Hutaweza kufikia kamwe ndoto zako kama wewe ni mtu ambaye unasubiria tukio Fulani litokee ndipo uchukue hatua. Kama Maisha yako yatakuwa yanaendeshwa na matukio bila ya mipango huwezi kwenda mbele.

Badala ya kusubiria tukio ndio likusukume kuchukua hatua anza kuchukua hatua sasa hivi. Hilo unalodhani litatokea kinaweza lisitokee kweli. Wanadamu wanaweza kutabiri mwaka huu mvua zitakuwa za shida sana. Sasa huo ni utabiri kama utasubiri utabiri ndio uanze kupanda mazao utajikuta unapoteza mengi sana.

Kitu ambacho unapaswa utambue ni kwamba matukio yanayotokea nje yakow ewe huna nguvu kubwa ya kuyadhibiti hivyo mwisho wa siku utakuja kuyatumia kama sababu ya kujitetea tu. Panga Maisha yako kabla hujapangwa na matukio.

Kuna msemo unasema usipojipanga utapangwa. Usipojitengenezea mfumo mzuri wa mazoezi ugonjwa utakuja kukutengenezea. Usipoweka akiba umaskini utakuja kukufundisha. Siku ukiwa na uhitaji mkubwa sana wa pesa ndipo utakumbuka kuweka akiba.

Rafiki yangu ngoja nikwambie ukweli, watu wengi hawapendi kuchukua hatua hadi pale mambo yanapokuwa mabaya. Yaani mpaka ufukuzwe kazi ndipo unakumbuka kufanya biashara. Hadi upate tatizo ndipo unakumbuka kuchukua hatua.

Usiwe mtu wa aina hii tengeneza Maisha yako. usikubali mipango ya watu wengine ndio ikuchukue. Unajua kama huna ratiba zako watatokea watu wenye ratiba zao na watakualika uende kutekeleza kile walichokuwa wamekipanga muda mrefu sana.

Kama huna unapoelekea utajikuta unawafuata watu wanaojua wanapoelekea. Kama wamepotea njia na wewe utakuwa umepotea njia.

UFANYEJE?

Jua Kusudi Lako

Anza kujua kwanini upoo duniani leo. Anza kufanyia kazi kile ambacho Mungu ameweka ndani yako. tambua vipaji ambavyo vipo ndani yako.

Tengeneza Maono makubwa ambayo unayafuata.

Kama huna maono ni kwamba huna unaoelekea au kuna watu unawafuata. Haukuzaliwa hapa duniani kwa bahati mbaya kila binadamu ana sababu ya kuwepo hapa. Kila binadamu anatakiwa awe na maono yake. Haijalishi baba yako ni nani bado unatakiwa uwe wewe kama wewe. Utafute pesa zako mwenyewe. Utengeneze jina lako mwenyewe hapa duniani. Hata yeye alikuwa na baba yake.

Soma: MAMBO 5 YANAYOONYESHA UNACHOKIFANYA SIO KUSUDI LAKO

Kuwa na Malengo na Mipango.

Ili usiwe mtu wa matukio lazima uwe na mipango yako binafsi. Lazima uwe na malengo yako binafsi. Na hakikisha watu wote wanayaheshimu malengo na mipango yako. isiwe kuna mtu anaweza kusema hapana au nimekataa. Naamini mpaka unaweza kusoma hapa wewe una umri ambao tayari unajitambua. Sasa ni vyema ukaanza kujifunza taratibu kuwa na umiliki wa Maisha yako. kuna nyakati utakuwa mwenyewe hapa duniani. Utakuwa huna mtu wa kumuuliza ufanye nini. Utatakiwa ufikiri na kuchukua hatua peke yako. Kama hujajiandaa utajikuta unakwama na hujui cha kufanya.

Jua ni wapi anatakiwa afanye Mungu na wapi unatakiwa ufanye wewe. Ukishindwa kutofautisha hivi vitu viwili utakuwa unaishia kungoja muujiza na Mungu anangoja ufanye.

Kipimo cha ukomavu wako ni kiwango cha maamuzi unayoweza kuchukua mwenyewe bila ya kumuuliza mtu mwingine au kuomba ushauri. Kama mambo mengi hasa madogo madogo ambayo ulitakiwa ufikiri na kuchukua hatua badala ya kuchukua hatua unakwenda kuuliza. Inaonyesha ni kiwango gani bado hujakua sawasawa. Fanya maamuzi madogo madogo usiogope kukosea. Watu wengi tunaomba ruhusa kwasababu tunaogopa kukosea.

Ukikosea utajifunza. Kama unaogopa kukosea huwezi kukua hata siku moja. Mtoto mdogo angeogopa kuanguka basi asingekaa atembee. Mtoto mdogo angekuwa akitaka kutembea anakwenda kuomba ruhusa basi ingemchukua muda mrefu sana kuweza kupiga hatua. Sasa lazima ujue ni lipi la kwenda kuomba ruhusa na lipi ni la kufanya mwenyewe.

” Kama umependa Makala Hii Usiache Kuweka Maoni yako Hapa chini”

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio Hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog Bonyeza hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Jacob Mushi,

Mwandishi, Mjasiriamali, Kocha wa Maisha, Mshauri na Mtaalamu wa Blogger ,

Simu: 0654 726 668,

Twitter: jacobmushitz

Instagram: jacobmushi

Facebook: Jacob Mushi Page                                                                   

Barua pepe: jacob@usiishienjiani.com

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading