Kuna zile nyakati katika Maisha unakuwa katika kupambana huku na kule ili japo upate namna ya kuweza kuinuka na kufikia hatua Fulani ya Maisha. Sasa kuna changamoto nyingi huwa unapitia na mojawapo ni vile watu wanavyokuchukulia. Katika marafiki zako au ndugu kuna wale ambao kwenye akili zako unaanzaga kuwaweka kama ambao utawategemea hivi.  Huenda ni kwasababu wamepiga hatua Fulani Zaidi yako.

Sasa hawa watu mara nyingi hubadilika tofauti na ulivyotarajia, mfano umeenda kwa mjomba wako umuombe akusaidie ada ambayo imebakia ili tu uweze kupokea cheti chako cha chuo angalau ukaombe kazi. Sasa mjomba ana uwezo kabisa wa kukusaidia kwasababu unajua ameshatoka kimaisha, na hata kama angekosa pesa yeye kama yeye ana uwezo pia wa kuomba kwa marafiki zake ukazipata. Sasa mjomba wako huyo akakugomea kabisa akasema mimi sina uwezo wa kukusaidia sina pesa kabisa. Wewe nenda tu katafute namna nyingine.

Bahati mbaya sana ile hali ilikuumiza sana kwasababu ilisababisha ukose kazi Fulani ambayo uliambiwa upeleke vyeti vyako ambavyo navyo vilikwama kwasababu ya ada uliyochelewa kulipa. Mungu wako ni mkubwa sana sasa hakukuacha katika pitapita zako ukakutana na mtu ambaye hata humjui sana ukamuelezea shida yako akakupa kabisa ile hela na akasema wala usifikirie kumrudishia.

Ukamshukuru sana Mungu na ukalipa ada na kuchukua cheti. Mungu akaendelea kuwa mwema kwako na ile kazi ukapata pia. Maisha yakabadilika sasa wewe uliekuwa unaomba pesa sasa watu wanakuja kwako kukuomba.

Unajua hata wale uliokuwa unawaomba na wakakukazia na kukuona wewe ni msumbufu watakuja waanze kutengeneza urafiki na wewe. Mjomba nae atataka msameheane yaishe muendeleze undugu.

Mimi hapo Rafiki yangu nakushauri kitu kimoja, wasamehe wote kabisa kutoka moyoni. Usiwawekee kinyongo hata kidogo, wakiwa na shida ya pesa au ya chochote ambacho unaona kwa uwezo wako unaweza kuwasaidia wasaidie. Lakini usikubali kuwapa kitu kimoja, tu.

Usikubali wakuzoee sana, usikubali wakujue sana kama marafiki zako, usiwape nafasi za kuwa marafiki zako kwasababu wanaweza kukuangamiza dakika moja. Na unapofanya hivyo najua watasema unaringa, hauongei nao kama zamani kiukweli usibabaike sana na maneno yao kwasababu yatakufanya uje kujuta siku moja.

Unajua Rafiki wa kweli ni yule wa shida na raha. Kama mtu hakuthubutu hata kukupa maneno ya kukutia moyo wakati una shida basi ni rahisi sana kwenda kusema maneno ya uongo ili tu upoteze kila kitu ulichonacho. Kwa kifupi sio kila unaemsamehe anapaswa kurudi kwenye nafasi ile aliyokuwa nayo zamani kwenye Maisha yako.

Wengine ndio walikuwa wanazuia baraka zako. Kuwarudisha ten ani kuziziba baraka zako. Unapoweka umbali nao usiweke kwa chuki moyoni mwako, hakikisha umeshawasamehe kabisa. 

Nakutakia kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

2 Responses

  1. Asante kwa kunitia moyi rafiki, maana watu kama hao wapo na nimekutana nao sana. Mungu akubariki kaka

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading