Category Archives: USIISHIE NJIANI

Mafanikio ni Mchakato.

Nilipokua sekondari tulitumia barabara mbaya sana kuelekea shuleni kitu kilichofanya safari iwe ya kuchosha sana na yenye kuchukua muda mrefu sana.
Kipindi hicho barabara nzuri ya lami ilikua ikitengenezwa, kila nilipokua nikisafiri kwenda na kurudi shule nilitumia muda huo kujifunza juu ya ujenzi wa barabara!

Ujenzi wa barabara unapoanza unaudhi sana kwani miti hukatwa , udongo huchimbuliwa na miamba huvunjwa, ni kazi isiyotamanisha kuiangalia inapoanza,

Na watu wengi hawapendi kusafiri barabara inapojengwa maana safari huwa ya kuudhi na kuchosha sana!
Ujenzi wa barabara ya lami ni mfano wa mtu anayepitia mchakato kuelekea mafanikio,
Mambo yanayomtokea mengi huwa ya kuudhi na lengo ni kumuimarisha na mengine huja ili kumkatisha tamaa,
Dharau,kejeli,njaa,magonjwa,kuumizwa,kutokukubaliwa na mengine mengi yanayoudhi!
Mara nyingi watu humuepuka na hukwepa kuwa naye karibu kwa kuhofia shida anazopitia!
Na marafiki wengi waliokosa utu humuumiza mtu aliye ktk mchakato kwa kutokujua kesho yake kutokana na anayopitia!
Mfano wa barabara ikishakamilika kila mtu hufurahia na hutamani kuitumia na kuielezea jinsi ilivyojengwa na ilivyo bora!

Na mtu akishafanikiwa kufikia aliyoandikiwa ndipo kila mtu hutamani kuwa naye na hutamani kila mtu ajue kuwa anajuana nae!

Ili uwe mtu bora lazima upitie hatua mbalimbali mfano wa barabara ijengwayo,
Lazima upitie MCHAKATO ndio uwe bora zaidi!
Watu wa kawaida hawapitiagi hatua za ukuaji za kimchakato!

NB. Usiogope mchakato, usiogope watu kukuacha ukiwa mchakatoni
Songa mbele!

Uwe mtumishi wa MUNGU,una huduma,una vipaji, una ujuzi flani, lazima upite kwenye mchakato ili uwe bora!

Watu wote bora tunaowasoma kyk Biblia walipitia michakato tena migumu mnoooo!
Tukiwatazama kina Yusuphu,Musa,Yohana,Petro,Ibrahimu ni mifano mikubwa!
Tumwangalie MUNGU na tusonge mbele

#Noturning back
By Theofrida Gervas

Haijalishi Umezaliwa Wapi, Maisha ni Zawadi.

Katika maisha haya kamwe usimlaumu mtu yeyote kwasababu ya kushindwa kwako au kufeli kwako jambo fulani, kwasababu kulaumu hakuibadilishi hali bali kunatengeneza tatizo lingine linaitwa KiNYoNgO.

Hakuna mtu aliyetuma barua ya maombi kwa MUNGU azaliwe katika familia fulani yenye hali fulani au uzuri fulani, Wote tumezaliwa tumejikuta watoto wa fulani na fulani, Wengine wamezaliwa wamejikuta kwenye ndani ya kasri wamezungukwa na wahudumu kila pande.

Wengine wamezaliwa wamejikuta kwenye banda linalovuja kiangazi na kuchoma jua masika,
Wengine wamezaliwa kwenye elimu yaani baba professor mama Daktari.

Wengine wamezaliwa tu wamekuta mama anapigwa vibao anaburuzwa,
Mwingine amezaliwa amekuta mama yake anajiuza mwili,mwingine amezaliwa mahali watu wanatumia madawa ya kulevya,
mwingine amezaliwa mahali watu hawajawahi enda shule wala kufanikiwa
Wengine wamezaliwa tu wazazi wao wakafariki papo.

Mwingine amezaliwa amezungukwa na chupa za bia, mwingine vichochoroni, mwingine kanisani,mwingine vitani kwenye mabomu na risasi….
Kila mtu na alivyozaliwa ndio maisha..

Tatizo sio kuzaliwa hapo, kwenye taabu na shida nyingi Tatizo ni kuendelea kuwa hapo….
Kila mmoja Mungu amemwandikia story yake ya Ushindi ni Wewe Kuamua kuchukua hatua na kutoka kujikwamua kwenye shida hiyo…..

Mradi upo hai unaweza kuvuka……..
MSHUKURU MUNGU KWA ZAWADI HII YA MAISHA na kuyatumikia kwa ajili ya UTUKUFU WA UFALME WAKE ALIYEKUWEKA

*kuzaliwa zizini haimaanishi uishi hadi ufie zizini*
Waweza zaliwa zizini ukaishi Ikulu na kuishia Ufalmeni

By
Theofrida Gervas

531; Ni Hatua Ndogo Ndogo.

Kinachoangusha mtu sio shoka moja lilipigwa kwa nguvu bali ni mkusanyiko wa kukatwa kidogo kidogo hadi mti unafikia hatua unakuwa umeanguka. Yale mambo makubwa unayotaka kuyafanya kwenye maisha yako unaweza kuyatimiza tu endapo utaamua kuanza kwa hatua ndogo ndogo.

Angalia ni kitu gani kidogo tu ambacho unaweza kufanya na kisha ukifanye. Usikae na kusema sina mtaji wa kutosha lakini kile kidogo ulichonacho hujaweza kukitumia. Kabla hujataka kuifikia kumi basi hakikisha umeweza kuitumia tano vizuri.

Kuna hatua hutaweza kuzifikiwa kama muujiza lazima uweke nguvu kidogo kidogo kila siku. Miaka mitano iliyopita ulikuwa unalalamika tatizo sina mtaji lakini ungeacha kulalamika na kuanza kuchukua hatua hata ya kuweka pesa kidogo kidogo kila siku au kila mwezi mwaka huu ungekuwa umefika hatua nyingine.

Rafiki nataka nikwambie chochote kikubwa unachotaka kufanya usitake kukianza kikubwa tafuta namna unavyoweza kuanza kidogo kwa hatua ndogo. Hii itakusaidia sana kukuwa na pia kupata uzoefu sana tofauti ya yule ambaye ameanza moja kwa moja akiwa na kila kitu.

Pata vitabu Vyangu kwa kubonyeza link hii www.jacobmushi.com/vitabu

Nikutakie Kila la Kheri.

Rafiki yako

Jacob Mushi.

530; Unavyovihofia Vingi Havipo Kwenye Uhalisia.

Habari ya siku rafiki, pole kwa changamoto ya Ugonjwa huu wa COVID-19. Nakutia Moyo usiogope tunakwenda kuvuka pamoja.

Kila kitu hutengenezwa kuanzia kwenye akili zetu. Furaha, huzuni, matatizo, na kila aina ya vitu ambavyo hutusumbua na kutufurahisha huanzia ndani yetu.

Vile unavyofikiri mara nyingi ndio huwa tatizo kuliko hata tatizo lenyewe, moyo wako ukijaa wasiwasi, hofu na mashaka juu ya jambo fulani asilimia kubwa ya vile unavyoona huwa imejaa zaidi kwenye hofu.

Hii husababishwa na uwezo wa akili yetu kuumba vitu (imagination) mfano umeingia kwenye simu ya mpenzi wako ukakutana na sms ambayo haiweleweki. Moja kwa moja utaanza kujenga mawazo kwamba huyu mtu ananisaliti, akili yako itaanza kukupa matukio mbalimbali ya nyuma ili kuthibitisha kile ulichokiona kwenye sms.

Mwisho wa siku kumbe ni mawazo yako tu hakuna ukweli wowote. Nataka nikwambie kitu kimoja jifunze kuyaongoza mawazo yako, jifunze kuzitawala hisia zako. Hisia zako ukishindwa kuzitawala zitakupeleka kwenye fikra potofu.

Hisia zako ukishindwa kuzitawala utajikuta unawaza mambo ya ajabu ajabu ambayo yatakupelekea kushindwa kuchukua hatua sahihi kwenye maisha yako.

Hisia za hofu huleta fikra za kushindwa ndani yako, usiruhusu ziutawale moyo wako.

Huwezi kuishi bila kuwa na hofu kabisa kwasababu vipo vitu vingi vinakuwa nje ya uwezo wako, kitu pekee unachoweza kufanya ni kuziongoza hisia zako na fikra zako.

Unapokuwa na hofu jitahidi uwe unajinenesha maneno ya kukutia nguvu na ujasiri. Jisemeshe nakwenda kushinda, nakwenda kuvuka hili jaribu, Mimi ni mzima, tayari nimepona, Nimelivuka hili jaribu, ninavuka hizi changamoto.

Maneno kama haya yatakufanya uweze kuzishusha chini hisia za hofu na utaweza kufikia ushindi mkubwa.

Kumbuka tunaambiwa tusiogope kwasababu kuna vitu vinaogopesha, tunatakiwa tuwe majasiri kwasababu kuna mambo mazito tunakwenda kupitia.

Yoshua 1:9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.

Unaweza kununua vitabu Vyangu kwenye link hii https://www.getvalue.co/home/seller_collection/200

Nakutakia Kila La Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

529; HEKIMA: Ongeza Viwango Vyako Vya Kufikiri.

Habari Rafiki yangu, leo ni siku ya pekee sana kwangu, kwani ndio siku nilizaliwa, naikumbuka hii tarehe na ninafurahi pamoja nawe. Nimekuandikia Makala hii uifurahie pamoja nami katika kukumbuka siku hii.

Siku moja nilikuwa napita kwenye jingo lililokuwa linajengwa maeneo ya Mlimani City, jingo lile ni refu san ana linatamanisha. Wakati natafakari nikapata mawazo ambayo nimekuwa natamani nikuandikie siku moja ujifunze, hatimae leo nimeweza kukuandikia Makala hii ujifunze yale niliyojifunza wakati napita jirani na jingo lile.

Niliwaza kwamba kuna watu wengi kama wanapita maeneo yale au wanaweza kuona jingo lile kwenye picha na wakalitamani kama mimi niliyoona linavutia. Nikawaza Zaidi hivi watu hawa watakuwa wanawaza nini ndani ya vichwa vyao baada ya kuliona jingo hili zuri? Nikajiwa na majibu kama manne hivi ambayo nakwenda kukushirikisha.

a/ Wapo watakaowaza Kwamba Haya ni Mambo ya Matajiri Tu Mimi Maskini Nitaishia Kutazama kwenye Picha….

Ukweli haya mawazo huenda ulikuwa unawazaga vinapoPita mbele yako vitu mbalimbali ambavyo huna uwezo navyo au unaviona ni vya gharama sana.

Umekuwa unajiweka kwenye kundi la watu ambao hawastahili vitu fulani kutokana na hali uliyonayo.

b/ Wapo ambao watatamani sana wangepata ajira kwenye ofisi mbalimbali ambazo zitakuwa ndani ya Jengo Hili.

Ndio kuna ambao akili zao kitu cha kwanza watawaza au watatamani endapo wangeajiriwa hapo ili kila siku wawe wanapandisha kwenye lifti ?.

c/ Wapo wengine watawaza kufungua biashara zao kwenye hili Jengo.

Ndio nikwambie ukweli hata mimi pia niliwaza hivi nikasema nitakuja kuuliza bei za vyumba vya juu juu kabisa.

d/ Wapo kundi la mwisho ambalo na mimi nilikuwepo, hawa watawaza hivi kumiliki Jengo kama hili nitahitaji kuwa na pesa kiasi gani? Gharama za hili Jengo zima ni Tsh ngapi?

Watajiuliza hivyo na ipo siku watapata majibu ya maswali yao au ya kile walichokuwa wanatamani.

Naomba nikuulize swali Rafiki wewe upo kundi gani? Unatamani kuwa sehemu ipi? Je mawazo yako yameishia wapi?

Ni mambo mangapi umekuwa unajiwekea ukomo wa kufikiri kuwezekana? Je umekuwa unajiona wewe ni kiwango Fulani hivi hivyo huwezi kuwaza hayo mambo ni makubwa sana.

Inawezekana hata ukisikia zile ndoto za kuwa bilionea unazikataa kabisa unasema mimi bado sijafikia kuwaza hayo makubwa hivyo.

Nataka nikwambie mtu atapata kile ambacho anakipigania, kile ambacho umeona unastahili ndicho haswa utakipata. Ikitokea umeenda Zaidi basi itakuwa ni bahati tu.

Usijipimie viwango kutokana na hali uliyonayo sasa hivi.

Usijiwekee kwenye kundi Fulani kwasababu eti sasa hivi hela ya kula ni shida.

Usione wewe huwezi kuwa bilionea kwasababu tu eti sasa hivi hujaweza kumsaidia mtu elfu kumi.

Usione kwamba ni vibaya kuwaza mambo makubwa ambayo hujayafikia.

Ndio ni kweli unaishi kwenye nyumba ya kupanga mpaka sasa lakini hiyo sio sababu ya wewe kuacha kuwaza kumiliki ghorofa refu kuliko yote hapa nchini. Hali uliyonayo sasa hivi haitabaki milele, chochote kile unachotamani kuwa usiogope kuwaza au kuandika.

Ndoto za wengi zimekuwa zinazimwa kwa woga wa kuwaza, unaogopa hata kuwaza kufikia level za kina Moo Dewji eti kwasababu tu sasa hivi kula ni shida. Sasa kwani ukiwaza kufikia level za Moo utaishiwa hela ya kula? Si ndio juhudi za kutafuta zitaongezeka? Acha woga Rafiki yangu. Pandisha viwango vyako vya Imani.

Hakuna ambaye amewahi kutimiza kitu ambacho hajakiwaza kwenye kwenye akili yake. Anza kutengeneza mawazo makubwa nenda mbali Zaidi ya wengine wanavyowaza.

Usiogope Ndoto Yako Inawezekana. Kile unachotamani kitokee kwenye Maisha yako, kinawezekana badili tu fikra zako. Vile viwango ulivyokuwa unasema hivi sio level zangu bado zinaweza kuwa level zako badili tu unavyofikiri. Ona kuwezekana kwenye chochote kile unachokitamani.

MWANZO WA MAMBO YOTE NI KWENYE FIKRA ZETU.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

527; HEKIMA: Kinyozi Anapokosea Kukunyoa.

Kinyozi anapokosea kukunyoa bila kujali amekosea kiasi gani siku zote baada ya muda Fulani nywele huota tena na utaweza kunyoa vile unavyotaka. Unapopoteza fedha haijalishi ni nyingi kiasi gani kama ni wewe mwenyewe ulizitafuta basi utaweza kuzipata tena.

Unapoachwa na mpenzi ambaye ulimpenda sana bila kujali alikuwa mzuri kiasi gani, bado ipo siku utakuja kukutana na mtu mwingine mzuri kuliko yeye na utampenda kuliko yeye. Ni wewe tu kuamua kwamba yaliyopita yapite uendelee na safari.

Kipo kitu kimoja kikitokea kwenye Maisha yako huwezi kubadilisha tena, kitu hicho ni KIFO. Unapokufa inakuwa ndio mwisho wako wa kufanya vitu hapa duniani. Huwezi tena kurudi kuja kubadilisha chochote. Na bahati mbaya sana baada ya kufa hakuna ajuae kinachoendelea au mtu anakuwa wapi.

Sasa nikuombe wewe ambaye upo hai usikubali jambo lolote ambalo linaweza kubadilishwa likuumize kichwa au likufanye ukate tamaa. Nataka ukumbuke kwamba ipo siku utakufa na hutopata tena hiyo nafasi ya kuanza upya uliyonayo sasa.

Dunia haina shida wala haijutii wewe ukifariki, kila siku wanazaliwa watu wapya ambao watakuja kufanya kile ambacho wewe ulishindwa kufanya. Sasa usikubali kuondoka hivi hivi, usikubali alama uliyotakiwa kuiacha ije iachwe na mtu mwingine.

Ndugu yangu kinyozi akikosea kukunyoa kumbuka kwamba nywele zitaota ten ana utakuja kurekebisha vile unavyotaka. Lakini siku ukiondoka ndio inakuwa imekwisha hakuna kingine utakachoweza kufanya. Hivyo basi nikukumbushe tena usikubali kuacha kutumia nafasi yoyote inayokuja mbele yako ambayo inakuwezesha wewe kufika kule unakotaka. Usikubali kukata tamaa na kusema haiwezekani na wakati bado upo hai.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

526; HEKIMA: Sumu Niliyowekewa Kwenye Chakula.

“Ilikuwa ni siku za mwisho wa mwaka ambapo tulikuwa na utaratibu wa kwenda kuwasalimia ndugu na jamaa ambao hatujawaona miaka mingi.

Katika kuwatembelea ndugu jamaa na marafiki wengi siku moja nikapitia kwa ndugu mmoja ambaye hatukuonana muda mrefu sana.

Huyu ndugu baada ya kunipokea alinisisitiza sana nile chakula. Nilimkatalia kwasababu nimepita nyumba nyingi na nimeshakula.

Lakini kwa maneno yake matamu nikajikuta nakubaliana nae. Akaniwekea chakula kingi kweli.

Tulikuwa tumekaa nje chini ya mti mkubwa wa mwembe, pembeni yangu nilizungukwa na kuku mwenye vifaranga aliekuwa anatafuta chakula.

Wakati nasubiria mwenyeji huyu aniletee maji ya kunawa ili nile chakula kile nikaona si vibaya nikiwatupia hawa vifaranga chakula kidogo tu (ulikuwa wali).

Wakati naendelea kusubiria maji ya kunawa akapita mtu kwenye njia iliyopakana na nyumba ya mwenyeji wangu. Akanisalimia nilikuwa nimemsahau kabisa. Kumbe nilisoma nae shule ya msingi.

Nikaondoka chini ya mwembe ule kwenda kumfata kwa karibu, wakati huo mwenyeji wangu hajaleta maji sijui ni nini kilimchelewesha.

Kumbe wakati naondoka yule kuku mwenye vifaranga akarukia juu ya kiti nilichoweka chakula akakimwaga na akaendelea kula na wanawe. Nikageuka kurudi kumfukuza lakini chakula chote kilimwagika.

Nikasema labda huyu kuku ndie alitakiwa ale hiki chakula. nikaendelea na kusalimiana na yule ndugu. Akaondoka, wakati narudi na mwenyeji nae alikuwa anakuja na maji. Kumbe chakula kuku ameshakimwaga.

Akasema anakwenda kunipakulia kingine, nikamkatalia nikamwambie ulinilazimisha sana ndio maana kimemwagika.

Tukaagana nikaondoka.

Kumbe Baada ya kuondoka masaa kadhaa baadae nakuja kuambiwa yule kuku pamoja na vifaranga wake wote walikufa.

Chakula nilichotakiwa kula kiliwekwa sumu ambayo ingeniua taratibu.

Mungu ni mkubwa sana akaniokoa na kifo, kwa namna ya ajabu.”

Nataka ujifunze hapa kitu kikubwa katika maisha yako rafiki.

Kuna amengi hutokea kwenye maisha tunayaona kama ni mabaya au ni mikosi lakini wakati mwingine ni mipango ya Mungu kutuokoa na tusivyoviona.

Unaweza kuachwa na gari kumbe uliokolewa na ajali mbaya.

Unaweza kuachwa na mpenzi kumbe umeokolewa na tatizo la maisha.

Unaweza kutengwa na ndugu kumbe ni ili uweze kukutana na watu watakaoweza kukusaidia.

Hakuna kitu kinatokea kwa bahati mbaya, yule mwenyeji wangu hakuchelewa kuniletea maji kwa bahati mbaya japo ningeweza kumlaumu.

Yule ndugu niliesoma nae aliepita akasababisha chakula kumwagwa na kuku hakupita tu kwa bahati mbaya. Alipita kwa kusudi maalumu. Huenda alikuwa apite mahali pengine lakini akasukumwa kupita njia ile bila hata yeye kujua.

Yule kuku na vifaranga vyake sio kwamba walishindwa kwenda kutafuta chakula shambani, hapana walikuja pale chini ya mwenye kwa kusudi la Mungu la kuniokoa.

Lolote baya linalotokea kwenye maisha yako usiwe mwepesi kulalamika, tafakari jiulize ni kwanini haya yanatokea. Ni kwa kusudi lipi?

Kuna mengine yatatokea leo ili tu uje utimize kusudi miaka 20 ijayo.

Musa hakuwekwa kwenye kisafina bahati mbaya, alikuwa anaandaliwa.

Yusufu hakuchukiwa na ndugu zake bahati mbaya yalikuwa ni makusudi maalumu ambayo yalikuja kuonekana miaka kadhaa mbele.

Wewe unapitia ugumu leo unakata tamaa, unapitia changamoto fulani leo unakata tamaa. Ndoto zako unaacha kuzifuatailia kumbe yale yanayotokea yanakuandaa kuelekea kwneye ndoto na kusudi lako.

Nataka Ujifunze kwenye kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako kila siku.

Nakutakia Kila La Kheri.

Kupata huduma na Bidhaa mbalimbali kwenye mtandao huu bonyeza linki hii www.jacobmushi.com/kocha

Makala hii imeandikwa na Kocha Jacob Mushi. Mwandishi wa Vitabu na Makala, Kocha wa Maisha, na Mjasiriamali.

523; HEKIMA: Uzima Ni Fursa

Kuna mtu yupo hospitali anamlilia Mungu ampe uzima ulionao, halafu wewe ni mzima na unakata tamaa.

Jacob Mushi

Unapotaka kukata tamaa kumbuka kwamba kuna watu ambao wanalilia nguvu ulizonazo sasa hivi. Kuna mtu anaipigania pumzi ya mwisho ili angalau aendelee kuwa hai.

Nataka ujue kwamba uzima ulionao ni fursa kubwa sana kwasababu ni nafasi ya kujaribu tena. Ni nafasi ya kujifunza kwenye makosa uliyofanya.

Kuna watu wamefanya mambo wakakosea na kukosea kwao kukawa sababu ya kupoteza maisha. Wewe ulie mzima unakubalije kusema huwezi kufanya tena.

Kila siku mpya unayoiona ni nafasi nyingine tena ya kuchukua hatua mpya, kujifunza vitu vipya, kukutana na watu wapya kwa ajili ya kesho yako.

Usikubali kuridhika na hatua ambayo umefikia sasa hivi, usikubali kuendelea kubakia kwenye hatua uliyofikia sasa. Tumia uzima ulionao kuchukua hatua ya kusonga mbele.

Kesho yako ipo mikononi mwako, kesho yako ipo kwenye uzima ambao umepewa.

Kupata huduma mbalimbali ninazotoa tembelea kwenye link hii www.jacobmushi.com/huduma

Nakutakia Kila la Kheri

Rafiki Yako

Jacob Mushi.

522; HEKIMA: Kabla Hujakata Tamaa

Jaribu Tena, ndio nasema jaribu tena bila kujalisha umeshajaribu mara ngapi. Jaribu tena ukiwa na uhakika kwamba kuna jipya ulilojifunza kichwani kwako.

Jaribu tena bila ya kuhofu labda utakosea tena. Kama tayari kuna somo umepata kwenye kushindwa kwako basi utakuwa na ujasiri wa kujaribu tena.

Watu wengi hukata tamaa kabla hawajakaa chini na kujitazama ni kipi kinachosababisha washindwe.

Wewe usikubali kuwa kama watu wengi, anza kwa kuangalia ndani yako. Jua ni kitu gani hukijui, kwasababu kama unashindwa mahali ni kwamba kuna kitu hujakijua vizuri.

Kwa kujaribu tena unajiongezea nafasi ya kukishika vizuri kile ambacho ulikuwa hukijui.

Kabala Hujakata tamaa, jaribu tena, jifunze tena, chukua hatua tena, omba msaada tena.

Usikubali tu kirahisi na kupotelea njiani.

USIISHIE NJIANI, JARIBU TENA.

Kupata huduma mbalimbali ninazotoa tembelea kwenye link hii www.jacobmushi.com/huduma

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako

Kocha Jacob Mushi.

SURA YA 428; Ukitegemea Hiki Pekee Utachoka Haraka.

Mwanadamu pekee aliekuwa na akili sana kuliko wanadamu wengine ni Adamu na yeye alipewa uwezo huo kwasababu alikuwa peke yake. Hivyo kwa akili na uwezo aliokuwa nao ukamuwezesha kuyaendesha Maisha yake kwa urahisi. Kwasasa kila unachotaka kukifanya kwa kiasi kikubwa kinategemea wengine, inawezekana ni vifaa, au hata watu wengine utawahitaji ili uweze kuwa na ufanisi Zaidi.

Usikubali kutumia nguvu zako mwenyewe na kila kitu mwenyewe wakati kuna uwezekano wa kutumia wengine na ukafanikiwa. Jifunze ni kwa namna gani hicho unachokifanya sasa hivi ukiongezea kitu kutoka kwa wengine utaweza kufanikiwa Zaidi.

Usizitegemee akili zako mwenyewe, jifunze kwa wengine, muombe Mungu.

Usitegemee Nguvu zako mwenyewe, jifunze kuzitumia nguvu za wengine pia.

Usitegemee muda wako pekee jifunze namna ya kutumia muda wa wengine ili kuongeza uzalishaji wa haraka kwenye kile unachokifanya.

Usitegemee pesa zako mwenyewe jifunze namna ya kutumia pesa za wengine na kuzizalisha ili upate faida Zaidi.

Ipo siku utachoka, ipo siku utakuwa na majukumu mengi Zaidi hivyo ni muhimu kutengeneza mfumo wa kuweza kuwatumia wengine ili mambo yako yawe na uwezo wa kuendelea kwenda hata kama haupo. Iwe ni biashara au hata kipaji chako bado kuna namna unawahitaji wengine ili uweze kuwa na matokeo bora Zaidi.

Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha