473; Mawazo Ya Mungu Si Kama Ya Mwanadamu.

jacobmushi
2 Min Read

Kuna namna ambavyo wanadamu tumekuwa tunajaribu kumtafsiri Mungu katika uelewa wetu kitu ambacho tunasahau ni kwamba uelewa wetu bado ni wa kibinadamu. Hivyo kwa vyovyote bado tunamtafsiri Mungu kwa viwango vyetu.

Kama Upumbavu wa Mungu ndio hekima ya mwanadamu basi sisi hatuwezi kusema sana juu yake kwasababu bado tutakuwa tunakosea. Yeye aliumba miti ya matunda ambayo inajitengenezea mbolea yenyewe, lakini mwanadamu akaja kutengeneza mbolea ya kisasa ambavyo inamletea magonjwa yeye mwenyewe.

Nataka ujifunze kidogo kuhusu huyu Mungu, kwasababu alisema alituumba kwa mfano wake embu jiulize wewe ni mfano wa Mungu kweli? Kama yeye aliumba Mti mara moja na hadi sasa miti ipo kila mahali duniani, hajawahi kurudia tena kuumba miti.

Kila alichokifanya yeye hajawahi kurudia mara ya pili wala kurekebisha. Sasa jiulize wewe una mfano wa Mungu? Kwenye maisha yako ya kawaida tu jitazame ni vitu vingapi ambavyo umevitengeneza ambavyo vinaweza kujizalisha vyenyewe? Je ni biashara, ni fedha umewekeza, ni kitabu umeandika?

Mungu ndio mwekezaji wa kwanza ambaye tunapaswa kujifunza kwake. Alivyoiumba dunia ni katika namna ya uwekezaji. Kaumba bahari ndani yake kaweka samaki ili binadamu aje kula na kuishi, kaumba misitu kaweka wanyama, matunda na mazao ili binadamu atumie kama chakula.

Wewe kama mfano wa Mungu kwa dunia ya sasa ambayo karibu kila kitu kinahitaji pesa umejiandaa kufanya uwekezaji wa namna gani? Ni vitu gani hasa utavifanya ili viendelee kukupa pesa kila wakati hata kama hautakuwepo? Ni vizuri ukajiuliza kwasababu leo na kesho hizo nguvu ulizonazo hazitakuwepo. Muda ulionao sasa utakuwa mchache sana, jifunze kufanya kwa mfano wa Mungu. Jitengenezee mifumo ambayo itadumu kwa muda mrefu.

Nataka ubadili mtazamo wako uanze kuwa na mtazamo wa kimungu ndani yako, usitafute pesa ya kula bali tafuta kujenga mifumo ambayo itakuletea pesa za kula hata wakati ambao hufanyi kazi. Usiishi kwa ajili ya leo fanya yale mambo ambayo unajua kabisa miaka 10 ijayo nitakuwa na muda wa kuishi katika namna ya kumpendeza Mungu.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi

www.jacobmushi.com

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
8 Comments

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading