Maana ya upendo ni kupoteza baadhi ya vitu ili upate kile unachosema unakipenda. Kama wewe unasema unapenda mafanikio upo tayari kupoteza nini ili uyapate hayo mafanikio?
Unaposema unampenda mtu upo tayari kupoteza nini ili uendelee kubaki nae? Kama unakosa majibu sahihi mara nyingi unakuta hujapenda umevutiwa tu na mtu yule.
Sijawahi kuona upendo ambao hauna kujitoa na kujitoa ni kupoteza. Ndio kujitoa kwa namna ya kwanza ni pale unapotoa muda wako kwa ajili ya kile kitu unachokipenda, muda ndio kitu chenye thamani Zaidi kuliko vitu vyote hapa duniani.
Unapotoa muda wako kwa ajili ya kile unachokipenda hatua ya pili lazima ukubali kuwaacha baadhi ya watu au vitu ili sasa muda ulioutoa kwa ajili ya kile unachokipenda uweze kuonekana thamani yake.
Mfano huwezi kusema wampenda mtu na umejitoa kwa ajili yake halafu bado kuna watu ambao wanaweza kukufanya wewe uachane na mtu yule. Watu hawa wanaweza kuwa labda ni wazazi, au marafiki au wengine unaowajali.
Kama unafikiri natania jitazame tu hicho kitu unachosema unakipenda upo tayari kukipigania hadi kifo? Yaani upo tayari kukipata kweli? Kama unahisi utakuja kukata tamaa kwa ajili ya ugumu utakaokutana nao njiani basi wewe hujakipenda hicho kitu.
Mara nyingi tumekuwa na marafiki ambao tunadhani wanaweza kuja kuwa msaada kwetu kwa namna moja ama nyingine lakini kama una rafiki ambaye anakuwa sababu yaw ewe kukosa kile unachosema unakipenda unakuwa chaguzi za aina mbili ubaki na rafiki au ubaki na kile unachosema unakipenda.
Ukiona kuna watu unabaki unawang’ang’ania kwenye Maisha yako kwa sababu yeyote ile ilihali hawaendi pamoja kule unakotaka kwenda basi ujue hujaamua kwenda. Bado una wasiwasi na safari yako.
Kama una Mtu anasema anakupenda nenda kamuulize swali hili “Upo tayari kupoteza nini ili ubaki na mimi”
Wewe mwenyewe jiulize kama una kitu unakipenda upo tayari kupoteza vitu gani ili upate kile unachokipenda?
Lipa gharama Upate kile unachokipenda.