Habari Rafiki,  natumaini unaendelea vyema.  Pole na majukumu mbalimbali ya kutimiza kile kinachokufanya uwepo hapa duniani.

Leo tunakwenda kutazama Nguvu ya Taarifa Juu ya Maono na Ndoto  zetu.  Kama tunavyojua katika ulimwengu wa sasa mawasiliano yamekua rahisi sana.  Na hii imeletwa na mapinduzi ya teknolojia yanayoendelea kuvumbuliwa kila siku.  Ninafurahishwa sana na teknolojia mpya zinazotokea duniani kipindi hiki.  Ninafurahi mno kuzaliwa nyakati hizi.

Pamoja na yote hayo teknolojia imerahisisha sana upatikanaji wa taarifa. Miaka michache iliyopita ulikua ukitaka kuzungumza na watu jambo na wakusikie wengi ni hadi uende kwenye Tv au Radio. Lakini kwa sasa unaweza kuwafikia maelfu ya watu ndani ya siku moja kwa kupitia mitandao ya kijamii. Sasa hivi tunaweza kujifunza mambo mengi sana kupitia mitandao hii.


Soma : TAARIFA

Taarifa zimegawanyika katika makundi makuu mawili.  Kundi la kwanza ni Taarifa Hasi na la pili ni Taarifa Chanya. Vipo vyanzo mbalimbali vya Taarifa hizi ikiwepo,  Tv,  Radio, Marafiki,  Vitabu unavyosoma, Mitandao ya Kijamii na nyingine nyingi.


Namshukuru Mungu Tabia ya kusoma nilikua nayo Tangu nikiwa mdogo sana. Darasa la tatu nilikua na tabia ya kusoma magazeti, Vitabu vya Hadithi, na Biblia. Nimesoma vitu vingi sana na vingine vilikua havinifai kutokana na umri wangu kua mdogo. Nikiwa shule ya Msingi tayari nilishafahamu vitu vingi mno katika nyanja mbalimbali. Kitu kilichoniokoa ni kwamba nilikua nasoma Biblia la sivyo ningeharibikiwa sana. 

Matokeo ya Taarifa nyingi nilizoingiza kwenye akili yangu kipindi hicho bado nayaona yakiathiri maisha yangu kwa sasa.

 Ni hatari sana kusoma au kuona jambo baya ambalo hujawahi kulifanya. Ni lazima utatafuta njia ukajaribu. 


(a) Nguvu ya Taarifa Hasi


Taarifa hasi zina mchango mkubwa sana katika kuharibu maono na Ndoto ulizonazo. Kwasababu zitakua zimejaa kwenye ubongo wako. Zitasababisha uone giza ushindwe kufanya mambo yanayokusogeza mbele. 

Unaweza kuchukulia ni kitu cha kawaida kwakua Matokeo yake huyaoni muda huo huo. 


Taarifa Hasi zinaleta Hofu. 

Zinakufanya uone kushindwa,  ujisikie kuchoka wakati mwingine. 

Zinakufanya uone giza. 

Zinaondoa au kufuta kabisa ile ndoto yako. 


Kama wewe ni mwimbaji na unatamani Tanzania ikujue kutokana na uimbaji wako.  Kisha kichwani kwako umejaza mambo hasi juu ya uimbaji. Juu ya rushwa, upendeleo, freemason na mengine mengi. Ukweli ni kwamba utakata tamaa na kushindwa kufikia ndoto yako. 

Makundi unayokaa nayo hawachangii chochote juu ya uimbaji wako. Lazima utakwama. 

Vipindi unavyotazama havichangii chochote juu ya uimbaji. Huwezi kuwa mbunifu. Utapoteza ile zawadi iliyopo ndani yako. 


Taarifa hasi ni sawa na sumu inayoua pole pole.  Ni kidogo sana lakini inakuletea madhara makubwa baadae. 


SOMA: MAMBO 7 YATAKAYOFANYA UPOTEZE YOTE UNAYOYATAFUTA


(b) Taarifa Chanya. 

Taarifa chanya zipo nyingi mno pia. Waalimu wanaofundisha tupo wengi pia. Lakini huwezi pia kula kila chakula Kwasababu kinafaa kuingia tumboni. Lazima ujue unahitaji chakula cha aina gani ili uwe na afya bora.


Kama wewe tayari ni muathirika wa taarifa mbaya utahitaji ule vyakula vingi hadi vijae ndani ya ubongo wako. Kama tayari upo kwenye mstari unatakiwa ujue ni wapi kwa kujifunza na ni Taarifa gani ya kutafuta na hii inatokana na maono yako na ndoto zako. 

Ni ngumu sana kunikuta mimi nipo kwenye kundi la wasap la Waimbaji wa Gospel. Lakini ndani ya Gospel Music Group hakuna taarifa hasi zipo chanya nyingi mno. Lakini sitazitumia katika maono yangu. Jua ni kitu gani unafanya ili ujue ni watu gani unawahitaji.


Waimbaji wakikaa pamoja watatiana moyo katika uimbaji wao. Na kushirikishana changamoto wanazopitia. Na vilevile waandishi, na wengine.  Simaanishi uache kujichanganya na wengine naamanisha pale unapochukua chakula cha ubongo wako. Ndio maana vyakula vya mzazi, mgonjwa na mtu mzima vitanatofautiana.  Haiwezekani wewe mtu mzima uwe unapikiwa chakula cha wagonjwa. 

Hivyo hivyo katika taarifa sio kila taarifa chanya unaihitaji. Kitu cha muhimu ni wewe kujua viwango au kiasi cha taarifa unayotaka kutokana na maono na Ndoto yako. Tengeneza mlo kamili wa taarifa.

Kuna wakati unahitaji kutiwa moyo, kuna wakati wa kufarijiwa,  kuna wakati wa kuonywa.  Wakati wa kutiwa moyo haufai kuonywa. 

Kila unachokiweka ndani ya akili yako kina Matokeo.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Jiunge na Usiishie Njiani Academy Hapa https://jacobmushi.com/academy/

Huduma Zetu https://jacobmushi.com/huduma/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading