Tupo kwenye dunia ambayo ni ngumu sana kumjua mtu kwasababu wengi wamevaa mavazi yanayofunika uhalisia wao. Wamevaa tabia za kuigiza ambazo sio za kweli na wala hawana kabisa. Wamevaa Maisha ambayo ni uongo na ndani yake wanateseka huku wakifurahia kuona watu wanawasifia.
Sasa ili uweze kuwavuta watu sahihi na kuwaacha hawa waliojivalisha mavazi ya uongo ili kufunika ule uhalisia wao inakupasa wewe uwe HALISI. Hakuna njia nyingine ukishaanza kuwa wewe, ukavaa vile unavyopenda na sio jamii inavyokulazimisha ukaishi Maisha ambayo wewe binafsi ndio unayataka kulingana na kipato chako. Ukaanza kuishi kile kilichopo ndani yako na kuisimamia haki na ukweli utawakimbiza kabisa watu wanafiki na kuwaacha watu sahihi ambao watakupenda kwa jinsi ulivyo.
Nimewahi kukutana na mtu ananiambia Jacob wewe ni mtu mkubwa sana, unapaswa uwe unavaa suti ili watu wakikuona wakuheshimu. Nilicheka nikamwambia kama mtu anataka kunikubali kwasababu nimevaa suti wapo wengi sana wanaovaa suti aende akawakubali hao. Kama mtu hawezi kunikubali kwa vile nilivyo na kile ambacho ninapenda mimi siwezi kufanya jambo lolote kumlazimisha akubaliane na mimi. Naamini pia ni sawa kabisa watu wasiponikubali, naamini hawawezi kunikubali wote na pia hawawezi kunikataa wote.
Usiishi Maisha ambayo yanaendeshwa kwa maoni ya wengine, usiishie kufuata kila ambacho watu wanataka ufanye utageuka kuwa mtumwa wao. Utakuwa ni mtu unaewaridhisha wengine huku moyo wako unaumia kwasababu hufanyi kile unachokipenda.
Ili uwavute watu sahihi kwenye Maisha yako amua sasa kuanza kuishi Maisha yako halisi. Vile ambavyo wewe unaona ni sahihi lakini ukumbuke tu usivunje sharia na wala usiende katika yale yaliyoko nje ya UADILIFU. Kwa kifupi fanya kile moyo wako unataka lakini kisiwe cha kumuumiza mtu mwingine, kisiwe sababu ya kumfanya mwingine atoke machozi.
Wavute watu sahihi kwa kufanya vitu sahihi ambavyo ulizaliwa kuja kufanya hapa duniani. Anza na kuishi lile kusudi la wewe kuja hapa duniani na utaanza kuwaona watu sahihi kwenye Maisha yako. Usiendelee kupoteza muda wako kufuata yale ambayo yametengenezwa na jamii badala yake ishi kile ambacho Mungu ameweka ndani yako.
Jiunge na Mtandao wetu uwe unapokea makala hizi moja kwa moja kwenye email yako. Mwishoni mwa makala hii kuna sehemu ya kuweka email na chini yake pameandikwa Subsrcibe. Weka email kisha Bonyeza Subscribe.
Ubarikiwe sana,
Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi