Habari rafiki karibu tena siku ya leo tujifunze kwa pamoja mambo matano niliyojifunza siku ya leo. Nina amini unaendelea vyema na mafanikio.

  1.      Hatuongozwi na msukumo wa kitu kimoja.

Kwenye dunia ya sasa kila mtu anafanya jambo analolifanya kwasababu yake binafsi. Inawezekana wewe unatafuta pesa kwa namna yeyote ile ili ubadilishe hali mbaya ya familia yenu. Mwingine inawezekana anafanya namna yeyote ili awaonyeshe wale waliomwambia yeye hawezi. Mwingine anafanya kile anachokifanya kwasababu ndio kilichomleta duniani. Hashindani na mtu na wala hakuna mtu anaweza kuja kumtoa. Wewe unaweza kukazana kutumia muda wako na nguvu zako kumlazimisha mtu afanye kile anachokifanya kwasababu yako wewe lakini ukashindwa kabisa. Hii ni kwasababu nguvu iliyopo ndani yake ni kubwa sana.

Kitu kimoja ambacho naweza kukushauri ni kwamba simamia kile unachokiamini hakuna wa kuja kukukatisha tamaa. Hakuna ambaye utaweza kuja kulinganisha nae ili uone kama unachokifanya ni sahihi au sio sahihi. Hakuna ambae unaweza kusema unashindana nae.

Kila mmoja ana wito wake. Kila mmoja anayosababu inayomfanya afanye kile anachokifanya. Kikubwa uwe unapata Amani ya moyo wakati unafanya hilo unalolifanya na sio kuwafurahisha wengine.

  

  1.  Usikubali kuwa mmoja wa wakatisha tamaa.

Katika maneno unayoongea kila siku angalia kwa namna moja ama nyingine kama yanakwenda kuponya au kuharibu. Neno lolote linalotoka linakuwa na kazi mbili kuponya na kuharibu. Mara nyingine unaweza kujikuta unazungumza maneno ambayo unadhani kwa mtazamo wako unasaidia kumbe kuna mioyo ya watu unaiharibu. Hivyo ni muhimu ukawa makini sana usije kuwa mkatisha tamaa wa kazi ambazo ni njema sana hapa duniani. Kuna watu wanaona baa nyingi na klabu za usiku zinaanzishwa hawazitazami wala kusema lolote lakini utasikia mtu analalamika kuanzishwa kwa makanisa mengi.

Ni kweli inawezekana wanaonzisha wana nia tofauti ya uanzishaji tofauti na inavyokusudiwa lakini ukishasema kwa pamoja siku hizi kila mtu anaanzisha kanisa unakuwa unakosea. Kama kuna wanaokosea waseme wanaokosea usijumuishe wote.

  1.  Mungu pekee ndie mpimaji wa kazi zetu.

Kwa lolote unalolifanya haijalishi upo kwenye dini gani au huamini dini yeyote nataka nikwambie hujajileta duniani mwenyewe. Hujajizaa mwenyewe. Unachokifanya hujajipa mamlaka yakukifanya wewe mwenyewe. Sio binadamu aliamua wewe uzaliwe. Sio binadamu alikupa ufanye hiyo kazi njema inayogusa maisha ya watu. Ni muhimu sana ukafanya kwa bidii sana kwasababu aliekutuma anakutazama.

Wote unaojaribu kujipima nao ili useme umefanikiwa au lah unakosea. Hao ni mifano tu wewe unaweza kuja kuwa mfano wa kipekee. Bado unaweza kwenda mbali Zaidi ya mtu yeyote aliewahi kutokea hapa duniani. Wote waliokutangulia watumie kama mfano na sio kama kipimo. Anaepima ni Mungu muumbaji alitutuma tufanye kazi yake. Akiamua kusema basi imetosha unaweza kuondoka hujafikia popote pale ulipokuwa unataka kufika.

  1.  Tupo Hapa duniani ili Kushinda.

Mwanajeshi anaenda vitani ili kuleta ushindi. Mchezaji anakwenda uwanjani ili ashinde sio acheze tu. Vivyo hivyo upo hapa unafanya kile unachokifanya ili ushinde. Tunaposema kushinda hatushindani na wengine wanaofanya vitu tunavyofanya. Tupo ili kushinda changamoto, maneno ya watu, vizuizi vya namna mbalimbali. Ili kufikia picha yetu kubwa. Usiwe sababu ya mwingine kushindwa.

Vitani ili ushindi upatikane lazima upande mmoja ushindwe, lazima wengine wauwawe au wakubali kushindwa. Kwenye mpira ili ushindi upatikane lazima timu moja ifungwe goli Zaidi ya mwenzake. Lakini sisi tunashinda wote kwa pamoja sio kwa kushindana. Usiwe na roho ya kufurahi unapomuona mwenzako anakwama.

  1.  Kuonekana wa Tofauti Tafuta Tofauti yako.

Kwasababu unachokifanya kuna mtu mwingine anakifanya ili uweze kuonekana na wewe lazima ujue tofauti yako. Kama huna tofauti na wengine utapotea katikati yao. Anza leo kuangalia wewe ni kitu gani kinakuweka tofauti na wenzako mnaofanya vitu vinavyofanana.

Tumia nguvu nyingi Zaidi kwenye tofauti yako. Ulipo utofauti wako ndipo ushindi wako ulipo. Watu wengi watavutwa na utofauti wako. Hivyo tumia nguvu nyingi hadi ule utofauti wako uanze kuonekana.

Ni mimi Rafiki Yako,

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.

 

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio Hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog Bonyeza hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Karibu Kwenye Kundi Maalumu la WhatsApp https://jacobmushi.com/whatsapp/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading