwenye Maisha yako amua sasa kuanza kuishi Maisha yako halisi. Vile ambavyo wewe unaona ni sahihi lakini ukumbuke tu usivunje sharia na wala usiende katika yale yaliyoko nje ya UADILIFU. Kwa kifupi fanya kile moyo wako unataka lakini kisiwe cha kumuumiza mtu mwingine, kisiwe sababu ya kumfanya mwingine atoke machozi.

Wavute watu sahihi kwa kufanya vitu sahihi ambavyo ulizaliwa kuja kufanya hapa duniani. Anza na kuishi lile kusudi la wewe kuja hapa duniani na utaanza kuwaona watu sahihi kwenye Maisha yako. Usiendelee kupoteza muda wako kufuata yale ambayo yametengenezwa na jamii badala yake ishi kile ambacho Mungu ameweka ndani yako.

Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

SURA YA 426; Hii Ndio Sababu Ya Wewe Kuanza Vizuri na Kumaliza Vibaya.

Hongera sana kwa kuona mwaka mpya, nafurahi pia kuona umesoma Makala hii kwa mara ya kwanza kwa mwaka 2019. Nimekuwa nahudhuria mikesha na matamasha ya kuingia mwaka mpya na siku zote nimekuwa najifunza kitu ambacho kimekuwa kinajirudia sana. Hakuna mwaka ambao umewahi kutabiriwa mabaya, na hata kama watasema utakuwa mwaka wenye magumu lazima watayataja mazuri mengi yatakuja.

Ukweli unakuja kwamba ili mwaka uwe wa ushindi, mavuno, kuvuna, kuinuka, kusogea, kufika viwango vingine inakupasa wewe binafsi uweke juhudi za kipekee na tofauti. Lazima wewe binafsi ujipange na ukubali kujitoa vya kutosha.

Mabadiliko na maendeleo yako sio muujiza, hakuna mafanikio ya kimiujiza Rafiki yangu. Hakuna mahali utakwenda kupewa nguvu Fulani ambayo itakufanya kila unachokifanya kifanikiwe vile unavyotaka. Acha kabisa kupoteza muda wako mwaka huu kwenda sehemu hizo za kupewa nguvu za namna hiyo.

Kila mmoja anaanza mwaka kwa hamasa kubwa na kelele nyingi lakini baada ya siku chache utaanza kuona kila mmoja analalamika kwamba Maisha ni magumu, mwezi huu haufai na mengine mengi. Baada ya muda sio mrefu sana utaanza kusahau kabisa malengo uliyojiwekea mwaka huu, pia inawezekana mpaka sasa hujaweka malengo yeyote na unasubiria mambo yatokee yenyewe.

Utakuwa unaendelea kupoteza muda wako kama mpaka sasa hujajua ni vitu gani unataka kwenye mwaka huu. Unajinyima haki zako wewe mwenyewe, unajikosesha fursa wewe mwenyewe, unajiweka kwenye hali mbaya wewe mwenyewe.

Habari njema ni kwamba bado nafasi ipo kama mpaka sasa hujaweka malengo yeyote anza leo andika kila kitu unachotaka kitokee kwenye Maisha yako mwaka huu. Andika pia ni lini unataka vitokee vitu hivyo na ni vitu gani unatakiwa ufanye ili viweze kutokea kama unavyopanga.

Kipaumbele chako kikubwa kwa mwaka huu kiwe ni wewe kuwa bora Zaidi hii ni kwasababu ukiwa bora Zaidi basi na sehemu nyingi kwenye Maisha yako zitakuwa bora. Hakuna kinacholeta matokeo mabaya kwenye Maisha yako tofauti na wewe ambaye sio bora. Ukiwa bora utapata matokeo bora, ukiwa mbovu utapata matokeo mabovu.

Tumia nguvu nyingi katika kujiboresha kuliko hata unavyowekeza kwenye vitu vingine hii ni kwasababu wewe usipokuwa bora hata hivyo vitu vingine hutaweza kuvisimamia. Ukitaka kumaliza mwaka vizuri na matokeo chanya hakikisha wewe unakuwa bora Zaidi.

Mwisho ni kwamba kama unataka matokeo anza sasa, usiseme tena mpaka tarehe fulani au ngoja mpaka mwezi huu ufike katikati. utachelewa sana chukua hatua sasa rafiki yangu.

Karibu kwenye program ya mwaka wa ushindi kama utahitaji msaada Zaidi katika kuwa na mwaka wenye matokeo chanya na mwaka wa mtu alie bora Zaidi. Bonyeza maneno haya

Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

TUSEMEZANE 424; Ukimpata Usikubali Aondoke.

Katika Maisha tunakutana na watu wa aina mbalimbali wanaweza kuwa wabaya kwetu na wengine huwa baraka kubwa sana kwenye Maisha yetu. Unaweza kukutana na mtu wa pekee sana kwenye Maisha yako na usiweze kujua kwasababu shetani amefunga ufahamu wako usione huyu mtu ni wa namna gani.

Ni vyema ukawa na uwezo wa kufahamu wale watu ambao Mungu anakukutanisha nao kwasababu mara nyingi wanaweza kuwa sababu ya wewe kusogea hatua nyingine. Usikubali mtu ambaye ana vitu vya pekee ndani yake aondoke bila ya kukugawia sehemu ya vitu vile alivyobarikiwa.

Tunaona kwenye Biblia Nabii Elia wakati anaondoka Elisha mtumishi wake alimuomba amuache japo sehemu ya nguvu alizokuwa nazo. Elisha alifanikiwa kuachiwa vazi ambalo lilikuwa ni baraka kubwa na msaada kwenye huduma yake.

2 Wafalme:2.9 Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.

Jiulize wewe ni mara ngapi watu wa maana wamekuja kwenye Maisha yako na baadae unakuja kusikia wamekuwa watu wakubwa sana na hata huwezi kupata nafasi ya kuwasogelea tena? Je watu hawa ungeweza kuwatambua mapema ingekuaje kwako?

Usikubali watu hawa waondoke bila ya wewe kujifunza kitu kwenye Maisha yao, bila ya wewe kuondoka na kitu ambacho Mungu aliwabarikia kuliko wewe. Kilichofanya Elisha akapata kupewa nguvu zile ni kwasababu alijua kung’ang’ania, alidhamiria kumfuata Elia hadi saa ya mwisho japokuwa aliambiwa asiende.

Kuna vitu hutavipata kwa kuomba peke yake bali kwa kuamua kuwa king’ang’anizi, usiogope kuonekana vibaya. Utaonekana wewe una shauku na una nia ya dhati kwenye kile ulichokiomba, usiombe mara moja halafu unasubiri majibu hapana, kumbusha kumbusha, sumbua sumbua, wacha uonekane msumbufu lakini kwa jambo ambalo ni jema.

Usikubali kumwacha aondoke mtu huyu wa maana ambaye amekuja kwenye Maisha yako. Hajaja bure, hujakutana nae bure, kuna jambo ameagizwa akuletee lakini yakupasa kulipa gharama kidogo ili upate kile ambacho unataka.

Kama mlango umefungwa usiondoke, ngonga kwa nguvu, sumbua walioko ndani hadi watoke waje kusikiliza shida yako.

jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

NGUVU MPYA 423; Usikae Hapo Muda Mrefu Sana.

Unaweza kufanya mambo makubwa kwenye Maisha yako na ukashindwa kusogea mbele tena kwasababu moja ya kulewa na yale matokeo. Jambo ambalo tayari umeshalifanya na ukashinda halitakiwi liwe ndio jambo unaloliongelea sana kwamba umelifanya. Waachie wengine walizungumzie wewe nenda katafute jambo jingine kubwa Zaidi la kufanya.

Sijasema usifurahie matokeo uliyopata bali nasema usifurahie sana hadi ukasahau kwamba bado upo safarini. Mafanikio ni vita, unaposhinda pambano moja usifurahie sana ukasahau kujiandaa kwa pambano linalokuja mbele.

Unatakiwa uwe na kiasi katika kufurahia ili uweze kujipanga tena kwa pambano jingine. Fahamu pia kuna wengi hawajafurahia mafanikio yako na wataanza kutafuta kila namna ya kukurudisha chini. Kama utakuwa umejisahau kwenye kufurahia utajikuta umeshindwa kujipanga kwa vita nyingine inayokuja.

Unapovuka hatua yeyote ya mafanikio usikubali kubaki kwenye hiyo hatua muda mrefu. Tafuta kusogea mbele kwa hatua nyingine tena. Hata kama mambo yako sawa na huna shida yeyote usikubali kubaki na hali ile ile jiongeze jaribu kusogea mbele Zaidi. Hii ni moja ya njia ambayo inawafanya waliofanikiwa waendelee kufanikiwa Zaidi. Hawakubali kubakia na yale matokeo waliyoyapata jana, kila leo wanajaribu vitu vipya vya kuwafanya waendelee kusonga mbele.

Angalia Zaidi kule mbele unapokwenda kila siku kuna mabadiliko mapya yanakuja ya aina mbalimbali. Ukikaa sehemu moja muda mrefu unaweza kuchelewa kuyapokea mabadiliko na hivyo kujikuta umekwamia hapo hapo ulipokaa muda mrefu.

Kila wakati penda kuangalia mbele na kuona ni mabadiliko gani yanaweza kuja na yataathiri vipi kile unachokifanya. Usikubali kuona wewe tayari ndio umefika na hakuna anaeweza kukutoa hapo. Mambo yanabadilika na unaweza kujikuta umebaki hapo na huna chochote.

Rafiki bila kujalisha wewe ni wa pekee kiasi gani na vitu vyako unavifanya kwa upekee kwa namna gani bado kuna watu watakuja wajaribu kuiga kile unachokifanya. Na kama sasa wewe umelala na umesharidhika na ule ushindi ulipata jana utajikuta wale waliokuja kukuiga wameweka mambo mapya na wakakuacha pale pale ulipokuwa umelalia.

Songa mbele, piga hatua kila wakati usikubali kuishia njia.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

NGUVU MPYA 422; Eneza Habari Njema.

Watu wamekuwa ni mashujaa sana wa kueneza habari mbaya kuhusu wengine, imekuwa ni desturi yetu pia kutoa vipaumbele Zaidi kwenye habari mbaya kuliko njema. Wafuatiliaji wa habari na watoaji wa habari wote wamekuwa wakipendelea Zaidi habari mbaya.

Kwenye Maisha yako kama unataka kufanya jambo lenye kuacha alama basi chagua kusema kile ambacho kinawasaidia wengine. Habari yeyote inayomhusu mtu kama sio njema basi usiiseme mahali kama unajua haitamsaidia yule unaemwambia.

Jifunze kutafuta yaliyo mema juu ya mtu na kama unataka kumuelezea muelezee kwa mema yake. Kuna watu wanabadilika kwasababu sisi tumeweza kuona yaliyo mema ndani yao hata kama ni kidogo.

Jifunze kuzungumza habari njema kwasababu wengine pia watavutiwa kukusikiliza. Ukiwa mueneza habari mbaya utaanza kujulikana kama Mbeya, na wakati mwingine watu wataanza kukuepuka.

Ukiwa mueneza habari njema watu watapenda kukueleza mambo yao kwasababu wanaamini huwezi kwenda kusema popote.

Kama huna sifa yeyote nzuri basi anza na hii ambayo ni rahisi sana na wala haikuhitaji uwe na mtaji wowote. Wewe anza tu kuzisema habari njema kuhusu watu wengine na mwisho wa siku utakuwa umelitengeneza jina lako vizuri na utawasaidia wengine pia.

Habari njema zinajenga.

Habari njema zinatia moyo.

Habari njema ni hamasa ya kusonga mbele.

Habari njema zinawasaidia waliokata tamaa.

Habari njema zinaleta tumaini jipya kwa wale waliotaka kurudi nyuma.

Kuna wale wapelelezi waliotumwa kwenda kuipeleleza nchi ya Kaanani kati yao wote wawili tu ndio walioleta habari njema. Wale walioleta habari mbaya za hofu na za kukatisha tamaa waliuwawa. Hivyo basi Rafiki yangu embu amua kuwa mueneza habari njema kwa wengine. Habari za matumaini na za kuwafanya waone duniani bado ni mahali pazuri kuishi.

Njia rahisi ya kuacha kuwa mtu wa habari mbaya ni wewe kuanza kubadilisha chanzo kinachokupa habari mbaya. Usifuatilie habari mbaya kabisa. Usisikiliza habari mbaya za wengine, ukikuta watu wanawasema watu vibaya waulize hivi hakuna jambo lolote zuri tulijadili hapa? Au unaachana nao unaondoka zako.

Sijasema watu wanaofanya mabaya waachwe hapana, kama mtu kafanya yaliyo mabaya ukimsema au ukaeneza mabaya yake hayatamsaidia yeyote hata yeye mwenyewe. Hivyo basi tafuta namna ya kumsaidia kama unataka kumsaidia. Mfate mwambie au tumia njia nyingine yeyote nzuri na ambayo ungependa wengine waitumie kwako unapokosea.

Kuwa mueneza habari njema kwa kuanza kupokea habari njema.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha